Na Seif Mangwangi
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa umesema hospitali hiyo haina upungufu wa vifaa tiba na dawa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter.
Hivi karibu kumekuwepo na taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikieleza hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa na madawa hali iliyosababisha wauguzi kuwakataa akina mama wanaoenda kujifungua hospitalini hapo wakiwa hawana vifaa kama mipira ya plastiki (gloves) na mikasi na kuwalazimu akina mama hao kwenda kununua vifaa hivyo katika maduka binafsi.
Moja ya picha hizo zinazosambaa mtandaoni ni ile yenye nembo ya blogu ya Dar Mpya ambayo imebeba madai hayo.
Habari hiyo inaweza kuwa ni uzushi kutokana na kutokuwa na vielelezo muhimu ili kuifanya kuwa halali ikiwemo majina ya akina mama iliyowahoji ambao ndiyo waathirika wa tukio hilo na uthibitisho kutoka kwa uongozi wa hospitali au wauguzi wanaodaiwa kuwarejesha nyumbani kina mama wanaokosa vifaa hivyo au takwimu za upungufu iliyodai.
Hata hivyo, tayari uongozi wa hospitali hiyo umetoa taarifa ukipinga madai hayo.
Mganga mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt Alfred Laison Mwakalebela amesema dawa na vifaa vya tiba vipo vya kutosha kwa asilimia 98 na hakuna upungufu kama inavyodaiwa.
Pia mtandao wa www.arushapressclub.blogspot.com ulifanikiwa kuzungumza kwa njia ya simu na baadhi ya wagonjwa wakazi wa Iringa hususani kina mama wanaopata tiba katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa ambao walikanusha taarifa za kutakiwa kununua vifaa tiba kama gloves na mikasi na dawa.
“Mimi mtoto wangu wa pili Queen mwenye umri wa mwezi mmoja na wiki mbili sasa nilijifungulia hospitali ya Mkoa wa Iringa na sijawahi kutakiwa kupeleka gloves na mkasi au kukosa dawa, lakini pia kliniki nimekuwa nikipeleka mtoto wangu hapo hapo hospitalini na sijawahi kutozwa pesa yoyote,”anasema Haika Mguruta anayefanyakazi kitengo cha biashara katika kampuni ya Tigo mkoani Iringa.
Francis Godwin ni mwandishi wa habari mkoani Iringa ambae na yeye kwa upande wake anaeleza kuwa pamoja na kwamba mke wake anatarajia kujifungua hivi karibuni, amekuwa akihudhuria kliniki katika hospitali hiyo na hajawahi kudaiwa kulipa chochote na mke wake amekuwa akipewa dawa ikiwemo za kuongeza damu bila malipo.
Kuna umuhimu wa wanahabari kuthibitisha habari kabla ya kuitoa jambo litakalosaidia kupunguza uzushi unaosambaa mtandaoni.