Hotuba ya waziri wa viwanda na biashara mhe.bashungwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2020/2021

Waziri wa Viwanda na Biashara
Mhe.Innocent Bashungwa,akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya
Fedha kwa mwaka 2020/2021 bungeni jijini Dodoma.
 1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika; kutokana na
taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ambayo ilichambua
Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara Fungu 44 (Viwanda) na Fungu 60
(Biashara) tarehe 24 na 25 Machi, 2020 Jijini Dodoma, naomba kutoa hoja
kwamba Bunge lako tukufu sasa likubali kupokea na kujadili taarifa ya
utekelezaji wa Mipango na Bajeti kwa Mwaka 2019/2020. Aidha, naliomba
Bunge lako tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Fedha kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka 2020/2021. 
Mheshimiwa Spika, naomba Hotuba
yangu yote iliyowasilishwa kwa Waheshimiwa Wabunge iweze kuingia katika
kumbukumbu za Bunge (Hansard) kama ilivyo. 
Mheshimiwa Spika; awali ya yote
naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na baraka
katika majukumu niliyokasimiwa. Kwa namna ya pekee namshukuru sana
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Waziri na kunipa majukumu yanayobeba
ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Nampongeza kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC na namna
anavyoshughulikia masuala ya biashara katika nchi za SADC na EAC ikiwa
ni pamoja na kuomba kufutiwa madeni kwa nchi za Afrika katika kipindi
hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa COVID -19. Nampongeza pia kwa namna
anavyotuongoza kwa ujasiri na misingi imara, yenye kusheheni uzalendo na
mapenzi kwa nchi yetu. Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; na Mheshimiwa Mheshimiwa Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
kwa jinsi wanavyomsaidia Mhe. Rais kusimamia ipasavyo misingi ya utaifa
wetu kupunguza pengo la walionacho na wasiokuwa nacho, kujenga Tanzania
yenye kutoa fursa za uhakika za kujiletea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja
na Taifa kwa ujumla. 
Mheshimiwa Spika; napenda kuchukua
nafasi hii, kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika kwa umakini wenu
katika kuliongoza na kulisimamia Bunge letu. Pia, naipongeza na
kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira,
chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Suleiman Ahmed Saddiq, Mbunge wa
Jimbo la Mvomero, Makamu wake Mheshimiwa Kanali Mstaafu Ali Khamis
Masoud, Mbunge wa Jimbo la Mfenesini na Waheshimiwa Wajumbe wote wa
Kamati. Ushauri na maelekezo yao 
yamekuwa chachu muhimu sana,
katika mageuzi ya kifikra na kiutendaji ya Wizara, na hivyo kuchochea
kasi ya maendeleo ya viwanda na biashara nchini. 
Mheshimiwa Spika; kwa namna ya
pekee, niwashukuru watangulizi wangu Mheshimiwa Charles John Mwijage,
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini na Mheshimiwa Joseph George Kakunda,
Mbunge wa Jimbo la Sikonge, waliokuwa mawaziri wa Viwanda na Biashara.
Nikiri kuwa misingi waliyoweka imeendelea kuwa chachu muhimu katika
kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara nchini. Aidha, nimshukuru Katibu
Mkuu mstaafu Prof. Joseph Buchweshaija kwa ushirikiano alionipa kipindi
nilichofanya naye kazi na nimkaribishe Prof. Riziki Shemdoe Katibu Mkuu
wetu mpya. Nampongeza Prof. Shemdoe kwa nguvu na kasi aliyokuja nayo
kwenye Wizara. 
Mheshimiwa Spika; niwapongeze pia
Mhe. Mussa Zungu, Mbunge wa Ilala, Mhe. Geogre Simbachawene, Mbunge wa
Kibakwe na Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi kwa
kuaminiwa na Mhe. Rais na kuteuliwa kuwa Mawaziri. Naahidi kuendelea
kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kutimiza majukumu yao. 
Mheshimiwa Spika; naungana pia na
Waheshimiwa Wabunge kutoa pole kwa familia zilizoondokewa na Wabunge
wenzetu ambao ni Mheshimiwa Rashid Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la
Newala Vijijini; Mheshimiwa Dkt. Getrude Rwakatare aliyekuwa Mbunge wa
Viti Maalum; Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Sumve;
na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustino Mahiga aliyekuwa Mbunge wa
Kuteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria. 
Mheshimiwa Spika; naomba kutumia
fursa hii pia kuwashukuru viongozi na watendaji wote wa sekta binafsi,
kwa michango yao katika kuendeleza Sekta za Viwanda na Biashara.
Nawashukuru TPSF, CTI, TCCIA, TNBC, CEO Roundtable, JWT na wengine
wengi. Tunaendelea kuwategemea kama nguzo na mihimili ya kushirikiana
katika kuendeleza viwanda na biashara na kuchochea uchumi wetu kwa
ujumla. 
Mheshimiwa Spika; hotuba hii ya
Bajeti ninayoiwasilisha leo ni matokeo ya uratibu na ushirikiano mzuri
wa viongozi wenzangu katika Wizara, akiwemo Naibu Waziri Mheshimiwa
Mhandisi Stella Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa; Katibu Mkuu, Prof.
Riziki Shemdoe; Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Ludovick Nduhiye; Wakuu wa
Idara, Vitengo, Taasisi na Watumishi wote wa Wizara na Taasisi. Napenda
kuwashukuru na kuwapongeza kwa kujituma, na kuonesha daima utayari wa
kuboresha mbinu na mikakati ya kisekta kwa vitendo. 
Mheshimiwa Spika; nawapongeza na
kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Karagwe kwa kuendelea kunipa
ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kitaifa na ya Jimbo.
Nawapongeza kwa namna wanavyojibidiisha katika kujiletea maendeleo.
Aidha, ninawaahidi kwamba nitaendelea kutetea maslahi yenu hapa Bungeni
na hata nje ya Bunge ili kuhakikisha Karagwe inaendelea kushamiri na
kuleta matokeo ya mtu mmoja mmoja, Wilaya, Mkoa na hatimaye kuongeza
mchango wake kwa Taifa letu. Kipekee namshukuru sana mke wangu mpendwa
Jennifer Bashungwa, watoto na familia yangu kwa upendo wao, uvumilivu na
maombi yao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ya kitaifa. 
Mheshimiwa Spika; naomba niungane
na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuomba ushiriki wa dhati wa kila
Mtanzania katika kupambana na virusi vya KORONA ili kulinda nguvukazi ya
Taifa. Nawaomba sana Watanzania wote kuwa kila mmoja, kila familia na
jumuiya zote nchini, kutambua kuwa usalama wetu hutegemea jitihada ya
kila mmoja kujilinda na kumlinda mwenzake. 
Mheshimiwa Spika; katika
kukabiliana na janga la ugonjwa wa KORONA, Kampuni ya Kilombero
Sugar ilichangia jumla ya lita 30,000 za Ethanol kwa ajili ya
kutengeneza vitakasa mikono ambapo Wizara ya Afya ilipewa lita 20,000 na
kiasi kilichobaki cha kita 10,000 zilipewa Taasisi za SIDO na TIRDO. 
Mheshimiwa Spika; hadi sasa tayari
Viwanda na Makampuni 65 yanazalisha vitakasa mikono vyenye ubora
unaokubalika na TMDA. Kwa Wastani Viwanda hivyo vinatumia kiasi
cha Ethanol kwa mwezi kisichopungua lita 2,548,951. Umoja wa wenye
Viwanda Vya Dawa na Vifaa Tiba (TMPA) kwa ujumla wao (viwanda vikubwa 4)
vinazalisha vitakasa mikono kwa mwezi lita zipatazo 900,000 na viwanda
vya kati na vidogo vipatavyo 61, vinazalisha lita zipatazo 2,745,000 za
vitasa mikono kwa mwezi, na kufanya jumla ya uzalishaji vitakasa mikono
kuwa lita 3,645,000 kila mwezi. Kati ya hizo TIRDO huzalisha
lita 90,000 kwa mwezi na SIDO huzalisha lita 18,000. 
Mheshimiwa Spika; kwa sasa tuna
viwanda viwili vya kutengeneza barakoa aina ya Surgical Masks ambavyo
ni Pristine na Five Star. Viwanda hivyo vina uwezo uliosimikwa wa
kutengeneza barakoa 150,000 kwa siku na uwezo wa uzalishaji kwa sasa ni
barakoa 30,000 kwa kiwanda cha Pristine na barakoa 40,000 kwa kiwanda
cha Five Star kwa siku. Aidha, barakoa za vitambaa (cloth masks) kwa
ajili ya kujikinga, tayari jumla ya viwanda 123 vimeitikia wito wa
kutengeneza barakoa hizo ambapo kati yao viwanda vikubwa ni 13 na vidogo
110. Wizara inaendelea kuhamasiha viwanda vya ndani vya nguo
kutengeneza barakoa kwa wingi kuwasaidia watanzania na mapambano ya
KORONA. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zetu kuhamasisha na
mafundi vyerehani kwenye kila kijiji kushona barakoa za nguo kuwasaidia 
wananchi vijijini. TMDA na TBS
toeni mafunzo kupitia vyombo vya habari na wapeni ushirikiano Wakuu wa
Mikoa na Wilaya katika majukumu haya. 
 1. MAFANIKIO YA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA
AWAMU YA TANO
Mheshimiwa Spika; katika kipindi
cha kwanza cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali iliweka
nguvu kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi 2015 – 2020. Umakini wa utekelezaji Ilani ya CCM
umehamasisha na kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufikia
malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa 2025. 2.1
Kukidhi Mahitaji ya Ndani ya Bidhaa za Viwandani
Mheshimiwa Spika; Nchi yetu
imejitosheleza katika baadhi ya bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini.
Saruji (uzalishaji halisi ni tani Milioni 7.4 na mahitaji halisi tani
Milioni 4.8); marumaru (uzalishaji halisi ni mita za mraba Milioni 32.4
na mahitaji halisi ni wastani wa mita za mraba Milioni 30). 
2.2 Ujenzi wa Viwanda Vipya
Mheshimiwa Spika; Serikali
inaendelea kuhamasisha uendelezaji na ujenzi wa viwanda nchini. Kutokana
na uhamasishaji huo, jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa kati ya
mwaka 2015 hadi 2019. Viwanda hivyo vinajumuisha, viwanda 201 vikubwa,
460 vya kati, 3,406 vidogo; na 4,410 vidogo sana. 
Mheshimiwa Spika; Sekta ya Viwanda
Vidogo na Biashara Ndogo imetoa ajira kwa wingi kwa Watanzania ambapo
kwa sasa inaajiri zaidi ya Watanzania 8,000,000. Ajira hizo zimewezesha
wananchi kujiongezea vipato na kutatua changamoto zao za kijamii na
kiuchumi. Hii imetokea kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuweka
mazingira wezeshi ikiwemo kupunguza mamlaka za udhibiti na kufanya
watanzania wengi kujiajiri na kutekeleza azma ya ujenzi wa viwanda
nchini ambapo takribani asilimia 99 ya viwanda vyote nchini vipo chini
ya sekta hiyo. 
2.3 Uzalishaji wa Dawa na Vifaa Tiba
Mheshimiwa Spika; Sekta ya Viwanda
vya Dawa na Vifaa Tiba kwa sasa ina jumla ya viwanda 15 ambapo viwanda
12 vinatengeneza dawa za binadamu, viwanda 2 ni vya dawa za mifugo na
kiwanda 1 kinatengeneza vifaa tiba. Kwa sasa viwanda vya dawa
vinazalisha chini ya asilimia 12 ya uwezo wake uliosimikwa na Serikali
imekuwa ikiwawekea wawekezaji 
mazingira wezeshi ili kufikia
asilimia 60 ya uwezo uliosimikwa. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na
kuweka vivutio vya uwekezaji kwa lengo la kuhamasisha wawekezaji wa
ndani na Nje ya Nchi kwa kuondoa VAT kwa vifungashio vya dawa
zinazozalishwa nje na ndani ya nchi; kushusha kodi ya mapato kutoka
asilimia 30 hadi 20 kwa mwekezaji mpya ndani ya miaka mitatu ya mwanzo;
na kuweka upendeleo maalum kwa ununuzi wa dawa zinazozalishwa na viwanda
vya ndani kupitia MSD. 
2.4 Uzalishaji wa Sukari
Mheshimiwa Spika; makadirio ya
uzalishaji wa sukari kwa msimu wa mwaka 2019/2020 yalikuwa tani 345,296
kwa viwanda vya ndani sawa na asilimia 73.46 ya kiasi cha sukari
inayokadiriwa kwa matumizi ya kawaida. Aidha, hadi kufikia mwezi Aprili,
2020 uzalishaji wa sukari nchini ulikuwa jumla ya tani 298,949, wakati
mahitaji ya sukari kwa mwaka ni wastani wa tani 635,000. Kati ya
mahitaji hayo, tani 470,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na tani
165,000 kwa matumizi ya viwandani. Makadirio hayo yametokana na ukweli
kwamba mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida kwa mwezi ni wastani wa
tani 38,000. Sababu zilipelekea kushuka kwa bei ni pamoja na mvua
nyingi kipindi cha vuli na kupunguza kiwango cha sukari kwenye miwa na
taratibu za usafirishaji ambazo zimesababishwa na ugonjwa wa KORONA
ulioenea duniani. 
Mheshimiwa Spika; kwa sasa
Serikali imetoa tamko kuhusu uuzaji wa sukari. Matamko hayo ni pamoja na
sukari iuzwe kwa kuzingatia bei elekezi na endapo wafanyabiashara
hawatazingatia maelekezo hayo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Napenda kuwapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao tumeshuhudia jitihada
zao katika kusimamia tamko la bei elekezi kwa lengo la kuwalinda
walaji. Aiidha, niwaombe Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kwa
kutumia kamati za ulinzi na usalama kuendelea kusimamia bei za ukomo
zilizotangazwa na Serikali ili wananchi waweze kupata bidhaa hii muhimu
kwa bei nafuu. 
2.5 Uendelezaji Maeneo Maalum ya Uwekezaji na Mapato
Kutokana na Uwekezaji Chini ya EPZA/SEZ
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia
EPZA, imefanya tafiti tatu kutathmini tija inayopatikana kutokana na
kampuni zilizowekeza chini ya EPZA na tafiti hizo zimeonesha uwepo wa
tija katika uwekezaji wa maeneo hayo. Hadi kufikia Desemba 2019, chini
ya BWM-SEZ, mauzo ya Nje ya Nchi yameingizia nchi Tsh. Bilioni 293.56
(USD 127.64); matumizi mengine ya kuendeshea biashara yameingiza Tsh.
Bilioni 146.58 (USD 63.73); kodi na tozo mbalimbali zilizolipwa kupitia
TRA zimeingiza Tsh. Bilioni 17.24 (USD 7.50); na zimepatikana ajira za
moja kwa moja viwandani zipatazo 3,000. 
Kutokana na manufaa hayo, Wizara
kupitia EPZA, imekuwa ikihamasisha ushiriki wa Serikali za Mikoa katika
uendelezaji wa Maeneo ya SEZ ili kuiwezesha Mikoa husika kutumia Maeneo
ya SEZ kama chanzo cha mapato na mbinu mojawapo ya kuchochea shughuli za
kiuchumi katika mikoa husika. Hadi sasa, mikoa ya Arusha, Geita,
Mwanza, Kigoma na Songwe imetenga maeneo yatakayoendelezwa kama Maeneo
Maalum ya Kiuchumi. Kupitia uhamasishaji huo, katika kipindi cha mwaka
2019/2020 EPZA imesajili kampuni sita (06) na hivyo kufanya viwanda
vilivyo chini ya EPZA kuongezeka kutoka viwanda 163 hadi viwanda 169
vikichangia ongezeko la mtaji unaokadiriwa kutoka Tsh. Tilioni 5.41 (USD
Bilioni 2.35) hadi Tsh. Tilioni 5.47 (USD Bilioni 2.38). Mauzo ya nje
yanakadiriwa kuongezeka kutoka Tsh. Trilioni 5.17 (USD Bilioni 2.25)
hadi takriban Tsh. Trilioni 5.21 (USD Bilioni 2.27) na fursa za ajira za
moja kwa moja kutoka 56,442 hadi 57,342. 
Mheshimiwa Spika; utekelezaji wa
mradi wa Kurasini ni kuliendeleza eneo hilo kama Kituo cha Biashara na
Ugavi -“Trade and Logistic Centre”. Serikali kupitia Mamlaka ya EPZ
imedhamiria kuliendeleza eneo la kituo cha Biashara cha kurasini kama
Soko la Mazao Mchanganyiko kwa kuanzia na zao la chai, kahawa na mazao
ya bustani. 
Umuhimu wa kutekeleza wazo la
kujenga kituo cha Biashara na Ugavi – Kurasini kwa ajili ya mazao ya
kilimo ni kuwezesha Sekta ya kilimo kuchangia vizuri zaidi katika pato
la Taifa kwa kuwezesha uongezaji wa thamani ya mazao na biashara ya
mauzo ya nje kufanyika. Baada ya kilimo shughuli zinazofuata ni
uchakataji (viwanda) na hatimae mauzo (biashara). 
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia
NDC imekamilisha upimaji wa eneo la TAMCO ambapo jumla ya ekari 201.63
zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na miundombinu. Hadi sasa
viwanda viwili (02) vinavyofanya kazi vimeajiri watumishi 200 na ujenzi
wa viwanda vipya eneo la TAMCO kibaha vinakadiriwa vitaajiri watumishi
21,220 ajira za kudumu. Madhumuni ya Serikali ni kuwa na Industrial Park
nyingi nchini ama kupitia EPZA ama NDC ama Halmashauri zetu ili
wafanyabishara na wawekezaji wenye mtaji na business plan wakute tayari
eneo lina maji, umeme na huduma nyingine muhimu. 
2.6 Mikopo kwa Wajasiriamali
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia
SIDO imefanikiwa kuchochea uanzishwaji wa shughuli za kiuchumi kwa
kutumia mikopo inayotolewa na Skimu ya Ukopeshaji kwa Wajasirimali (SME
Credit Guarantee Scheme-CGS) na Mfuko wa Wafanyabiashara Wananchi
(NEDF). Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Machi 2020, mtaji wa
Mfuko wa NEDF umeongezeka 
kutoka Shilingi Bilioni 6.429
Machi 2016 hadi Bilioni 8.65 Machi, 2020 ikiwa ni ongezeko la Shilingi
Bilioni 2.22. Ongezeko hilo limetokana na riba inayopatikana kutokana na
fedha inayojizungusha (Revolving Fund) kupitia mikopo hiyo. Aidha,
jumla ya wajasiriamali 17,696 wakiwemo wanawake 8,933 na wanaume 8,721
walipatiwa mikopo iliyowezesha kupatikana jumla ya ajira 47,180. Kupitia
mifuko hiyo, jumla ya viwanda vipya 437 vilianzishwa na kutoa ajira
1,481. Jitihada hizo ni kichocheo na chachu kubwa kwa huduma na taasisi
za fedha ambazo nazo hutoa huduma ya mikopo. 
Mheshimiwa Spika; mwezi Februari
2020, yalisainiwa makubaliano kati ya SIDO, VETA, AZANIA BANK, NSSF na
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ya kuanzisha programu ya
kutoa mikopo kwa wajasiriamali waliohudumiwa na SIDO na wahitimu wa VETA
kupitia Benki ya AZANIA. Makubaliano hayo yalifanyika chini ya uratibu
wa NEEC yanatoa nafasi kwa SIDO na VETA kuwapeleka wajasiriamali na
wahitimu Benki ya AZANIA kuomba mikopo ya viwanda ya kuanzia Tshs
milioni 8 hadi milioni 500. Fedha zitakazokopeshwa kiasi cha TSh.
Bilioni tano (5) zimetolewa na NSSF kwa mkopeshaji ambaye ni Benki ya
AZANIA. 
Mwongozo wa utekelezaji wa
programu unaandaliwa ndipo utekelezaji wa programu hiyo uanze. Wizara
inakusudia kuweka msukumo mkubwa wa program hiyo ili iwafikie
wajasiriamali wengi nchini na wapate kunufaika. Tunawashukuru NSSF na
AZANIA Bank na natoa wito kwa mabenki yote nchini na mifuko ya jamii
kuiga mfano huu ili kuinua wajasiriamali nchini. 
2.7 Majengo na Maeneo kwa Shughuli za Wajasiriamali
Mheshimiwa Spika; Serikali
imefanikiwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wajasiriamali kufanya
shughuli mbalimbali za kiuchumi. Jitihada hizo zimewezesha ujenzi wa
majengo viwanda (Industrial Shades) 12 katika mitaa ya viwanda ya SIDO
iliyopo mikoa ya Dodoma (3), Manyara (3), Kagera (1), Mtwara (1) na
Geita (4). Jumla ya viwanda 29 vimeweza kusimikwa katika majengo hayo na
hivyo kuzalisha ajira 648. Kutokana na umuhimu huo, Wizara inaendelea
na ujenzi wa majengo ya viwanda katika mikoa mingine kwa kuanzia mikoa
ya Kigoma, Mtwara na Ruvuma ambapo SIDO imekamilisha upembuzi yakinifu
wa majengo matatu pamoja na michoro ya usanifu (architectural drawings)
katika mikoa ya Mtwara (2) na Kigoma (1) na ujenzi umeanza. 
Mheshimiwa Spika; ukamilishaji wa
majengo viwanda (industrial sheds) unategemewa kuwezesha uanzishwaji wa
viwanda vipya saba vitakavyotengeneza ajira 76. Vilevile, Serikali
imefanikisha kusogeza karibu huduma za kusaidia na kuhamasisha wananchi
kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kujenga ofisi nne (4)
za SIDO katika mikoa mipya 
ya Simiyu, Katavi na Geita. 
2.8 Fursa za Biashara na Masoko ya Kikanda
Mheshimiwa Spika; katika kutumia
fursa za masoko ya kikanda, Wizara imefanikisha kuongezeka kwa mauzo ya
bidhaa na huduma kwenye masoko hayo yanayotoa fursa za upendeleo maalum
(preferential market access). Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo
ya bidhaa kwenda kwenye masoko ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mfano, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka mwaka 2015 hadi
mwaka 2018 Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwa
wastani wa USD Milioni 288.04. 
2.9 Uboreshaji Mazingira ya Biashara Nchini
Mheshimiwa Spika; katika kuboresha
mazingira ya biashara nchini, Wizara imefanikiwa kuandaa na kutekeleza
Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara Nchini – BLUEPRINT.
Mpango huo umewezesha maboresho ya tozo 173 ambapo tozo 163 zimefutwa na
tozo kero 10 zimepunguzwa kiwango. Kati ya tozo zilizofutwa, 114 ni za
Sekta ya Kilimo na Mifugo, 5 za OSHA, 44 za TBS, Mamlaka za Mkemia Mkuu
wa Serikali (GCLA), Utalii, Maji, Uvuvi na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula
na Dawa – TFDA. Aidha, tozo zilizopunguzwa ni za GCLA. Mpango huo
umewezesha kuhamisha jukumu la usimamizi wa masuala ya chakula kutoka
iliyokuwa TFDA kwenda TBS, ili kuondoa muingiliano wa majukumu.
Maboresho hayo yamesaidia kuondoa urasimu na kupunguza gharama za
kufanya biashara. 
2.10 Utoaji Huduma za Kieletroniki kwa Wafanyabiashara na
Wajasiriamali Nchini
Mheshimiwa Spika; kutokana na
kufutwa kwa tozo hizo, usajili wa usalama mahali pa kazi (workplace)
umeongezeka kutoka 16,457 mwaka 2019 ikilinganishwa na mahala pa kazi
11,963 mwaka 2018. Aidha, BLUEPRINT imeandaliwa Mpango Kazi (Blueprint
Action Plan-BAP) ili kuongoza utekelezaji wake. Sambamba na hilo,
Serikali inaendelea na maandalizi ya kutunga Sheria ya Uwezeshaji
Biashara ya mwaka 2020 (Business Facilitation Act, 2020), ili kuipa
nguvu ya kisheria misingi ya maboresho iliyobainishwa katika Blueprint.
Rasimu ya Waraka wa Sheria hiyo imekwishawasilishwa kwenye ngazi za
maamuzi Serikalini. 
Mheshimiwa Spika; Wizara inafanya
kila linalowezekana kuboresha utendaji wa BRELA na mifumo yake ya
Usajili wa Majina ya Biashara, Makampuni, Alama za Biashara na Huduma,
Hataza, Leseni za Viwanda na Leseni za Biashara kwa njia ya
Mtandao. Hadi kufikia Machi, 2020, Wakala 
imesajili Makampuni 7,549, Majina
ya Biashara 12,627, Alama za Biashara na Huduma 1,970, Hataza 55, Leseni
za Viwanda 200 na Leseni za Biashara 9,927. 
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia
BRELA imekusanya taarifa za bidhaa mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali
zaidi ya ishirini (20) za kutoka Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar. Tayari taarifa za bidhaa zaidi ya 18 zinazosafirishwa nje
ya nchi (Export) na zaidi ya bidhaa 8 zinazoingizwa nchini (Import)
zimekwishakusanywa na kuingizwa kwenye Mfumo. 
2.11 Kuwaunganisha Wazalishaji, Wasindikaji na
Wafanyabiashara na Masoko ya Ndani na Nje ya Nchi
Mheshimiwa Spika; Wizara kwa
kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Taasisi za Soko la Bidhaa Tanzania
(TMX), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) na AGRA inaandaa
mkakati wa namna bora ya kufungamanisha Sekta za Kilimo na masoko kwa
mazao ya kimkakati yatakayozalishwa nchini. Mkakati huo unalenga:
Kuunganisha wazalishaji ikiwemo wakulima na wasindikaji wa ndani na nje
ya nchi; Kujenga na kuhamasisha uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya
uwezeshaji badala ya kudhibiti biashara kwa Taasisi na Mamlaka za
Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali na leseni za biashara; na
Kuweka vivutio kwa sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mazao ya
kilimo. 
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia
TanTrade imeratibu tafiti za kutambua fursa za masoko ili kuongeza mauzo
ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje. Kipaumbele ni katika masoko
ya: China (Madini, Vito, Nyama, Tumbaku, Korosho na Muhogo); India
(Mikunde, Korosho, Ngozi na Nafaka); Ulaya (Matunda, Mbogamboga, Asali,
Kahawa na Korosho); na Nchi za EAC (nafaka, bidhaa za ujenzi, bidhaa za
ngozi, bidhaa za viwandani na vyakula vya mifugo); na Nchi za SADC
(Madini, nafaka, bidhaa za viwandani, bidhaa za ujenzi). Aidha, mikutano
na misafara ya kibiashara iliyoratibiwa ilizingatia na kutumia matokeo
ya tafiti hizo na hivyo kufanikisha kutumia fursa hizo za biashara. 
2.12 Kuimarika kwa Biashara za Mipakani
Mheshimiwa Spika; Serikali
imewezesha kuanzishwa kwa Vituo kumi vya Mipakani. Aidha, kati ya hivyo
Vituo sita vinafanya kazi kwa mujibu wa utaratibu wa OSBPs, Vituo viwili
(Hororo/Lungalunga; na Sirari/Isebania) ujenzi wake umeshakamilika
vinasubiri kuzinduliwa rasmi. Vituo viwili vilivyobaki (Kasumulo/Songwe;
na Mugina/Manyovu) viko kwenye hatua za awali za ujenzi. Vilevile,
Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na masoko ya kimkakati kwa ajili ya
kukuza biashara na mauzo nje ya nchi kwa maendeleo 
ya wananchi wake na Taifa kwa
ujumla. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imekuwa ikichukua hatua za
kuanzisha, kuboresha na kuendeleza masoko ya kimkakati ya mipakani ya
Nkwenda na Murongo (Kyerwa), Kabanga (Ngara), Kahama (Kahama), Remagwa
(Tarime) na Bweranyange (Karagwe) ili kurasimisha ufanyaji biashara. Kwa
sasa Wizara inaratibu Mradi wa Ujenzi na Uboreshaji wa Masoko ya
Mipakani ili kuhakikisha wananchi waishio mipakani wananufaika ipasavyo.
Jitihada hizo zimekwenda sambamba na mpango wa Wizara wa ujenzi wa
masoko ya kimkakati mipakani. 
2.13 Kuhuisha Soko la Biashara ya Zao la Tumbaku
Mheshimiwa Spika; kipekee naomba
nimpongeze Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
anayoingoza kwa namna alivyosimama imara na kuweka msimamo thabiti dhidi
ya mifumo ya kumyonya mkulima katika mazao mbalimbali na hususan
korosho, pamba, kahawa na mazao mengine. Wizara itahakikisha kupitia
taasisi zake ikiwemo FCC inasimamia na maeneo mengine kuharibu mifumo ya
aina hiyo iliyowekwa na wafanyabishara wasio waaminifu kwa lengo la
kumnyonya mkulima. Mheshimiwa Rais ni mfano wa kuigwa katika utendaji
wetu hasa katika kuhakikisha haki za wakulima na wananchi wanyonge
zinalindwa. Na hii inadhihirisha utayari wake katika kuhamasisha
wananchi kufanya kazi kwa kujituma na hivyo kuakisi kauli yake ya “HAPA
KAZI TU”. 
Mheshimiwa Spika; Wizara
imefanikiwa kuhuisha soko la zao la Sekta ya Tumbaku baada ya Serikali
kufikia muafaka na wanunuzi wakuu wa zao hilo kuhusiana na madai ya
ukiukwaji wa taratibu za ushindani. Mahauri dhidi ya allince one,
Alliance one international na ATTT yameshamalizika kwa suluhu na
kufungwa ili wadau hao waendelee na shughuli zao katika kuendeleza sekta
ya tumbaku. Aidha, mashuri yaliyokuwa yanaikabili TLTC, TTPL, ULT na
ATTT nayo pia yamemalizwa kwa suluhu. 
Hadi sasa mchakato wa kumaliza kwa
suluhu mashauri yanayowakabili kampuni ya JTI Leaf Services Limited na
JT International uko hatua za mwisho. Kutokana na mwenendo huu wa suluhu
kampuni ya JTI Leaf Services Limited katika mpango wake wa ununuzi
imethibitisha kununua tumbaku yenye thamani ya USD Milioni 12.6 kwa
mwaka 2019/2020, USD Milioni 14.1 kwa mwaka 2020/2021, USD Milioni 15
kwa mwaka 2021/2022 na USD Milioni 15.5 kwa mwaka 2022/2023. 
2.14 Miradi ya NDC
Mheshimiwa Spika; Serikali kupitia
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) inatekeleza miradi mikubwa mitatu
ambayo ni; mradi wa kuunganisha na kuuza matrekta aina ya URSUS (Ubia wa
NDC na kampuni ya URSUS ya 
10 
Poland); mradi wa ujenzi na
uendeshaji wa kiwanda cha viuadudu (Ubia wa NDC na kampuni ya LABIOFAM
ya Cuba); na mradi wa makaa ya mawe (Ubia wa NDC na kampuni ya Intra
Energy Tanzania Ltd na kuendesha kampuni ya TANCOAL Energy Ltd). 
Mheshimiwa Spika; utekelezaji wa
miradi hiyo umekabiliwa na changamoto mbalimbali kiasi cha kuathiri
matokeo chanya yaliyotarajiwa na Serikali. Aidha, jitihada mbalimbali
zimekuwa zikifanywa na Serikali ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo.
Mwezi Machi,2019 Wizara kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za
Serikali tumeanza kufanya mapitio, tathmini na uchunguzi wa miradi hiyo,
ikiwemo kuunda timu za Serikali zijadiliane na timu ya Serikali ya
Poland kwa mradi wa matrekta ya URSUS; Serikali ya Cuba kwa mradi wa
viuadudu uliopo Kibaha; na timu ya kampuni ya Intraenergy Tanzania kwa
ajili ya mradi wa makaa ya mawe ya ngaka (TANCOAL). 
Mheshimiwa Spika; timu hizo
zimeshaundwa na zinatarajia kuanza vikao vyake hivi karibuni. Kutokana
na changamoto za CORONA tunatarajia vikao hivyo vitafanyika kwa njia
ya Video Conference. Wizara inaamini kuwa makubaliano katika majadilino
hayo yataleta matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi hiyo na
inakuwa na manufaa zaidi kiuchumi na kijamii kwa Taifa, hususani katika
ujenzi na uendelezaji wa sekta ya viwanda nchini. 
2.15 Mikataba na Itifaki na Marekebisho ya Sheria
Mheshimiwa Spika; Wizara iliandaa
na kuwasilisha Waraka wa Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba
wa Marrakesh ulionzisha Shirika la Biashara la Dunia ili kufanya Mkataba
wa Uwezeshaji Biashara (Trade Facilitation Agreement) kuwa sehemu rasmi
ya mikataba ya WTO. Tayari waraka huo umekwisharidhiwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Hati ya Kuridhia (Instrument of
Ratification) ya Itifaki hiyo imekwishasainiwa na kuwasilishwa WTO.
Vilevile, Itifaki ya Marrakesh inayolenga kuwezesha upatikanaji wa kazi
zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu, ulemavu unaofanya
mtu kushindwa kusoma wa mwaka 2013 iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Tayari, Hati ya Itifaki hiyo imesainiwa na
kuwasilishwa WIPO. Tunashukuru Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Rais
kwa kuridhia na kufanikisha Mikataba na Itifaki hizo. 
 1. MWELEKEO NA VIPAUMBELE VYA SEKTA YA VIWANDA NA
BIASHARA
3.1 Mwelekeo wa Sekta ya Viwanda na Biashara
Mheshimiwa Spika; mtazamo na
mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha
Mapinduzi kuhusu maendeleo ya viwanda na biashara nchini, unalenga
kujenga uchumi wa viwanda utakaowawezesha 
11 
Watanzania kufikia na kunufaika na
uchumi wa kati ifikapo 2025. Hatua hiyo itawezesha Watanzania kutumia
fursa za kiuchumi na kijamii katika mifumo iliyoboreshwa na
inayozingatia haki na utawala bora. Ni dhamira ya nchi yetu kumfanya
kila Mtanzania kuwa na maisha bora na kunufaika na rasilimali na fursa
zilizopo na zinazojitokeza. 
 1. Kuhamasisha Uendelezaji na Matumizi ya Bidhaa za Ndani
Mheshimiwa Spika; kuthamini
rasilimali na bidhaa za ndani ni ukombozi muhimu wa kiuchumi kwa Taifa
lolote. Mifano hai ni nchi ya Japan na China ambazo wananchi wake
wamejijengea utamaduni wa kuthamini bidhaa zinazozalishwa katika uchumi
wao. Hivyo, Wizara itaendelea kuhamasisha uimarishaji wa ubora na
matumizi ya bidhaa za ndani, nguvukazi na malighafi za ndani ili kuleta
ufungamanisho wa sekta katika kujenga uchumi na kuleta maendeleo kwa
wananchi wake. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TanTrade inaendelea
kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani
kupitia kauli mbiu ya Nunua Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania (Buy
Tanzania, Build Tanzania). Mbinu hiyo ni muhimu sana katika kipindi hiki
cha ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuimarisha viwanda vya ndani na
kutumia Kiswahili katika bidhaa. 
 1. Kuimarisha SIDO
Mheshimiwa Spika; kwa kutambua
umuhimu na mchango wa Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo katika
uchumi na hususan ujenzi wa viwanda, Serikali itachukua hatua za
makusudi kuimarisha ujasiriamali nchini. Kipaumbele kitakuwa katika
kuimarisha taasisi ya SIDO kwa kupitia upya muundo wake na kuijengea
uwezo ili iweze kubeba ipasavyo dhamana ya uendelezaji wa viwanda vidogo
na biashara ndogo inayowabeba Watanzania walio wengi. Jitihada hizo
zitaenda sambamba na kuendelea ujenzi wa shades katika mikoa yote nchini
ili manufaa yalioyoonekana ya ajira na uongezaji thamani wa mazao, na
kuongeza ushindani katika soko yasambae nchi nzima. 
Mweshimiwa Spika; Wizara pia
itaweka mkazo na umuhimu katika upatikanaji wa teknolojia, kuongeza
miundombinu ya uzalishaji (Industrial shades) ili kuwawezesha
wajasiriamali kupata mahali pa kufanyia uzalishaji, na kuweza kuhudumiwa
kirahisi na taasisi mbalimbali zikiwemo za udhibiti wa ubora wa bidhaa,
taasisi za fedha na mafunzo muafaka. Juhudi za kuimarisha jasiriamali
nchini zitaenda sambamba na kuimarisha SIDO ili imudu kutoa huduma bora
na zenye kuleta tija katika uzalishaji wa bidhaa, huduma na ufanyaji
biashara. 
12 
iii. Kuvilinda Viwanda na Biashara za Nchini
Mheshimiwa Spika; uchumi himilivu
unaotabirika na shindani unatokana na jitihada za kuujenga, kuuendeleza
na kuulinda. Kujilinda isitafsiriwe kuwa ndiyo kujitenga kiuchumi na
nchi nyingine, na wala siyo dhambi, kwani hata nchi zilizoendelea
kiuchumi duniani mbinu mbalimbali zinaendelea kutumika kwa njia tofauti.
Hivyo, sera, sheria na mikakati ya kisekta itaendelea kuhakikisha kuwa
kunakuwepo ushindani wa haki ili kulinda viwanda na biashara nchini.
Aidha, tutaendelea kulinda haki za msingi za walaji kwa kuweka utaratibu
wa kisheria utakaotaka wawekezaji, wenye viwanda na wafanyabiashara
katika mazao, bidhaa na huduma kutotumia nguvu ya soko isivyotakiwa na
kusababisha kuwakandamiza wanyonge. 
Mheshimiwa Spika; ili kuongeza
nguvu za utafutaji wa fursa za masoko ya nje, Wizara inafanya uchambuzi
wa kina wa kuona umuhimu wa kuhuisha na kurejesha Waambata wa Biashara
(Trade Attachee) katika ofisi za Balozi zetu zilizo nje ya nchi, ili
kuweka mfumo wa kufanya tathmini na utafiti wa mahitaji ya soko la
bidhaa zinazozalishwa nchini. Tathmini na tafiti hizo zitatoa picha ya
mahitaji ya soko la nje na kuwezesha wazalishaji wa bidhaa za ndani
kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko la nje. 
Mheshimiwa Spika; utoaji huduma
bora kwa wananchi kwa kiwango kinachoridhisha ni lengo kuu la mabadiliko
ya kiutendaji ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayapa kipaumbele.
Hivyo, mwelekeo wetu ni kuhakikisha kuwa taasisi za kisekta
zinajielekeza katika kutoa huduma kwa kiwango kinachokidhi matarajio ya
wananchi. Wizara yangu na taasisi zake zitaongeza ubunifu katika
utendaji kazi kwa tija na kutoa huduma kwa weledi ili kuchochea ufanisi
katika Sekta ya Viwanda na Biashara na hatimaye kuongeza Pato la Taifa. 
 1. Uimarishaji wa Taasisi za Udhibiti na Maendeleo ya Teknolojia na
Uwekezaji Nchini
Mheshimiwa Spika; katika
kuendeleza uchumi wa viwanda, Serikali inaimarisha taasisi zake ili
ziweze kukidhi na kuhimili mahitaji ya maendeleo na ujenzi wa viwanda
nchini. Wizara inajizatiti kuimarisha Taasisi za Utafiti na Maendeleo ya
Teknolojia yaani TIRDO, TEMDO na CAMARTEC kwa kufanya tathmnini ya
kitaalam, kupitia upya na kwa kina majukumu na miundo ya kisheria ya
taasisi hizo. Lengo ni kuzifanyia maboresho mahsusi yatakayozingatia
ushauri wa kitaalam na itakapoonekana inafaa, zitafanyiwa maamuzi ya
kimuundo ikiwemo kuziunganisha ili ziweze kuwa na tija na ufanisi katika
kuleta mwendelezo wa mafanikio ya taasisi hizo na pia kuongeza nguvu
katika kuendeleza viwanda nchini. 
13 
Mheshimiwa Spika; Serikali pia kwa
kuzingatia tathmini ya kitaalam, itajielekeza katika kuimarisha taasisi
za uwekezaji nchini hususan EPZA na NDC ili ziwe mihimili na nguzo za
uwekezaji katika viwanda ambavyo ni muhimu katika kujenga uchumi wa
Taifa lakini wakati mwingine sekta binafsi haiko tayari kuwekeza.
Msukumo ukiwa ni kuunda taasisi / mamlaka mpya itakayobeba jukumu la
kujenga viwanda mama, viwanda vya kimkakati. 
 1. Kutunga Sheria (Business Facilitation Act) kutekeleza Mpango
Kazi – BLUEPRINT
Mheshimiwa Spika; ujenzi wa
mazingira bora na endelevu ya biashara ni kichocheo kikubwa na muhimu
katika kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Hivyo, Serikali kupitia Wizara
yangu imejipanga kuhakikisha kuwa inaendelea kuboresha mazingira ya
biashara nchini. Maboresho hayo yatavutia wawekezaji wa ndani na nje
katika viwanda na biashara na hivyo kuwezesha kutumia fursa mbalimbali
za ndani na nje ya nchi kadri zinavyojitokeza. Misingi ya maboresho ya
mazingira ya kibiashara yanategemewa kuwekewa nguvu ya kisheria na
utaratibu wenye ushirikishaji mpana zaidi wa wadau. 
 1. Muunganisho wa Kiutendaji Kati ya Wizara na Mamlaka za
Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
umuhimu wa utendaji kazi wenye tija katika ngazi za Makatibu Tawala Mkoa
(RAS) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs), Kada za Maafisa Biashara
zitapewa msukumo wa kipekee, ili kuhakikisha inahuishwa na kufanya kazi
zake kitaaluma. Aidha, Wizara imeanza mazungumzo na Ofisi ya Rais
TAMISEMI ili kuandaa Mkataba wa Makubaliano (Memorandum of Undestanding)
wa kuweka mifumo na mazingira bora ya kufanya kazi pamoja na kwa
kushirikiana. 
vii. Utungaji wa Sheria ya Kujilinda Dhidi ya Athari za Biashara
(Trade Remedies Act, 2020)
Mheshimiwa Spika; Wizara
inaendelea na taratibu za kutunga Sheria ya Kujilinda Dhidi ya Athari za
Kibiashara ya mwaka 2020 (Trade Remedies Act, 2020) ambayo inalenga
kulinda biashara na viwanda vya ndani. Ulinzi huo unalenga kuzuia
uingizwaji wa bidhaa kwa wingi (import surge); bidhaa kuuzwa kwa bei ya
chini ikilinganishwa na bei ya bidhaa kama hizo kwenye nchi zinakotoka
(dumping); na bidhaa nyingine kupewa ruzuku (subsidies) na nchi zao au
taasisi nyingine na hivyo kuathiri bidhaa ambazo zinazalishwa ndani ya
nchi bila kupata ruzuku. Mapendekezo ya kutunga Sheria hiyo
yamekwishawasilishwa Serikalini kwa ajili ya maamuzi. 
14 
viii. Utekelezaji wa Mikakati Mbalimbali ya Uendelezaji Viwanda
Nchini
Mheshimiwa Spika; Mkakati wa
Kuendeleza Sekta ya Ngozi wa mwaka 2016-2020 umejikita katika kuendeleza
mnyororo wa thamani wa Zao la Ngozi. Katika kutekeleza mkakati huo,
Serikali imetoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi na vifaa
vinavyotumika kutengenezea viatu na bidhaa za ngozi vinavyoingizwa
kutoka nje ya nchi. Lengo likiwa ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa
viwanda vya ngozi na kuvutia uwekezaji. Fursa hiyo imetumiwa na Kiwanda
cha Karanga Leather Industries ambacho hivi karibuni kimeingiza mashine
na vifuasi (accessories). Vilevile, Kiwanda cha ACE leather Morogoro
kimetumia fursa hiyo kuingiza mashine na vifuasi ili kusindika ngozi
hadi hatua ya mwisho. Mkakati huo pia umehamasisha taasisi za umma na
shule kununua bidhaa za ngozi hususan viatu kutoka viwanda vya ndani
kulingana na upatikanaji. Kwa sasa maandalizi ya kuhuisha Mkakati huo
yanaendelea. 
 1. Kuimarisha Sekta Binafsi
Mheshimiwa Spika; mtazamo wa Sera
za Taifa zinatambua nafasi ya sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya
kiuchumi. Kujenga sekta binafsi hasa wajasiriamali wadogo kwa kuwawekea
mazingira wezeshi na rafiki kupitia upatikanaji wa mitaji, teknolojia
rahisi na rafiki, masoko ya uhakika na huduma muhimu zinazolenga
kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji ni suala lisilohitaji
mjadala. Hivyo, katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara, mtazamo
wa kisera utalenga kukuza na kutengeneza uwekezaji kuanzia ngazi ya
ujasiriamali mdogo hadi kuwa matajiri wazalendo wa baadaye. Msukumo
utawekwa katika kuweka sera zinazotabirika, kujenga mazingira
yanayotabirika na kutoa fursa ya masoko. 
 1. Nguvukazi Kukidhi Mahitaji ya Viwanda
Mheshimiwa Spika; suala la kuwa na
rasilimali watu ya kutosha yenye sifa, uwezo na inayotumika vizuri ni
muhimu katika kujenga uchumi endelevu wa viwanda. Wizara imejipanga
kuendeleza kimkakati rasilimaliwatu iliyonayo kwa kuwa na mpango mpana
wa kuwaendeleza na kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara ili kuongeza
ujuzi na weledi katika kutekeleza majukumu yao. Hii itawezesha kuboresha
huduma zitolewazo na kukidhi matarajio ya wadau na umma wa ujumla.
Tutajielekeza zaidi katika maeneo ya kuboresha huduma (service delivery)
kwa njia mbalimbali, kuimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za
kisekta (Regulatory role) na kuishirikisha sekta binafsi na wadau
wengine kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi. Ili kuwa na
rasilimaliwatu yenye afya, Wizara itahakikisha kuwa watumishi wanapata
elimu ya afya na huduma za kinga dhidi ya 
15 
magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza. 
 1. Kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji
Mheshimiwa Spika; kuwekeza katika
ujenzi wa miundombinu ya msingi na wezeshi kwa ajili ya ujenzi wa
viwanda na ufanyaji biashara ni suala la msingi. Uendelezaji wa
miundombinu hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi utapewa msukumo zaidi
ili kuleta tija na mvuto kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Wizara
itashirikiana na Balozi za Tanzania pamoja na Ofisi ya Waziri
Mkuu-Uwekezaji kuja na mkakati wa kuvutia wawekezji kutumia sehemu
ambazo zimefidiwa chini ya EPZA. Pia, imezindua miradi ya ujenzi wa
miundombinu hiyo katika mikoa yote nchini ambapo kwa Mkoa wa Dodoma
tumeanza na ujenzi wa Kongano la Viwanda Kizota (Kizota Industrial
Cluster). 
xii. Uendelezaji wa Miradi ya Kimkakati na ya Kielelezo
Mheshimiwa Spika; katika
kuendeleza Miradi ya Kimakati, Wizara, TIRDO, Wakala wa Jiolojia
Tanzania (GST), na African Minerals and Geosciences Centre (AMGC)
ilifanya uhakiki wa awali wa wingi na aina za madini yaliyopo kwenye
miamba ya Liganga. Matokeo ya awali yalibainisha kuwa kuna tofauti ya
wingi na aina za madini ikilinganishwa na ilivyobainishwa katika taarifa
ya mwekezaji. Utafiti wa kina unaendelea kufanyika kwa nia ya
kubainisha hali halisi ya rasilimali zilizopo. Aidha, NDC kwa
kushirikisha na uongozi wa Wilaya ya Ludewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi imekamilisha kazi ya uthaminishaji mali ndani ya
eneo la mradi ili kufidia wananchi watakaopisha Mradi unganishi wa
Mchuchuma na Liganga. 
Mheshimiwa Spika; TIRDO inaendelea
kufanya “Techno Economic Study” katika Mradi wa Magadi Soda Engaruka.
Lengo la utafiti huo ni kubainisha kiasi cha mahitaji ya magadi nchini,
thamani ya uwekezaji utakaofanyika na faida za mradi huo kwa ujumla.
Makadirio ya awali ya rasilimali magadi (brine) yameonesha uwepo wa
kiasi cha mita za ujazo Bilioni 4.68. Aidha, ilibanika kuwa rasilimali
hiyo inajiongeza kwa kiasi cha mita za ujazo wa Milioni 1.9 kwa mwaka.
Uhakiki wa rasilimali hiyo unaendelea sambamba na ukamilishaji wa
upembuzi yakinifu wa mradi na athari ya mradi katika mazingira na jamii.
Utafiti huo unategemewa kukamilika mwisho mwa mwezi Aprili, 2020. 
3.2 Vipaumbele kwa Bajeti ya Mwaka 2020/2021
Mheshimiwa Spika; vipaumbele vya
bajeti na malengo ya sekta ya viwanda na biashara ya mwaka 2020/2021
vimeelezewa kwa kina ukurasa 138 hadi 181 ya hotuba ya bajeti. 
16 
 1. MAKADIRIO YA MAKUSANYO NA MAOMBI YA FEDHA KWA
MWAKA 2020/2021
4.1 Makusanyo ya Serikali
Mheshimiwa Spika; Katika mwaka
2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya Shilingi
15,000,000 kutokana na uuzaji wa nyaraka za zabuni na makusanyo mengine.
Kati ya fedha hizo, Shilingi 9,000,000 zitakusanywa katika Fungu 44 na
Shilingi 6,000,000 zitakusanywa katika Fungu 60. 
4.2 Maombi ya Fedha
Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka
2020/2021, Wizara ya Viwanda na Biashara inaomba kutengewa jumla ya
Shilingi 81,366,902,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 51,679,016,000 ni
za Matumizi ya Kawaida na Shilingi 29,687,886,000 ni za Matumizi ya
Maendeleo. Aidha, katika Bajeti hiyo, Shilingi 57,414,395,000 ni za
Fungu 44 na Shilingi 23,952,507,000 ni za Fungu 60. 
 1. SHUKRANI
Mheshimiwa Spika; ujenzi wa uchumi
wa viwanda ni shirikishi na jumuishi, hivyo huhitaji ushiriki wa wadau
mbalimbali. Kwa kutambua umuhimu huo, napenda kutumia fursa hii
kuwashukuru kwa dhati washirika wetu wa maendeleo, zikiwemo nchi rafiki.
Vilevile, nashukuru taasisi zote, sekta binafsi, taasisi zisizo za
kiserikali (CBOs & FBOs) kwa kuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa uchumi
wetu. Kama nchi, tunaendelea kutegemea ushirikiano wenye tija katika
kufikia malengo endelevu ya jamii nzima ya Watanzania. 
Mheshimiwa Spika; Naomba
nihitimishe kwa kuwashukuru tena Watanzania kwa kuendelea kuunga mkono
jitihada za Serikali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na hivyo kuwa
kichocheo cha kukua kwa sekta nyingine za uchumi. Ni dhahiri kuwa Taifa
kwa kipindi hiki kinahitaji kuendeleza ari hiyo katika kupambana na
majanga mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa mafua makali wa KORONA. Kwa pamoja
tuungane kujikinga na kulindana ili Taifa libaki salama na likiwa na
nguvukazi ya kutegemewa. 
 1. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika; Wizara
ninayoisimamia imeazimia kuendeleza maamuzi makini na yenye mashiko ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda wenye mafanikio
ambayo yanajitafsiri katika ubora wa maisha ya kila mwananchi na Taifa
kwa ujumla. Hivyo, Sera, Sheria na Mikakati iliyopo itaendelea
kuboreshwa ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuchochea 
17 
mbinu za utekelezaji ili kufikiwa
kwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha
Mapinduzi. Ni dhahiri kuwa jitihada hizo pamoja na utekelezaji
wa Blueprint utatutoa hapa tulipo na kutupaisha katika maendeleo na
kufikia lengo la uchumi wa kati ifikapo 2025 kama ilivyoazimiwa na Dira
ya Taifa ya 2025. Inawezekana, endapo kila mmoja wetu atachukua nafasi
yake na kujituma ipasavyo. 
 1. MAOMBI RASMI YA FEDHA
Mheshimiwa Spika; Naomba Bunge
lako Tukufu liidhinishe makadirio ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya
kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 15,000,000 na matumizi ya jumla ya
Shilingi 81,366,902,000 kwa mwaka 2020/2021. 
 1. MWISHO
Mheshimiwa Spika; Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara yenye anuani ifuatayo: www.mit.go.tz. 
Mheshimiwa Spika; Naomba kutoa hoja.