Egidia Vedasto
APC Media, Arusha
Jamii imekumbushwa kuchukua tahadhari kutokana na kuongezeka kwa maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi ambapo kwa mwaka huu yamefikia asilimia 2.9, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1, ukilinganisha na takwimu za kitafiti za mwaka 2016/2017.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, ambayo katika Jiji la Arusha yamefanyika Viwanja vya Soko la Kilombero, Katibu Tawala Wilaya Arusha Khaman Simba Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Felician Mtahengerwa amesema, ni muhimu jamii kuendelea kuchukua tahadhari juu ya maambukizi mapya ili kuweza kufikia malengo ya ulimwengu ya kuutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
“Nitoe wito kwa wazazi, walezi na walimu shuleni, endeleeni kuzungumza na watoto, hizi zama si za kumuonea aibu mtoto, wafanyeni marafiki ili mpate kuwaelimisha juu ya UKIMWI namna unavyopatikana na jinsi ya kujikinga” amesema Simba.
Aidha amesema kuwa serikali imekuwa ikichangia gharama za matibabu kwa kaya za watu wanaoishi na virusi yva Ukimwi (WAVIU) na makundi maalum (Waraibu) walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU, ambapo kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 Halmashauri imepanga kulipia gharama za matibabu kwa kaya 35 (watu 210) yenye thamani ya shilingi milioni moja na elfu hamsini (1, 050,000) kwa watu wanaoishi na VVU.
“Leo tunapoadhimisha siku ya UKIMWI katika wilaya yetu, tukumbuke kuwa jamii yetu pia inakabiliwa na ongezeko kubwa la magonjwa mengine sugu yasiyoambukizwa (MSY) ambayo yanachangiwa na mtindo wa maisha na ulaji usiofaa, nawasihi ndugu zangu tuendelee kujali afya zetu kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, kwa kuwa magonjwa haya mengi yanaweza kuzuilika” amesema Simba.
Hatahivyo ameongeza kwamba, Serikali imepokea ombi la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi la kuunganishwa na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.
Mmoja wa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi na Mshauri katika Kituo cha Afya Levolosi Gustaf Ramale, ameikumbusha jamii kuwa na desturi ya kupima afya mara kwa mara na kutumia dawa za kufubaza inapotokea Mtu amegundulika kuwa na Virusi Vya Ukimwi.
“Kupata Ukimwi sio kufa, bali inakupasa kuzingatia ushauri wa Madaktari, kuzingatia kula chakula bora, kutumia dawa kama inavyoelekezwa na kuchukua tahadhari ili usimuambukize mwingine” ameeleza Mzee Gustaf.
Mkazi wa Kata Ngarenaro Jamila Swaib ameelezea kuhusu Siku ya Ukimwi Duniani, kwamba kila mmoja anatakiwa kutomuamini mwenzake na kuchukua tahadhari za kupima mara kwa mara ili ikitokea umeupata uanze dawa mara moja.
“Huu ugonjwa ni mbaya, tunaishi na waathirika tunaona wanavyopata taabu, nasahauri mtu akijua ameambukizwa asichelewe kutumia dawa, ili imsaidie kupandisha kiwango cha CD4 na kuendelea na maisha kama kawaida”amefafanua Jamila.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kote Ulimwenguni yamebeba kaulimbiu “Chagua Njia Sahihi Tokomeza Ukimwi”