Jeshi la polisi lazuia mkutano wa mchungaji peter msigwa



Jeshi
la Polisi mkoani Iringa, limezuia mkutano wa Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, kwa madai ya kutokuwapo kwa askari wa
kutosha wa kulinda mkutano huo.


Taarifa
za kuzuiwa kwa mkutano huo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii,
ikionyesha barua ya zuio kutoka polisi. Mkutano huo ulikuwa ufanyike
katika viwanja vya Mwembetogwa.

Kamanda
wa Polisi Mkoani Iringa, Juma Bwire, alisema marufuku hiyo ilitokana na
kutokuwapo kwa askari wa kutosha kwa kuwa wako kwenye usimamizi wa
mitihani ya kidato cha nne, kidato cha pili na darasa la nne pamoja na
kuwapo kwa taarifa za kiintelijensia juu ya kutokea vurugu na
kusababisha uvunjifu wa amani.

Kamanda
huyo amesema sababu nyingine ni dalili za kuanza kampeni mapema za
kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya kalenda ya kampeni
kuanza.


Kamanda huyo amebainisha kuwa sababu nyingine ni barua ya mkutano huo
kutoweka wazi dhumuni la mkutano ikiwa ni kinyume cha kifungu cha
43(1)(b) cha Sheria ya Polisi na Polisi wasaidizi sura 322 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akizungumzia
kuhusu kuzuiwa mikutano yake, Msigwa alisema hiyo ni kinyume cha sheria
kwa kuwa Mbunge hutakiwa kutoa taarifa ili kuhakikisha usalama wa
mikutano yake na si kuomba ruhusa kwa jeshi hilo.

“Mimi
ni mbunge na ile ndiyo kazi yangu. Sasa kazi yao ni kulinda mikutano
yangu ili pasitokee vurugu na si kuzuia.” alisema Msigwa.