Jumla ya vyeti na leseni 246 vimetolewa na tbs kwa wazalishaji wa bidhaa nchini

 

Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dkt.Athuman Yusuf Ngenya akimpatia
leseni ya kutumia alama ya ubora ya uunganishaji wa mabasi Bw.Jonas
Nyagawa kutoka kampuni ya BM Motors iliyopo mkoani Pwani. TBS inatoa
leseni hiyo kwa mara ya kwanza Tanzania kwa Kampuni ya kitanzania
inayojishughulisha na uunganishaji wa mabasi nchini.

Meneja
wa Uthibitishaji ubora Bw.Gervas Kaisi akizungumza na wazalishaji
waliohudhuria hafla ya utoaji leseni mapema leo, TBS Ubungo jijini Dar
es salaam.

Kaisi alitoa wito kwa wazalishaji hao kuhakikisha wanaendelea
kuzalisha bidhaa bora wakati wote ili kuendelea kumlinda mlaji na kuunga
mkono jitihada za serikali za kuendeleza Viwanda.

Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dkt.Athuman Yusuf Ngenya akimpatia
leseni ya kutumia alama ya ubora mjasiriamali kutoka kampuni ya Ulanzi
Halisi ya mkoani Iringa inayotengeneza pombe ya ulanzi .

Mjasiriamali huyo ameishukuru TBS kwa kupata alama ya ubora na anategemea kupata soko zaidi ikiwemo nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Viwango Tanzania Dkt.Athuman Yusuf Ngenya akizungumza na wazalishaji
waliohudhuria hafla ya utoaji leseni mapema leo, Makao Makuu ya TBS
Ubungo jijini Dar es salaam.

NA EMMANUEL MBATILO

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
limetoa jumla ya leseni na vyeti 246 kwa kutumia alama ya ubora wa TBS
kwa wazalishaji wa bidhaa nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa TBS, Dkt.Athuman Ngenya amesema kati ya leseni na
vyeti 127 sawa na asilimia 51.63 vimetolewa kwa wajasiriamali.

“Vyeti na leseni vilivyotolewa
vinahusisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile za
vyakula,vipodozi,viatu,vifaa vya ujenzi, vifaa vya umeme, magodolo na
vifungashio kwa pamoja”. Amesema Dkt.Ngenya.

Aidha Dkt.Ngenya amesema kuwa
leseni na vyeti hivyo vitasaidia bidhaa zilizothibitishwa kukubarika
sokoni pamoja na kupata faida kiushindani.

Pamoja na hayo Dkt.Ngenya amesema
kuwa katika kipindi cha mwezi Januari mpaka mwezi Mei mwaka huu, TBS
imesajili majengo 3295 ya biashara na kuhifadhi bidhaa za vyakula na
vipodozi kwa pamoja pia katika kipindi hicho wamesajili bidhaa 642 za
vyakula na vipodozi kwa pamoja.

Kwa upande wake Meneja wa
Uthibitishaji ubora TBS, Bw.Gervas Kaisi ametoa wito kwa wazalishaji hao
kuhakikisha wanaendelea kuzalisha bidhaa bora wakati wote ili kuendelea
kumlinda mlaji na kuunga mkono jitihada za serikali za kuendeleza
Viwanda.