Na Ahmed Mahmoud Arusha
Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya Ukimwi imeusifia mkoa wa Arusha kwa kushuka kwa kiwango Cha maambukizi ya ukimwi kutoka mwaka 2003 /4 ulikuwa ni asilimia 5.1 hadi asilimia 1.9 mwaka 2016/17.
Akiongea na wanahabari Mara baada ya ziara yao ya siku mbili mkoani hapa kutembelea Magereza na Hospital ya mkoa ya Mount Meru Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya masuala ya Ukimwi Kifua kikuu na madawa ya kulevya Oscar Mukasa alisema kuwa wamefurahishwa Sana na mkoa huo kwenye suala hilo la kushuka kwa viwango vya maambukizi ya Ukimwi.
Alisema kuwa mafanikio ya Kwanza kwenye hospital ya Mont Meru ni suala zima la Usafi kwenye hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na shughuli za huduma za utoaji dawa CTC wamejipanga vizuri na taarifa yao inaonyesha mafanikio makubwa japo Kuna changamoto kidogo.
Alisema kuwa changamoto kubwa ni taarifa ya wagonjwa kutoendelea na dawa nao wameshauri watumie huduma ya kuwafuata majumbani kwani wamebaini kuwa wengi wasioendelea na dawa ni wagonjwa wa nje ambao wanakaa mbali na hospital hiyo hivyo kuwataka kusogeza huduma hizo kwenye vituo vya karibu na wagonjwa hao.
“Utaona mkoa huu umeweza kupunguza maambukizi ya Ugonjwa huu na inafanya vizuri mfano ni hospitali ya mkoa ya Mount Meru ipo Safi hili ni kiashiria kizuri Cha utoaji wa huduma bora Ila changamoto inatakiwa wasogeze huduma kwa wagonjwa kwenye vituo vya Afya vyote ili kuweza kuwahudumia kwa ukaribu zaidi” alisisitiza Mukasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga wizara ya Afya Dkt.Leonard Subi alisema kuwa uwasilishaji wa taarifa kwa watendaji wamelichukuwa huku Serikali ikiwa na malengo ya kufikia tisini Tatu kwenye zile tisini Tatu.
Alisema kuwa vituo vya kutibu Ugonjwa wa kifua kikuu ni 144 ambapo hapo awali mwaka 2005 hospital ya kibongoto ilikuwa pekee ikitibu Ugonjwa huo hapa nchini na hii ni mafanikio makubwa Sana ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt.John Magufuli kuweza kujenga hospitali na vituo vya Afya kila Kona ya nchi.
“Utaona mafanikio makubwa tumeweza kuzifikia tisini Tatu kwa asilimia kubwa mfano tisini ya Kwanza ni sawa na asilimia karibu 87 ambayo ni ya watu wanaojua hali zao na wanatumia dawa huku tisini ya pili ikiwa ni asilimia 85 na tisini ya Tatu ni asilimia 87 hadi 88 utaona jinsi mafanikio yalivyo” alisema Dkt.Subi
Awali mjumbe wa kamati hiyo na mbunge wa Mbulu Vijijini Fratey Massay alisema kuwa mafanikio hayo yanaonyesha ushirikiano uliopo Kati ya viongozi na watendaji hivyo suala hilo la kupunguza kwa maambukizi mapya linahitaji ushirikiano huo utakaosaidia kuendelea kupunguza maambukizi na kutoa huduma za Afua za Ukimwi.