KAMATI YA BUNGE YA PAC YAIMWAGIA SIFA TANAPA,

#Ni kwa kuboresha miundo mbinu, ongezeko mapato hifadhi ya Saadan

Na Mwandishi Wetu, APC

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Wadhamini TANAPA, na Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kufanikisha ongezeko kubwa la mapato ya Hifadhi ya Taifa Saadani. 

Ongezeko hili limetokana na mapato ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kwa njia ya ndege, ambapo mapato yameongezeka kufikia shilingi bilioni 1.68 kuanzia Julai hadi Machi mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na makadirio ya ukusanyaji ya shilingi bilioni 1.41 katika kipindi cha miezi 8.

Kamati hiyo imehimiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuendelea kusimamia miradi ya miundombinu ya utalii inayotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani ili kurahisisha watalii kufika kwa urahisi, kuchochea shughuli za kiutalii, na kuongeza mapato ya Serikali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Mb.Josephat Hasunga

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Japheti Hasunga (Mb), alitoa maelekezo hayo Machi 26, 2025, wakati wa ukaguzi wa miradi miwili inayotekelezwa ndani ya hifadhi hiyo, ikiwemo uboreshaji wa barabara za ndani ya hifadhi na upanuzi wa uwanja wa ndege.

“Tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Saadani. Sasa endeleeni kusimamia miradi hii ili kuhakikisha inakamilika kwa viwango vya juu na kuleta manufaa kwa sekta ya utalii. 

Pia, tunashauri uwekezaji zaidi katika miundombinu mingine kama hoteli na huduma za usafiri ndani ya hifadhi ili kuvutia wageni wengi zaidi,” alisema Hasunga.

Mwenyekiti wa bodi Mkuu wa majeshi mstaafu George Waitara

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara, alitoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za kutekeleza miradi hiyo na kuongeza kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.

“Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo katika Hifadhi za Taifa inatekelezwa kwa ufanisi. Hatua hii ni muhimu kwa mustakabali wa utalii nchini, na tunapaswa kuendelea kuwekeza zaidi ili kuvutia watalii wengi na kukuza uchumi wa Taifa,” alisema Jenerali Waitara.

Kamishna Mkuu wa Uhifadhi shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Musa Kuji

Naye, Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Juma Kuji alieleza kuwa maboresho ya miundombinu ya utalii Saadani yameongeza mvuto wa hifadhi kwa watalii, hali inayosaidia kuongeza idadi ya watalii na mapato. 

Kamishna Mkuu wa uhifadhi wa shirika la higadhi za taifa (TANAPA), Musa Juma kuji akitoa maelezo ya maendeleo ya shirika hilo kwa kamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC).

Pia, alibainisha kuwa miundombinu bora huongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa watalii, hivyo kuimarisha shughuli za utalii.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Afisa Uhifadhi Mkuu Gladys Ng’umbi, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani, alieleza kuwa maboresho ya miundombinu hiyo yamezingatia viwango vya kimataifa ili kuhakikisha uwanja wa ndege wa Saadani unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege nyingi na kubwa zaidi.

“Maboresho ya uwanja huu yamezingatia viwango vya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ili kuhakikisha kuwa uwanja wa ndege wa Saadani unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba watalii 35 hadi 40 kwa ndege moja, ambapo uboreshaji huo utasaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja kutembelea hifadhi pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii,” alisema Ng’umbi.

Hifadhi ya Taifa ya Saadani imekuwa ikifanya maboresho ya miundombinu ya hifadhi ili kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii, ikizingatiwa kuwa hifadhi hiyo ni muhimu kiikolojia kwani inakutanisha nyika na bahari katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki. 

Maboresho hayo yana umuhimu mkubwa katika kuongeza vivutio vya utalii na kuboresha huduma kwa wageni, hali inayochochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini na kuongeza mchango wake kwa uchumi wa Taifa.