Kamati ya bunge yaipongeza pura kwa kuokoa tshs bilioni 10 za psas


Teresia Mhagama – WN

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini imepongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa
Petroli (PURA) kwa kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 10.08 kutokana na
kaguzi za gharama na mapato ya mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia nchini
(PSAs).

Pongezi hizo wamezitoa tarehe 25
Oktoba, 2019 wakati wa kikao baina ya Kamati hiyo na Wizara ya Nishati
pamoja na PURA ambapo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliiongoza
Wizara ya Nishati katika uwasilishaji wa taarifa hiyo akiwa ameambatana
na Katibu Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na Menejimenti ya Wizara, PURA na
Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA,
Charles Sangweni alisema kuwa kama kaguzi hizo zisingefanyika,
wawekezaji wangeweza kujirudishia fedha hizo (cost recovery) kulingana
na mkataba hivyo kiasi hicho kilichookolewa kitafanya mapato ya Serikali
kuongezeka wakati wa ugawanaji wa faida itokanayo na mauzo ya Gesi
Asilia.

“ PURA ilianza kutekeleza jukumu
hili kwa kufanya kaguzi za gharama na mapato kuanzia mwaka 2016 ambapo
kiasi cha shilingi bilioni 10.08 zimeokolewa hadi sasa.” Alisema
Sangweni
Sangweni alieleza kuwa Mamlaka
hiyo pia imeendelea kufanya kaguzi katika maeneo ya uzalishaji wa Gesi
Asilia kwa lengo la kuhakiki usalama wa mazingira na wafanyakazi pamoja
na kupata uhalisia wa shughuli zinazotekelezwa katika uzalishaji wa Gesi
Asilia nchini.

Alisema kuwa, katika kipindi cha
robo mwaka wa 2019/2020, masuala mbalimbali yaliangaliwa na kuhakikiwa
na kaguzi hizo zilibaini kuongezeka kwa uzalishaji wa Gesi Asilia ambapo
katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2018/19 uzalishaji ulikuwa
ni futi za ujazo bilioni 15.73 na kwa kipindi cha robo ya kwanza ya
mwaka 2019/20 uzalishaji ulikuwa ni futi za ujazo bilioni 16.05.

Alisema kuwa, kwa ujumla Gesi
iliyogunduliwa nchini hadi sasa ni takriban futi za ujazo Trilioni 57.54
ambapo kati ya kiasi hicho, Gesi iliyogunduliwa nchi kavu (onshore) ni
futi za ujazo Trilioni 10.41 na kwa upande wa Bahari Kuu (offshore) ni
futi za ujazo Trilioni 47.13.

Aidha alisema kuwa, kaguzi za PURA
zilibaini kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi wazawa katika kampuni
zinazozalisha Gesi Asilia huku akitolea mfano kampuni ya PanAfrican
Energy na Maurel et Prom ambapo idadi ya wafanyakazi wazawa imefikia
zaidi ya asilimia 90.

Sangweni pia aliieleza Kamati ya
Bunge kuhusu kazi inayofanywa na Mamlaka hiyo katika kusimamia shughuli
za utafutaji na uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo ya kusimamia shughuli ya uchukuaji wa data na
uchorongaji katika Kitalu cha Eyasi Wembere kilicho chini ya TPDC ambapo
visima vifupi vitatu vya utafiti wa awali vimeanza kuchorongwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu alieleza kuhusu faida mbalimbali za uwepo wa Gesi
Asilia nchini ikiwemo kuwa kama chanzo cha kuzalisha umeme nchini kwani
zaidi ya asilimia 57 ya umeme unaozalishwa unatokana na Gesi Asilia.

Aidha alieleza kuhusu juhudi
mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa PURA
inatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuongeza bajeti ya Taasisi
hiyo, kukamilisha muundo wa Taasisi hiyo na kuipatia fedha kwa wakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *