Kamati ya kudumu ya bunge yaipongeza wizara ya madini

Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini
kutokana na mafanikio kadhaa yaliyojitokeza katika Sekta ya Madini
ikiwemo Ukuaji wa Sekta ya Madini, Ukusanyaji wa Maduhuli na kueleza
kwamba, matunda yanaonekana huku kazi nyingi zikifanywa kwa Mfumo wa
Kisasa.


Pongezi
hizo zinafuatia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa  shughuli na
miradi iliyotekelezwa na Wizara na Taasisi zake kwa Kipindi cha Nusu
Mwaka  kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 ambazo zimewasilishwa kwa kamati
hiyo.
Kamati
ya Bunge imeleza kuwa, Sekta ya Madini imepiga hatua huku ikitoa
pongezi kwa Rais Dkt. John Magufuli na kueleza kuwa, sababu za
kuitenganisha iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kuanzishwa kwa
Tume ya Madini zinaonekana.
Aidha,
Kamati hiyo imetoa ushauri kwa wizara na kuitaka kuendelea kuisimamia
sekta ya madini kwa lengo la kuhakikisha kwamba sekta hiyo inazidi
kuchangia zaidi katika pato la taifa, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
taifa.
Awali,
akitoa taarifa kwa Kamati kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha na
utekelezaji wa majukumu ya wizara, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara
ya Madini, Augustine Ollal ameieleza Kamati ya Bunge kuwa, kwa kipindi
cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2019, Sekta ya Madini ilishika nafasi ya
pili kwa kasi ya ukuaji wa asilimia 13.7 ukichangiwa zaidi na ongezeko
la uzalishaji wa madini ya dhahabu na makaa ya mawe. 
Ameongeza
kuwa, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2019, Wizara kupitia Tume ya
Madini ilikusanya maduhuli ya kiasi cha Tsh. 242,531,173,458.83 sawa na
asilimia 103 ya lengo la Nusu Mwaka na asilimia 51.5 ya lengo la
makusanyo ya mwaka mzima.
Akizungumzia
mauzo ya madini ya dhahabu kwenye masoko ya madini ameeleza kuwa, kwa
kipindi cha Julai hadi Novemba 2019, kiasi cha dhahabu kilichozalishwa
katika masoko ya Geita, Chunya, Kahama, Mwanza na Mara kimeongezeka hadi
kufikia Kilo 5,546.6 ikilinganishwa na kiasi cha kilo 1,188.4 kipindi
cha nyuma kabla ya kuendeshwa kwa kaguzi za kimkakati katika maeneo
hayo.
‘’Mheshimiwa
Mwenyekiti, wizara ilikusudia kuanzisha masoko ya madini katika Mikoa
yote nchini, hadi kufikia Mwezi Desemba, 2019 jumla ya masoko 28 na
vituo vya ununuzi wa madini 25 yalikuwa yameanzishwa nchini,’’ amesema
Ollal.
Pia,
ameeleza kuwa, baada ya wizara kufanya kaguzi za kimkakati za leseni za
biashara ya madini katika maeneo ya Geita, Mara, Mwanza , Chunya,
Kahama na  Arusha kumekuwa na ongezeko la leseni  308  kutoka leseni 696
za biashara ya madini kabla ya ukaguzi wa kimkakati kufikia leseni
1004,  huku ongezeko hilo likitajwa  kuchangiwa na kuimarika kwa
utendaji wa Tume ya Madini.
Vilevile,
ameitaja Maabara ya Taasisi ya Jilojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) na kueleza kwamba, ilipata ITHIBATI ya Kimataifa ya uchaguzi wa
sampuli za dhahabu kwa ya tanuru kutoka shirika la SADCAS na kueleza
kwamba, itasaidia sampuli zinazopimwa katika maabara za taasisi hiyo
kuweza kuaminika kimataifa na kuruhusu upimaji wa sampuli kutoka nje ya
nchi na kupunguza gharama za uchunguzi wa sampuli zetu nje ya nchi.
Naye,
Waziri wa  Madini Doto Biteko, akizungumza katika kikao hicho, ameileza
Kamati hiyo kuwa, Wizara ipo katika mchakato wa kuandaa andiko la
kuanzisha Bodi ya Kusimamia Wajiolojia nchini ambayo inalenga katika
kudhibiti Wajiolojia wanaotoa taarifa zisizo sahihi kuhusu tafiti za
madini nchini. 
Aidha,
Waziri Biteko ameishukuru Kamati hiyo kwa pongezi na kuendelea
kuishauri  na kueleza kuwa, mafanikio hayo yanatokana na kujituma kwa
watumishi wa wizara na taasisi zake ikiwemo msukumo mkubwa unaotolewa na
Rais Dkt. John Magufuli kwa Sekta hiyo.
Aidha,
ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa madini nchini kutekeleza shughuli
zao kwa kufuata Sheria na taratibu zilizowekwa na kueleza kuwa, wizara
inataka kuona wafanyabiashara wanafanya biashara zao bila kukamatwa
kamatwa huku akisema kuwa, wizara itaendelea kuboresha mazingira ya
biashara na shughuli za madini kuwawezesha watanzania zaidi kushiriki na
kumiliki uchumi wa madini.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila,
ameieleza Kamati hiyo kuwa, katika mkakati wa kuwaendeleza watumishi na
kuwajengea uwezo, jumla ya watumishi 12 leo Januari 20, 2020 wanaondoka
kuelekea nchini India kwa ajili ya kujifunza  masuala ya Jimolojia
ambayo yanahusisha pia masuala ya utambuzi wa madini na uthaminishaji
madini na kuongeza kuwa, wizara itaendelea kuangalia nafasi zaidi katika
nchi nyingine ikilenga kuwajengea uwezo watumishi kuweza kusimamia
sekta hiyo.
Mbali
na taarifa ya upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu, taarifa
nyingine iliyowasilishwa kwa kamati hiyo ni taarifa kuhusu  hatua
zilizofikiwa katika uendelezaji wa Leseni za Mradi wa Liganga na
Mchuchuma . Vikao kati ya Wizara na taasisi zake vimeanza leo Januari 20
na vinatarajiwa kuendelea hadi Januari 22, 2020.