KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA LEGAL AID YAACHA FURAHA ARUSHA

  • YAMKUA MJANE BI. MWANAIDI HUSSEIN KWA KUREJESHEWA ARDHI YAKE ILIYOCHUKULIWA MWAKA 1997 KWA MATUMIZI YA UMMA

Na Seif Mangwangi, Arusha

KAMPENI ya msaada wa kisheria ya Mama Samia legal aid imemsaidia Bi Mwanaidi Mussa Hussein mkazi wa Unga limited jijini Arusha kurejeshewa eneo lake la ardhi lililotwaliwa mwaka 1997 kwa manufaa ya umma baada ya kusubirishwa kwa miaka mingi.

Akizungumza kwenye viwanja vya mnara wa mwenge jijini Arusha, Bi mwanaidi amemshukuru Rais Samia suluhu Hassan kuwezesha kampeni hiyo na kumuombea miaka mingi zaidi ya uongozi.

Mjane Bi.Mwanaidi Hussein akiwa katika banda la msaada wa kisheria la samia legal aid Arusha

“Mimi ni mjane Mume wangu alifariki miaka mingi iliyopita, ofisi ya kata ilichukua eneo langu na kuahidi kunifidia nikakubali lakini hata hivyo wamekuwa wakinizungusha kila nilipokuwa nikifuatilia, nashukuru sana leo nimepewa hati ya kiwanja change licha ya kutokuwa na uwezo wa kukijenga lakini angalau nimepata,”amesema na kuongeza:

“ Namuombea Samia miaka mingine kumi sio tano tena, kwa kweli amenisaidia sana, mfano mimi tangia mume wangu amefariki mwaka 2001 ni miaka mingi sana, nimepambana kusomesha wanangu kwa kuuza mandazi kwenye karai hadi leo hii huku nikihangaikia kiwanja changu hatimaye leo nimekipata kweli ni furaha sana, kampeni hii ina msaada mkubwa sana,”amesema.

Hamisa Mhando Afisa sheria mkuu wizara ya katiba na sheria anasema Bi. Mwanaidi alikuwa na changamoto ya ardhi yake kuchukuliwa na shule ya msingi ungalimited ili kuongeza majengo ya shule na kumuahidi kumpatia eneo lingine bila kutekeleza agizo hilo.

Amesema mapema mwaka jana baada ya kufuatilia kwa muda mrefu  aliahidiwa kupewa ardhi nyingine eneo la oljoro lakini hata hivyo hakuweza kupatiwa hati wala kiwanja alichoahidiwa na hivyo kuendelea kuishi bila ya matumaini ya kupata kiwanja.

“Jumatatu alifika hapa na mimi niliweza kumpeleka ofisi za ardhi jiji ambao walidai kuwa kulikuwa na tatizo la kimfumo lakini waliweza kumsaidia na sasa wamempatia ardhi yake,”amesema Hamisa.

Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama samia Legal Aid ilihitimishwa jijini Arusha Machi 8, 2025 wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ambapo wakazi wengi walifanikiwa kutatuliwa migogoro iliiyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.