Katibu mkuu ccm awaomba wananchi kupuuza kauli za viongozi zinazowahimiza kufanya starehe badala ya kufanya kazi

Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally, amewaomba wananchi
kupuuza sera na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya
siasa nchini zikitaka wananchi wale bata (wafanye starehe) badala ya
kufanya kazi jambo ambalo likiachwa bila kukemewa litafanya kuwa na
taifa legelege la kupenda starehe badala ya kazi.


Dkt.
Bashiru amesema kuwa, katika nchi ambayo wananchi wanapambana
kujikomboa kiuchumi, hasa katika nchi zetu za Afrika ambazo bado tupo
nyuma kimaendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, kutokea
kiongozi mmoja kuwaambia watu wafanye kazi kwa starehe ni usaliti mkubwa
wa mapambano ya kiuchumi ambayo kama taifa tunayahimiza.

Katibu
Mkuu ameyasema hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa
ofisi ya CCM Kata ya Bwanjai wilayani Misenyi tarehe 28 Desemba, 2019 na
kuzungumza na wanachama na wananchi waliojitokeza katika ukaguzi huo.

“Nchi
hii ambayo tunaongoza mapambano ya kujikomboa kiuchumi, inamuhitaji
kila mtu kwa nafasi yake kuhimiza kufanya kazi kwa bidii, na huku CCM
kuna kauli mbalimbali za kuhimiza kazi zikiwemo, Hapa Kazi tu, Kazi na
Maendeleo, Uhuru na Kazi na Kazi ni Utu, ila kuna baadhi ya Vyama wao
wanahubiri kazi na starehe, na huo ndio utofauti wa Chama kiongozi na
Vyama vya uchaguzi.’’ Dkt. Bashiru ameeleza

Ameongeza
kwa kusisitiza kuwa, “Unaposema kazi na bata, maana yake ni
kudharirisha wanawake na mama zetu ambao wakati wote wamekuwa wakifanya
kazi kusomesha watoto wao, wakifanya kazi kulisha familia zao, na sote
hapa ni matokeo ya juhudi kubwa za mama zetu, ambao kuwambia wale bata,
ni sawa na kuwataka washinde kwenye starehe huku watoto wakidharirika
kwa kutokwenda shule, hizi ni kauli za kipumbavu za Vyama vya uchaguzi,
ambazo hatuna budi kuzidharau na kuzipuuza.”

Aidha
ameongeza kuwa, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwa chama cha kutetea
haki za wanyonge na kitaendelea kusisitiza sekta zote za serikali
zikiwemo afya, elimu, miundombimu na maji kutoa huduma kwa wananchi bila
usumbufu wala ubaguzi na kuthamini utu wa watu wote.

Mkutano
huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali
wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera mama Costancia Buhiye na
Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanal Mstaafu Denis Mwila

Ikumbukwe
kuwa, Dkt. Bashiru yupo nyumbani kwake Bukoba mkoani Kagera kwa
mapumnziko ya siku kumi, na anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mapema
mwezi Januari, 2020.