Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akisaini kitabu cha
wageni kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga wakati alipofika
wilayani hapo kushiriki kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu
usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya
Mungu. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Thomas Apson na kulia
ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wajumbe wa Kikao cha
ujirani mwema (hawapo pichani) kilichojadili kuhusu usimamizi
shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu
ambacho kimejumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara na Halmashauri
za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro. Kikao kimefanyika
katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw.
Emmanuel Bulayi (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa Kikao cha
ujirani mwema kilichojumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara,
Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro kuhusu
usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya
Mungu ikiwa ni pamoja na udhibiti wa uvuvi haramu. Kikao kimefanyika
katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya Viongozi na Wataalam
kutoka Wizara na Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na
Simanjiro wakisikiliza mada kwenye Kikao cha ujirani mwema kilichojadili
kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la
Nyumba ya Mungu. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko
wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Serikali kwa kushirikiana na wadau imepanga kudhibiti Uvuvi haramu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Mkoani Kilimanjaro.
Haya yamesemwa na Katibu Mkuu
anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah baada ya kumalizika
kwa kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu ulinzi na usimamizi wa
rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kikao hicho
kiliwajumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na
Wilaya za Mwanga, Moshi na Simanjiro kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga.
Dkt. Tamatamah amesema kupitia
kikao hicho wamejadili kwa kina kuhusu tatizo la Uvuvi haramu
unaofanyika kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na kutoka na maazimio ambayo
Wizara na Halmashauri zilizoshiriki pamoja na wadau watakwenda
kuyasimamia utekelezaji wake lengo likiwa ni kudhibiti shughuli za uvuvi
haramu katika bwawa hilo. Moja ya maazimio hayo ni pamoja na udhibiti
wa uuzwaji wa samaki wadogo kwenye masoko yanayosimamiwa na halmashauri.
“Samaki wadogo wanavuliwa pasipo
halali na huwa wanauzwa kwenye masoko ambayo yapo chini ya halmashauri,
hivyo tumekubaliana wote kuwa baada ya siku saba halmashauri zihakikishe
samaki hao hawauzwi tena katika masoko na hii itasaidia kuwafanya
wavuvi kupunguza au kuacha kuvua samaki hao kwa kuanza kukosa wanunuzi,”
alisema Dkt. Tamatamah.
Dkt. Tamatamah amesema sera ya
uvuvi ya mwaka 2015 imekasimu majukumu ya usimamizi wa rasilimali za
uvuvi kwa serikali kuu kwa maana ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya
TAMISEMI kupitia Halmashauri na majukumu mengine yamekasimiwa kwa
wavuvi na wadau wengine.
Vilevile amesema kuwa Wizara
inayojukumu la kutunga sera, sheria na kanuni lakini TAMISEMI kupitia
halmashauri zinaowajibu wa kuzisimamia na kuhakikisha kwamba utekelezaji
wake unafuatwa. Lakini kwa upande wa wavuvi wanaowajibu wa kushiriki
katika ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi kwa kuwa wao ndio
wanufaika wa kwanza.
Mkutano huo umewahusisha wadau wa
pande zote kwa maana ya wizara, halmashauri na wadau ili kuwa na mkakati
wa pamoja badala ya kila mmoja kuwa na mkakati wake kuhusu udhibiti wa
uvuvi haramu na kuhakikisha rasilimali za uvuvi kwenye bwawa la Nyumba
ya Mungu zinalindwa na kusimamiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,
Mhe. Thomas Apson amesema moja ya changamoto iliyojitokeza katika
udhibiti wa uvuvi haramu ni kwamba kila wilaya ilikuwa ikifanya doria
kwa wakati wake hivyo wavuvi wakiona doria inafanyika katika wilaya moja
wanakimbilia kwenye wilaya nyingine. Lakini kutokana na makubaliano ya
kikao, sasa utawekwa utaratibu mzuri wa doria zinazofanyika ili kutotoa
tena nafasi kwa wavuvi kufanya uvuvi haramu.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhe.
Zephania Chaula amesema moja ya changamoto iliyopo ni ya uingizwaji wa
zana haramu za uvuvi kupitia mipakani. Hivyo ameziomba mamlaka
zinazohusika kuhakikisha zana hizo hazipitishwi kwani hiyo ni moja ya
njia ya kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya uvuvi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi amesema kwamba wizara
inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili
waweze kuunganishwa na taasisi za fedha kama Benki ya Maendeleo ya
Kilimo (TADB) ambazo zipo tayari kuwakopesha na hivyo wataweza kununua
zana sahihi na zenye ubora kwa ajili ya kufanyia shughuli za uvuvi.