Katibu mkuu wa ccm awaonya wana ccm……”mwenyekiti wala katibu mkuu hawana wagombea wao”

Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally ameweka bayana kuwa
wanachama wote wanaotarajia kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika
uchaguzi Mkuu wana haki sawa, na hakuna mwanachama wa Mwenyekiti wala
Katibu Mkuu kama ambavyo baadhi ya wanachama wanavyoanza kuwalaghai
wajumbe wa vikao kuwa wametumwa na Mwenyekiti na Katibu Mkuu kugombea.



Amesema
kuwa ni vema, kila mmoja ajiandae kueleze sifa zake na kwa nini
anadhani anafaa kuliko mwingine na sio kutumia sababu za kilaghai za
kutumwa na Mwenyekiti, Katibu Mkuu ama Wazee, kwani anafahamu kuwa
Mwenyekiti hana Mgombea yeyote, na  yeye (Katibu Mkuu) hana Mgombea kwa
kuwa wagombea wote ni wakwao na wanahaki sawa.

Ameyasema
hayo jana tarehe 18 Januari, 2020 katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini wa kupokea  taarifa ya kazi ya Mbunge wa jimbo hilo
Ndg. Peter Serukamba.

“Wapo
watarajiwa wanataka kugombea udiwani, ubunge, ni haki yao, na zipo
kanuni na mila zetu, na mojawapo ni wewe kusema sifa zako sio kusema
uongo, kusema nimetumwa na Katibu Mkuu kugombea hapa ni uongo, sema sifa
zako, kusema nimetumwa na Mwenyekiti (Rais) ni uongo, nimetumwa na
wazee, ni uongo, umewafanyaje wazee wakutume, sema sifa zako, una agenda
gani, una sifa gani, una uwezo gani, unauzoefu gani, una mipango gani,
na unaweza nini sio kusema uongo..”

Amesisitiza
kuwa, watu ambao hawana sifa wanajiuza kwa kusema uongo, Mwenyekiti
(Mhe. Rais Magufuli) hana Mgombea, wagombea wote ni wa kwake na
Mwenyekiti hawezi kuwa na mgombea mmoja, hata yeye wakati anagombea
hakusema ametumwa na yeyote ila sifa zake zilimuuza kwa wapiga kura.

Aidha,
Katibu Mkuu kabla ya mkutano huo ametembelea na kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Chankele –
Mwamgongo, upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bitale na Kituo cha Utafiti wa
mbegu za michikichi cha Kihinga

Ziara
hii imeongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma Ndg. Amandus Nzamba,
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ndg. Kirumbe Ng’enda, Mkuu wa Mkoa
huo Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, wabunge ni Ndg. Daniel
Nsanzugwako, Hasna Mwilima na Peter Serukamba.