Katibu mkuu wa wizara ya ujenzi amkalia kooni mkandarasi

Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi)
Arch. Elius Mwakalinga, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya
Chunya -Makongolosi kwa kiwango cha lami kuhakikisha anamaliza mradi huo
ndani ya muda wa mkataba na si vinginevyo.

Aidha,
ameongeza kuwa hatamuongezea mkandarasi huyo muda wa kumaliza kwani
muda aliopewa ulikuwa unamtosha kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Hayo
ameyasema mkoani Mbeya alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua
hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara hiyo ambapo pamoja na mambo
mengine amemuelekeza mkandarasi huyo kuongeza vitendea kazi na wataalamu
ili kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliobakia.

“Natarajia
utaongeza vifaa na wataalamu ili kuhakikisha kazi hii inakamilika kwa
wakati, pia ukumbuke kuwa sitakupa muda wa nyongeza hivyo fanya juhudi
ili umalize mradi huu ndani ya muda”, amesisitiza Arch. Mwakalinga.

Katibu
Mkuu huyo amefafanua kuwa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi
yenye urefu wa KM 39 unajengwa na mkandarasi China Railway 15 Bureau
Group Corporation kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 59 ambazo
zote ni fedha za Serikali na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2020.

Arch.
Mwakalinga amemuelekeza pia mkandarasi kutumia muda wake wote kuwa
katika eneo la mradi hata ikiwezekana kuongeza masaa ya kufanya kazi
usiku na mchana.

“Fanyeni
kazi usiku na mchana ili kuepukana na changamoto za vipindi vya mvua na
hakikisheni barabara hii inajengwa kwa viwango vya ubora zaidi”,
amesema Arch. Mwakalinga.

Naye,
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mbeya
Eng. Mwita Magesa, amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa mpaka sasa ujenzi wa
mradi huo umefikia asilimia 53 ukilinganisha na muda wa mkataba
uliotumika ambao ni miezi 23 sawa na asilimia 85.19 ya muda wa mkataba.

Eng.
Mwita ameeleza kuwa mkandarasi mpaka sasa ameshakamilisha kujenga
tabaka la juu la barabara kwa mawe yaliyosagwa KM 9.18, lami ya prime KM
6.78 na kazi zingine za ujenzi wa makalvati madogo na madaraja makubwa
matatu zikiendelea.

Mradi
wa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 ni
sehemu ya barabara ya Mbeya-Rungwa yenye urefu wa KM 293 inayounganisha
mkoa wa Mbeya na mikoa jirani ya Singida na Tabora ambapo barabara hii
ikikamilika itaongeza zaidi fursa za kimaendeleo kwa wananchi kiuchumi
na usafirishaji.