Kero zaidi ya 50 zawasilishwa kwenye mkutano wa hadhara wa mkuu wa mkoa wa shinyanga

 

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme leo Februari
28,2024 ameanza ziara yake ambapo amesikiliza, kutatua kero na changamoto
mbalimbali zaidi ya 50 za wananchi wakazi wa  Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Changamoto hizo zinagusa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya
Maji, Elimu, Ardhi pamoja na miundombinu ya Barabara.

Wananchi hao pamoja na mambo mengine wamehoji ni lini
serikali itakamilisha ujenzi wa soko kuu la Mkoa wa Shinyanga ambalo
lilitarajiwa kukamilika Mwaka jana mpaka sasa halijakamilika, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ametumia nafasi hiyo kumuagiza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha soko hilo linakamilika kufikia
Tarehe 30,05 Mwaka huu 2024.

Pamoja na changamoto mbalimbali zilizowasilishwa leo,
wananchi wameendelea kuitaka serikali kuboresha miundombinu ya Barabara kutoka
Ndala kuelekea Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambapo wamesema ni
muhimu Barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa usumbufu
unaojitokeza na kusababisha ajali mbalimbali.

Katika mkutano huo wa hadhara kero na changamoto nyingi
zimetokana na migogoro mbalimbali ya ardhi na kwamba mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Mhe. Christina Mndeme katika ziara hiyo ameongozana na wataalam mbalimbali wakiwemo
wakuu wa idara ambapo  changamoto za
wananchi zimetolewa ufafanuzi.

Pia wananchi wameikumbusha serikali kuharakisha zoezi la
mikopo inayotolewa na Halmashauri kwani wengi wao wamekuwa wakijiingiza kwenye
mikopo yenye riba kubwa (Mikopo umiza au kausha damu) na kupelekea kukimbia
familia zao ambapo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amewaomba
wananchi kuwa wavumilifu na kwamba serikali bado inaboresha mfumo katika mikopo
ya Halmashauri.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amesema zoezi
la kupokea kero za wananchi linaendelea ambapo katika ziara yake kesho Alhamis
Februari 29 kuanzia majira ya saa tano asubuhi atakuwa katika Manispaa ya Kahama.

RC  Mndeme pia  Machi mosi, 2024  atazungumza na wananchi wa Halmashauri ya
Msalala kupitia Mkutano wa hadhara 
ambapo saa tano asubuhi atafanya Mkutano wa hadhara katika kata ya Kakola,
na baadaye Saa nane mchana atazungumza na wananchi wa kata ya Segese.

 

Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga akiwasilisha kero yake kwenye
mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina
Mndeme kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi leo Jumatano
Februari 28,2024.


 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *