- Inaituhumu Rwanda kufadhili waasi wa M23 kuua raia,kutaka kumpindua Rais Tishekedi
Na Seif Mangwangi, Arusha
MAHAKAMA ya Afrika ya watu na Haki za Binaadam (AfCPHR),imeanza kusikiliza kesi ya ukiukwaji wa mkataba wa kimataifa wa haki za Raia na uvamizi wa mipaka ya nchi iliyofunguliwa na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), dhidi ya nchi ya Rwanda katika Mahakama hiyo.
Kesi hiyo inayosikilizwa chini ya Majaji kumi wa Mahakama hiyo, DRC inaishitaki Rwanda kwa kuvamia mipaka ya kimamlaka ya Kongo, kuchochea machafuko ya mara kwa mara Mashariki mwa Kongo na kusababisha uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu kwa watoto, kina Mama , wazee na wagonjwa.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa leo Februari 12 , 2025 ilifunguliwa mahakamani hapo mwaka 2023, kufuatia nchi zote mbili kuwa mwanachama wa mahakama hiyo ambapo DRC inaituhumu Rwanda kufadhili kikosi cha waasi cha M23 ambao wanataka kuipindua Serikali halali ya nchi hiyo chini ya Rais Tish2kedi.
DRC inadai kupitia mapigano hayo yaliyoanza mwaka 2021 chini ya ufadhili wa Serikali ya Rwanda na washirika wake yamesababisha watu zaidi ya 500,000 kukimbia makazi yao, huduma za kijamii ikiwemo hospitali na shule kufungwa na kupelekea watoto zaidi ya 20,000 kukosa masomo.

Madai mengine ya Kongo dhidi ya Rwanda yanahusu nchi hiyo kuhifadhi wahalifu wa kivita bila ya kuwachukulia hatua za kisheria au kuwarudisha nchini DRC ili waadhibiwe kisheria.
Aidha hati hiyo ya madai inadai kuwa Kwa kuleta kesi hiyo katika Mahakama hiyo ya kikanda, Kongo inatumaini mahakama hiyo itaitia hatiani Rwanda kwa ukiukwaji wa Mamlaka ya Mipaka ya Kiutawala ya Kongo, kuchochea machafuko na kusababisha uvunjifu mkubwa haki za binadamu.
Kutokana na madai hayo, Kongo inataka Mahakama iiamuru Rwanda kuacha kufadhili vikundi vya waasi, kuondoa wanajeshi wake katika mipaka ya Kongo na kulipa fidia kwa waathirika wa machafuko yaliyosababishwa na vita hivyo.
Katika majibu yake, mbali ya kukanusha kuhusika kwenye mgogoro wa vita inayoendelea Nchini Kongo dhidi ya waasi wa M23, Rwanda pia imedai kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kulingana na mkataba wa uanzishwaji wake na kuitaka kutupilia mbali.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa kesho Februari 13 kwa mawakili wa pande mbili za Rwanda na DRC kujibu hoja kabla ya mahakama hiyo kukaa na kupanga siku ya kutolea uamuzi.
