Kijana aliyefungwa minyororo chumbani afunguliwa shinyanga

Kijana wa miaka 26, mkazi wa Old
Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga, aliyekuwa amefungwa minyororo
chumbani kwa miezi miwili, Shadrack Johanes amefunguliwa na kufanyiwa
usafi, kuvishwa nguo na kuanza kupatiwa matibabu ya afya ya akili.


Shadrack Johanes, alifunguliwa minyororo
hiyo jana mara baada ya Nipashe kuripoti habari kuhusu ukatili uliokuwa
unafanywa dhidi ya na ndugu zake.

Kwa miezi miwili alikuwa amefungwa
minyororo mikono na miguu akiwa mtupu huku akila chakula kwenye chumba
ambacho alikuwa anajisaidia haja kubwa na ndogo.

Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya
Shinyanga, Panuela Samwel, alisema kijana huyo amefunguliwa minyororo
hiyo na serikali itatoa matibabu kwake bila malipo.

Panuela Samwel ameongeza kuwa,
wameambiwa na wataalamu wa afya kuwa matibabu ya kijana huyo
yanatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita hadi mwaka mzima. Ofisa huyo wa
serikali alisema kama kijana huyo hatapona, watampatia rufani kwenda
jijini Dodoma kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mirembe jijini
Dodoma.

”Tukio alilofanyiwa kijana huyu ni la
kinyama sana, nashukuru vyombo vya habari kwa kuliibua, bila ninyi
huenda kijana huyu angefia ndani. Sisi sasa kama serikali, tutamtibu
kijana huyu bure kabisa, na leo (jana) anaanza kupatiwa dawa ambayo
itachukua muda wa miezi sita hadi mwaka mzima.” amesema Panuela Samwel
ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga.

Akiwa kwenye familia ya kijana huyo
jana, ofisa huyo aliitaka isimnyanyapae tena, badala yake imweke kwenye
mazingira mazuri pasi na kumfunga minyororo.

Mratibu wa Magonjwa ya Afya ya Akili,
Brigita Nyangare, alisema kijana huyo hana tatizo kubwa sana la akili
kwa kuwa ana bado ana uwezo wa kuongea na hajapoteza kumbukumbu.

Alisema atakuwa karibu na kijana huyo
muda wote wa matibabu yake na atakuwa anafuatilia anavyoishi nyumbani
hadi pale atakapojiridhisha amepona.

Akizungumza kwa shida, Johanes aliwaomba
ndugu zake wasimfungie ndani tena. Ndugu wa kijana hauyo waliomba
msamaha kutokana na kumfungia na kuahidi kufuata maagizo waliyopewa na
serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *