Kitambulisho cha taifa na cha kupigia kura havitahusika kupigia kura novemba 24-rc ndikiloNA MWAMVUA MWINYI,PWANI
 

SERIKALI Mkoani
Pwani, imetoa rai kwa wananchi kupuuza baadhi ya watu wanaowahadaa kuwa
kitambulisho cha Taifa -NIDA na cha kupiga kura wataweza kupigia kura
katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vitongoji na vijiji Novemba 24
mwaka huu,suala ambalo ni upotodhaji mkubwa.
 

Aidha imeweka bayana
takriban watu 680,000 wanatarajiwa kujiandikisha kwenye daftari hilo,
hivyo wamehamasishwa kujiandikisha ili kuwa na haki ya kupiga kura
kuchagua viongozi wanaowataka.
 

Akihamasisha umuhimu
wa kujiandikisha katika daftari hilo hadi octoba 14 mwaka huu ,wakati
alipokwenda kutimiza haki yake ya msingi kujiandikisha kituo cha
Mwanalugali ‘A ‘ Kibaha ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo
alisema kitambulisho cha Taifa na cha kupigia kura havitahusika katika
zoezi la kupiga kura.
 

“Nimetumia haki yangu
ya msingi kujiandikisha ,nimejiandikisha wa 123  lengo la kituo hiki ni
kuandikisha watu 1,332, na kimkoa tunatarajia kuwa na watu 680,000
,alifafanua Ndikilo.

“Wapo baadhi ya watu
wanahadaa wenzao kwamba hakuna ulazima wa kujiandikisha kwenye daftari
la wakazi ,na badala yake watatumia vitambulisho kama si cha uraia basi
cha kupiga kura,sio kweli mtapoteza haki yenu ya msingi”

Hata hivyo Ndikilo alieleza ,suala la kupiga
kura ni la wananchi wote siyo la watu wachache ili kuondoa malalamiko
kuwa viongozi waliochaguliwa hawafai wakati wao hawakushiriki hilo ni
tatizo.
Alisema taratibu zote zimekamilika ikiwa ni
pamoja na fedha ambapo wasimamizi tayari wameshateuliwa  kwa ajili ya
uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka.

Katika hatua nyingine
,anaeleza ni wakati wa mabadiliko na kujitambua kuacha kuchagua
viongozi wanaokingiwa kifua na fedha zao kutoa rushwa bali wachague
viongozi walio bora ,watakaowaletea maendeleo.


Nae ofisa uchaguzi wa halmashauri ya Mji wa
Kibaha ,Saidi Kayangu alisema ,wamejipanga kuweka mazingira rafiki na
kusimamia haki kwa makundi yote ili kuondoa vikwazo wakati wa uchaguzi.


Alitoa wito kwa
wananchi wenye sifa kushiriki katika uchaguzi huo muda utakapowadia
kwani ushiriki wao ndio mchango katika maamuzi na washiriki bila rushwa.

Kayangu alihimiza,
wananchi kujiorodhesha kwenye rejesta za wakazi katika mitaa yote 73 ili
kupata takwimu kwa uhalisia hasa idadi ya kuanzia umri wa miaka 18 na
kuendelea,:”hatua hii anaelezea itasaidia maandalizi ya uchaguzi kama
vile idadi ya karatasi za kupiga kura.