- Yatoa fulana 1000 zitakazovaliwa na washiriki wanaume kwa wanawake
- RC Makonda asema ni wiki ya kula nyama choma na kusikiliza kero za wananchi
Na Seif Mangwangi, Arusha
KATIKA kunogesha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Kiwanda cha kuzalisha chandarua chenye dawa ya kuua mbu na bidhaa mbalimbali za nguo na kilimo nchini, A to Z kimetoa msaada wa zaidi ya fulana 1000 ambazo zitavaliwa na washiriki katika maadhimisho hayo ikiwemo wanaume.

Akitoa taarifa ya maandalizi ya maadhimisho hayo kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum Dkt. Doroth Gwajima, leo Februari 25, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema maandalizi ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika kitaifa Jijini Arusha yamekamilika.

Amesema wadau mbalimbali wamejitokeza kunogesha maadhimisho hayo kutokana na nia yao njema kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkoa wa Arusha na kuhakikisha hakuna kitu kinaharibika.
“Mheshimiwa Waziri, tumepanga kumuheshimisha mheshimiwa Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, nipende tu kusema kwamba maandalizi kwaajili ya siku hii muhimu kwa kina Mama yamekamilika na kila idara imejipanga vizuri, kwanza kabisa tutakuwa na siku saba za kazi kuelekea kilele chenyewe ambapo shughuli mbalimbali tumepanga kuzifanya,”amesema.
Amesema kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, kutakuwa na kliniki ya kusikiliza kero za wananchi, ambapo idara mbalimbali za Serikali zitakuwa jijini Arusha na hivyo kuwataka wananchi kufikisha kero zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

“Watu wa sekta ya ardhi watakuwepo kwaajili ya kusikiliza migogoro ya ardhi na wataipatia ufumbuzi, lakini pia watu wa TRA watakuwepo kwaajili ya kusikiliza matatizo ya wananchi kuhusiana na kodi hivyo nipende tu kuwaalika wakazi wote wa Arusha na mikoa ya Jirani wafike jijini kwetu kwaajili ya kero zao kusikilizwa,”amesema.
Amesema tarehe 7, siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na hafla ya kula nyama bure ambapo zaidi ya ng’ombe 100 mbuzi na kondoo zaidi ya 80 pamoja na nyamapori wanatarajiwa kuchinjwa.

“Tunataka kutumia maadhimisho haya kuwaonyesha wakazi wa Arusha na viunga vyake kwamba tunaweza kutumia nishati safi kuchoma nyama na tusiharibu mazingira, “amesema Makonda.
Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya maadhimisho hayo, Hindu Ally Mbwego amesema zaidi ya wageni 7000 wanatarajia kuhudhuria katika maadhimisho hayo wakiwemo kutoka jamii za pembezoni Wamaasai, Barbaig na Datoga.
“Mheshimiwa Waziri kamati ya Hamasa imeendelea na kazi yake vizuri, mpaka februari 18 tulikuwa na idadi ya washiriki zaidi ya 7000 zaidi ya lengo la awali la watu 400,…pia tunashukuru sana kiwanda cha AtoZ ambao wametoa T-shirt 1000, ambazo zitavaliwa siku hiyo, na pia wanaume 1000 wameshathibitisha kushiriki,” amesema Bi.Hindu.

Maadhimisho hayo yataenda sanjari na kongamano ambalo mada mbalimbli zitajadiliwa ikiwemo mada kuhusiana na mchango wa utalii kwa mwanamke na mafanikio ya azimio la Beijing kuleta usawa wa kijinsia.
Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum, Dkt Doroth Gwajima amezitaka taasisi zote za serikali nchini kutumia nafasi zao kuhamasisha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani na kutoa ripoti ofisini kwake.


Mbali ya waziri gwajima viongozi mbalimbali pia walihudhuria ikiwemo washauri wa Rais Samia, Angela Kairuki na Sofia Mjema, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum, wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Arusha.
