Kiwanda cha kuchakata nyama cha tanchoice kuzalisha ajira 500

Kiwanda
cha kuchakata nyama na machinjio ya mifugo cha Tan Choice kinatarajiwa
kuzalisha ajira 500 za kudumu katika fani mbalimbali nchini mara baada
ya kuanza kazi rasmi mapema Machi, 2020.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa kiwanda hicho Bw. Albert Kilalah wakati
akiwasilisha taarifa ya kiwanda kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki
alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda pamoja na
kusikiliza na kutatua changamoto zilizowasilishwa za kiwanda hicho.
Waziri Kairuki alifanya ziara hiyo (Ijumaa tarehe 17 Januari, 2020)
ambapo alipata fursa za kukagua maeneo ya kiwanda hicho chenye uwezo wa
kuchakata nyama bora (organic meet) na kusema amevutiwa na kupongeza
jitihada za uwekezaji huo mkubwa.
“Nimefarijika kuwa hadi sasa mmeweza kutoa ajira zaidi ya 300 na ni
matarajio yenu kutoa ajira 500 kiwanda kitakapoanza kazi mapema mwaka
huu na tutaendelea kuwaunga mkono ili kuwafikia wananchi kwa utoaji wa
bidhaa bora zenye uhakika,”alisema Waziri Kairuki.
Waziri alieleza kuwa huo ni uwekezaji mkubwa wenye tija ambapo hadi sasa
umegharimu zaidi ya Tshs bilioni 25, hivyo ni kiwanda cha mfano kwa
nchi za Afrika ya Kati na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia malengo
ya kiwanda hicho.
Aidha Msemaji wa Mradi huo alieleza uwepo wa kiwanda hicho ulizingatia
mahitaji ya nyama bora na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyopo nchini
kwa kuzingatia umuhimu wa wawekezaji na wafanyabiashara.
“Bodi ya Tan Choice ilivutiwa uwekezaji kwenye sekta ya nyama kutokana
na uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji nchini chini ya Serikali ya
Awamu ya Tano na uwepo wa mifugo itayowezesha uendeshaji wa miradi huu
na kukidhi soko la ndani na nje ya nchi,” alisema Bw. Albert Kilalah
Alieleza kiwanda hicho ni fursa kwa wafugaji na wafanyabiashara wa
mifugo nchini ambapo zaidi ya watu 10000 watanufaika kiuchumi kwa
kuzingatia uhakika wa soko la nyama na mazao yatokanayo na mifugo.
Alifafanua, Kiwanda hicho kitakuwa cha pili kwa ukumbwa kwa nchi za
Africa Mashariki kikifuatiwa na kiwanda cha Ethiopia ambacho kina uwezo
wa kuchinja ng’ombe 3,000, kondoo na mbuzi 6,000 kuzalisha zaidi ya tani
300 kwa siku.
“Kiwanda kitakapokamilika kitakuwa kikubwa na bora cha aina yake katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati  na kitakuwa na uwezo wa kuchinja
ng’ombe 1,000 na mbuzi na kondoo 4,500 kwa siku nyama na mazao mengine
yatakayozaliswa na kiwanda yatazingatia ubora na usalama,”alisema
Kilalah.
Alisema kuwa, Tan Choice inatarajia kuuza nyama soko la nchi za Uarabuni
Mashariki ya Kati ikiwemo Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia pamoja
na masoko yatakayo jitokeza ikiwemo China, Malaysia, Vietnam na
Indonesia pamoja kutumia fursa ya soko huru la kibiashara
litakaloazishwa barani Afrika na kuuza nyama hiyo.
Akihitimisha taarifa hiyo aliomba Serikali kuendelea kuboresha barabara
kutoka eneo la kiwanda hadi Kongowe iboreshwe kwa viwango vya lami ili
kurahisisha usafirishaji wa mifugo kiwandani na pamoja na nyama
zitakazozalishwa kwenda uwanja wa ndege, bandarini na masoko ya ndani.
Aidha aliomba kuwe na uboreshwaji wa minada ili kuwe na uhakika wa upatikanaji wa wanyama wengi na wenye uhakika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Asupter Mshama alishukuru wawekezaji
katika Wilaya yake, na kuwatoa shaka juu ya utatuzi wa changamoto
walizonazo na kuendelea kuunga mkono jitihada zao kwa kuhakikisha huduma
muhimu ikiwemo, nishati ya umeme, maji, barabara na mawasilino
vinazingatiwa ili kuwa na manufaa ya uzalishaji wa kiwanda.
=MWISHO=

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *