Kukosekana kwa Ulinzi wa watoa taarifa kikwazo cha mapambano dhidi ya Rushwa Afrika

Na Seif Mangwangi, Arusha

BARA la Afrika linaelezwa kuwa bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya ulinzi wa watoa taarifa na kufanya sababu hiyo kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha juhudi za kupambana na rushwa katika nchi nyingi barani humo.

Hayo yameelezwa jana Februari 3, 2025 jijini Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya Umoja wa Afrika dhidi ya rushwa(AUABC), Seynabou Ndiaye Diakhate alipokuwa akifungua kikao cha nane cha wajumbe wa bodi hiyo.

Hata hivyo amesema pamoja na changamoto kubwa ya ukosefu wa ulinzi wa watoa taarifa amezipongeza nchi wanachama wa umoja huo ambazo zimetekeleza azimio la umoja wa Afrika kwa kutuga sheria na kanuni za kuhakikisha usalama wa watoa taarifa zinatunzwa.

wajumbe wa bodi ya ushauri ya umoja wa Afrika ya mapambano dhidi ya Rushwa wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa bodi hiyo
Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Afrika dhidi ya Rushwa akisoma hotuba yake katika kikao cha nane cha ushauri cha wajumbe wa bodi hiyo kinachoendelea jijini Arusha

“Katika mjadala wa mwaka huu, ni muhimu kutambua kuwa baadhi ya Nchi Wanachama zimefanikiwa kuanzisha mifumo ya ulinzi wa watoa taarifa, ikiwa ni pamoja na sheria na kanuni zinazowalinda.,”amesema.

Amesema  baadhi ya nchi ambazo bado hazijachukua hatua za kuanzisha mifumo ya kulinda watoa taarifa inahitajika juhudi zaidi ili kuhakikisha kuwa kila nchi inatekeleza wajibu wake katika kulinda watoa taarifa na mashahidi.

Diakhate amesema  suala la haki za binadamu na haki za kijamii na kiuchumi limekuwa na umuhimu mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na kwamba haki za binadamu haziwezi kustawi bila utawala bora na heshima kwa taasisi zinazohakikisha haki.

“Uwiano kati ya mapambano dhidi ya rushwa na haki za binadamu niza wazi, na hili limekuwa suala la majadiliano ya kimataifa, kama ilivyoonekana katika mikutano ya G-20 nchini Brazili, ambapo makubaliano ya kimataifa kuhusu uhusiano huu yalisisitizwa,”amesema.

Amesema gharama za rushwa ni kubwa, na imekuwa ikiathiri jamii nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na Afrika, ambapo hasara inayosababishwa na rushwa inakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 50 kila mwaka.

“Hii inaonyesha wazi kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo na ustawi wa bara la Afrika, na hivyo ni muhimu kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na tatizo hili,”amesema.

Amesema mjadala katika mkutano huo wa nane wa bodi hiyo unalenga kujadili mafanikio na changamoto zinazokabili mifumo ya watoa taarifa katika bara la Afrika ambapo watendaji wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wanajukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa mifumo hii inaimarika.

Mwaka 2023, Umoja wa Afrika ulitimiza miaka ishirini tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (AUCPCC) ambapo katika kipindi hicho mapitio ya utekelezaji wa mkataba huo yalionyesha maendeleo makubwa, hatua zilizochukuliwa, na mafanikio yaliyojiri.

Hata hivyo, changamoto kadhaa bado zinaelezwa kutatiza utekelezaji wake, ikiwa ni pamoja na mifumo duni ya ulinzi wa watoa taarifa.

Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Afrika dhidi ya Rushwa Seynabou Ndiaye Diakhate