Lhrc yakutanisha ustawi wa jamii, ofisi ya dpp, polisi dawati la jinsia kujadili changamoto wa ukatili wa kijinsia kuondoa vikwazo vinavyokatisha tamaa

Na Seif Mangwangi, Arusha 
KUTOKANA na mlolongo wa ngazi za
maamuzi kwenye ufuatiliaji wa mashauri yanayotokana na ukatili wa kijinsia kwa
watoto na wanawake, watu wengi wamekuwa wakikata tamaa na kushindwa kuripoti
matukio ya ukatili wa kijinsia na kujikuta wakiendelea kuumia pasipo kupata
msaada.

Wakili
Doto Joseph akiwasilisha mada kuhusiana na masuala ya ukatili wa
kijinsia katika mafunzo yanayotolewa chini ya kituo cha msaada wa
kisheria na haki za binaadam LHRC yanayoendelea jijini Arusha

Hayo yameelezwa leo Oktoba 17, 2019
Jijini hapa na Afisa Programu anayeshughulikia ,masuala ya kijinsia, watoto na
wanawake katika shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binaadam (LHRC),
Renatha Selemani.
Amesema kutokana na changamoto
hiyo, kituo cha LHRC kimelazimika kutoa mafunzo kwa maafisa ustawi wa jamii,
Maafisa polisi katika dawati la jinsia, 
mawakili, Hakimu na waendesha mashtaka wa Serikali katika mafunzo
yanayoendelea jijini Arusha kujadili namna ya kupunguza mlolongo huo na kesi
hizo kuharakishwa.
Lilian amesema kumekuwepo na
changamoto kubwa ya matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kutoripotiwa kwenye
vyombo vya kimaamuzi kutokana na kuwepo kwa mlolongo mrefu wa ngazi za
kimaamuzi na kuwafanya wanaotendewa vitendo hivyo kukata tamaa.
“Mfano dawati la jinsia polisi
wamekuwa wakipokea matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, hapa lazima
wazichunguze kama zina tija au la, baada ya hapo wanapeleka kwa mwanasheria wa
Serikali na yeye apitie awarudishie halafu ziandaliwe kupelekwa mahakamani,”anasema.
Anasema baada ya kupelekwa
mahakamani na kesi kusomwa, mahakimu na wanasheria wanaanza kusikiliza kesi
ambazo pia hutegemea ushahidi na hivyo kufanya kesi kuchukua muda mrefu jambo
ambalo limekuwa likikatisha tamaa.
Kwa upande wake Mwezeshaji katika
mafunzo hayo, Mwanasheria na Wakili wa Mahakama Kuu, Dotto Joseph amesema suala
la ukatili wa kijinsia ni suala pana ambapo wakati mwingine masuala hayo
yamekuwa yakifanyika katika ngazi ya familia kwa mume kumpiga mkewe na hivyo
kumalizana nyumbani bila kuripoti mashauri hayo kwenye ngazi za kimaamuzi.
Amezitaja changamoto mbalimbali
ambazo zinatakiwa kutatuliwa ili kurahisisha uendeshaji wa mashauri hayo kuwa
ni pamoja na kutolewa elimu ya mambo yanayopelekea ukatili wa kijinsia,
kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria pamoja na kukomeshwa kwa mila
potofu.
Kwa upande wake Afisa wa Polisi
kutoka kanda maalum ya Tarime, Claud Mtweve pamona na Lilian Mugwe Afisa Ustawi
wa jamii Halmashauri ya Wilaya ya Bunda wamesema ukatili wa kijinsia katika
maeneo yao ikiwemo wajane kulazimishwa kuolewa baada ya kufiwa na waume zao umekuwa
ukichangiwa na mila na desturi ambazo jamii imekuwa ikizirithi kutoka kwa
wazazi wao.
Afisa Program masuala ya jinsia, wanawake na watoto wa LHRC Renatha Seleman  akimsikiliza mtoa mada katika mafunzo hayo kuhusu ukatili wa kijinsia

  

Washiriki wa mafunzo ya ukatili wa kijinsia wakimsikiliza mwezeshaji Doto James (hayuko pichani), akieleza mazingira yanayosababisha watu wengi kutofikisha mashtaka yao