Maafisa kazi msimchonganishe Rais na wafanyakazi: Ridhiwani

  • Ni kuhusu malalamiko ya wafanyakazi wanaoumia mahala pa kazi
  • Watakiwa kutoa taarifa WCF kwa wakati

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI imewataka maafisa kazi kote nchini kutoa taarifa za wafanyakazi wanaoumia maeneo ya kazi kwa wakati ili waweze kupewa stahiki zao kwa wakati kama Sheria inavyotaka.

Aidha maafisa hao wametakiwa kusimamia maslahi ya wafanyakazi sehemu za kazi kwa uadilifu na weledi na kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya msingi dhidi ya watendaji hao.

Wito huo umetolewa leo Agosti 30, 2024 Jijini hapa na Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Ridhiwani Kikwete alipokuwa akifungua kikao kazi kati ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF), na maafisa kazi kote nchini.

Kikwete amesema baadhi ya maafisa kazi wa mikoa wamekuwa wakilalamikiwa kutotatua migogoro na malalamiko ya wafanyakazi jambo ambalo limekuwa likitoa taswira mbaya dhidi ya Serikali.

Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikijali maslahi ya wafanyakazi na ndio sababu imefanyia mabadiliko mswada wa sheria za huduma ya Jamii2024, hivyo maafisa wanaoshindwa kuhudumia wafanyakazi wanamkosea Rais na huko ni kumchonganisha na Rais wao.

” Niwakumbushe tu kwamba hamkupewa ofisi kuwa vitanda na nyumba zenu za kuishi, nataka kusikia mnatatua malalamiko ya wafanyakazi na sio kuwapatia majibu ya kashfa kama baadhi yenu ambavyo mmekuwa mkiwajibu wafanyakazi,” amesema.

Kikwete amesema tangu ameingia ofisini amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi kutotendewa haki maeneo ya kazi na kushangazwa kwanini yamekuwa yakimfikia yeye wakati kila mkoa una Afisa kazi ambaye angeweza kusikiliza malalamiko hayo na kuyatatua.

” Jukumu lenu maafisa kazi ni kusikiliza malalamiko na kwa shughuli zinazohusu WCF jukumu lenu ni kuandika na kutoa taarifa WCF, sio kugeuka washauri wa waajiri ili kudhulumu haki za wafanyakazi, ” amesema na kuongeza:
“andikeni vitu ambavyo mwisho wa siku wafanyakazi watapata haki zao na sio kuandika ili sheria ionekane haifai,” amesema.

Awali Mkurugenzi wa mfuko wa WCF, Dkt John Mduma amesema mfuko huo umefanyia mabadiliko makubwa mfumo wa utendaji wake wa kazi ambapo hivi Sasa huduma za mfuko zinapatikana kwa njia ya Mtandao kwa asilimia tisini.

Kamishna wa kazi nchini, Suzan Mkangwa amesema ofisi yake imekuwa ikishirikiana na mfuko wa WCF kuhakikisha malalamiko ya wafanyakazi yanatatuliwa kwa wakati.

Kikao hicho cha siku mbili kinatarajiwa kumalizika kesho ambapo Katibu Mkuu Wizara ya nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu Mary Maganga anatarajiwa kufunga kikao kazi hicho.