- Rais Neves wa Cape Verde awataka watoa haki kutibu majeraha ya mijeledi walopigwa waafrika
Na Seif Mangwangi, Arusha
RAIS wa Jamhuri ya watu wa Cape verde Jose Maria Neves amesema bara la Afrika bado linakabiliwa na tatizo la majeraha mengi ikiwemo mfumo wa ubaguzi wa rangi na dhulma zilizoanzishwa na mataifa ya nje kwa lengo la kutugawa.
Aidha amesema Bara la Afrika ambalo ni chimbuko la ubinadamu, bado linabeba makovu ya mijeledi mingi waliopigwa mababu zetu , vita vya udugu, ukabila uliotumika kutugawa mambo ambayo yanaendelea kuhatarisha maisha ya waafrika ya sasa na mustakabali wake.
Ili kukomesha mambo hayo Rais Neves ametoa wito kwa Mahakama ya Afrika ya watu na Haki za binaadam kutetea watu na jamii zilizopoteza Utu wake kutokana na ukoloni ili wapate fidia ya mateso hayo au kurejeshwa kwa rasilimali zilizotoroshwa.
Wito huo ameutoa leo Februari 3, 2025 Jijini hapa katika hotuba yake ya ufunguzi wa mwaka mpya wa mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binaadam ambapo shughuli mbalimbali za mahakama hiyo zinaanza rasmi.
“ Niruhusu niipongeze Mahakama hii tukufu kwa uamuzi wake uliokuwa makini wa ‘Kuendeleza Haki Kupitia Fidia’, sambamba na kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka huu 2025 inayosema: “Haki kwa Waafrika na Watu Wenye Asili ya Kiafrika kwa njia ya Fidia”. Amesema.
Amesema mtazamo kama huo unaonyesha nia na ujasiri wa watendaji wa Mahakama hiyo kukabiliana na kuamua kutatua tatizo la ukosefu wa haki wa kihistoria ambao umekuwepo katika bara la Afrika ambapo suala la fidia linatakiwa kuchukuliwa uzito zaidi ya fidia tu ya mali.
Rais Neves amesema suala la fidia linajumuisha masuala ya msingi kama afya, elimu, na utamaduni hivyo ni muhimu kuangaliwa kwa umakini kwaajili ya kuponya majeraha ya zamani na kwa ajili ya kujenga mustakabali unaofafanuliwa kwa usawa na ustawi wa jamii za Kiafrika.
Rais Neves amesema bara la Afrika lina historia kubwa duniani kutokana na watu wake kuteswa na kunyiwa haki huku rasilimali zake zikichukuliwa na kupelekwa nchi za ulaya.
Amesema jamii nyingi barani Afrika zinapaswa kupewa fidia kutokana na mateso mengi waliyoyapata wakati wa ukoloni kabla ya kupata uhuru hivyo ni jukumu la watoa haki kutofanya upendeleo ili kuleta usawa.
” Bila kuwa na haki hakuna amani watu wengi wa Afrika walipokonywa maeneo yao ya kihistoria, ni jukumu la nyie mliopewea dhamana ya kutoa haki kutofanya upendeleo na badala yake mtoe haki kwa usawa,”amesema.
Amewataka waafrika kudumisha utamaduni wake kwa kuwa ni lulu dhidi ya mataifa mengine na ni elimu endelevu kwa vizazi vijavyo ili kuwawezesha kujua historia ya bara la Afrika.
Awali akimkaribisha Rais Neves, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binaadam Jaji Kmani Aboud amesema katika mwaka mpya wa mahakama, wamejipanga kutetea suala la fidia kwa walioumia kwa kukosa haki zao.
Amesema nchi ya Kenya na Bukinafaso ni mfano mmojawapo ya nchi zenye jamii zinazohitaji kupatiwa fidia kutokana na mateso mbalimbali waliyopitia wakati wa Ukoloni hivyo mahakama hiyo itajikita zaidi katika suala la fidia kwa mwaka huu wa mahakama.

Aidha Jaji Aboud amesema Mahakama ya Afrika iko tayari kutekeleza wajibu wake kwa kuendelea kuhukumu kesi kwa uadilifu, uhuru, na bila upendeleo kwa kuendeleza sheria za haki za binadamu na kuchangia katika kupatikana kwa haki ya upatanishi.
” Lakini hatuwezi kufikia lengo hili la mabadiliko peke yetu. Tunahitaji ushirikiano wenu kwa haraka, tunahitaji kujitolea kwenu bila kuyumbayumba, na tunahitaji maono yenu ya pamoja kwa ajili ya Afrika bora, yenye haki zaidi. Wito huu wa kuchukua hatua ni muhimu hasa kutokana na hali ya kutatanisha, duniani na ndani ya bara letu la Afrika, ya kurudisha nyuma haki za binadamu. Tunaona tabia ya kutia wasiwasi ya kupuuza haki za kimsingi, mara nyingi chini ya kivuli cha manufaa ya kisiasa au maslahi finyu ya kitaifa,” Amesema.
Katika muendelezo wa shughuli za ufunguzi wa mwaka mpya wa mahakama hiyo, kesho kutakuwa na semina ya Kimahakama ambapo wawakilishi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, Mahakama za kimataifa, kikanda na kitaifa.
Washiriki wengine ni vyombo vya Umoja wa Afrika vilivyo na mamlaka ya haki za binadamu, taasisi za kitaifa za haki za binadamu, wataalamu wa sheria na wawakilishi wa Vyama vya Wanasheria watashiriki.
Wengine ni mashirika ya kiraia, wanachuo, waandishi wa habari na wadau wengine wanaohusika katika kazi ya Mahakama na ulinzi wa haki za binadamu katika bara la Afrika wanatarajiwa kushiriki.
