Na Seif Mangwangi,Arusha
MAHAKAMA ya Afrika ya watu na haki za binaadam (AFCPHR), imezitaka nchi wanachama wa Mahakama hiyo kuiga mfano wa nchi ya Mali ambayo imebadilisha sheria kandamizi dhidi ya wanawake na watoto nchini humo.
Wito huo umetolewa Februari4,2025 na Rais wa Mahakama ya Afrika ya watu na haki za binaadam Jaji Imani Aboud katika hotuba yake ya ufunguzi wa semina kwa wawakilishi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, Mahakama za kimataifa, kikanda na kitaifa.
Washiriki wengine ni vyombo vya Umoja wa Afrika vilivyo na mamlaka ya haki za binadamu, taasisi za kitaifa za haki za binadamu, wataalamu wa sheria na wawakilishi wa Vyama vya Wanasheria watashiriki.
Wengine ni mashirika ya kiraia, wanachuo, waandishi wa habari na wadau wengine wanaohusika katika kazi ya Mahakama na ulinzi wa haki za binadamu katika bara la Afrika wanatarajiwa kushiriki.

Jaji Aboud amesema wanawake na watoto wamekuwa ni wahanga wakubwa kihistoria na hivyo ni wakati wa mataifa kuwalipa fidia na kuwafanya kuwa huru.
” Wanawake wamekuwa wakibakwa, wametengwa kwenye mirathi, sheria za kuolewa pia zimekuwa kandamizi, mfumo mzima umekuwa ukitoa upendeleo kwa wanaume, lakini ifikie mahali haya mambo yaishe, wanawake wapewe fidia kwa haya yote,” Amesema.
Amesema katika semina hiyo mambo mbalimbali kuhusiana na ukiukwaji wa haki za wanawake yatajadiliwa na kwa pamoja watatoka na kauli moja ambayo wataipeleka kwa wakuu wa nchi za Afrika wanachama wa Mahakama hiyo zenye sheria kandamizi dhidi ya wanawake ili kuzibadilisha.

Jaji Imani Aboud amesema nchi ya Mali ilishtakiwa katika mahakama hiyo kwa kuwa na sheria kandamizi dhidi ya wanawake na watoto na baada ya kupitia madai yaliyowasilishwa mahakamani hapo, Serikali ya Mali ilikutwa na makosa na kutakuwa kulipa fidia.
” Nchi ya Mali ilikuwa na sheria nyingi kandamizi dhidi ya wanawake na watoto lakini baada ya kushtakiwa imefanyia mabadiliko sheria zote, hii ndio fidia tunayoitaka, sio lazima fidia iwe ni fedha hata kubadilishwa kwa sheria ni fidia,” amesema.
Amesema kauli mbiu ya mahakama hiyo mwaka 2025 ni ‘kulinda haki za binaadam hasa wanawake kwa kuzingatia fidia’ hivyo semina hiyo imejikita katika kutafuta suluhu ya chanzo cha unyanyasaji wa wanawake pamoja na namna watakavyoweza kupewa fidia kutokana na unyanyasaji huo.
