Mahakama ya rufaa kusikiliza kesi 60 kwa njia ya mtandao

Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mhe. Richard Mziray akisikiliza kesi kwa   njia ya mtandao   “Video Coference”.
Mleta maombi Victor Binamungu (katikati) akiendelea na kesi yake dhidi ya Farida Hamza (kulia) na Geofrey Kabala (kushoto).
Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mhe. Shabani Lila akiendesha kesi kwa mfumo huo (kushoto) Wakili Dkt.  Masumbuko Lamwai.
Edward Chuwa na Aaron Kabunga wakifuatilia kesi baina yao wakiwa mkoani Mwanza.
(Picha na Mary Gwera – Mahakama)





Na Magreth Kinabo – Mahakama


Mahakama ya Rufani Tanzania
inatarajia kusikiliza jumla ya kesi 60 kwa kutumia mfumo wa mawasiliano
kwa njia ya picha maarufu jina la ‘Video Conference’ kuanzia Oktoba 9
hadi 16, mwaka huu.


Mfumo huo ambao husaidia
Mahakama ya Tanzania kuokoa fedha zinazotumika kuendesha kesi mbalimbali
na muda unaotumika, ikiwemo kuwapunguzia gharama wanazozitumia wananchi
kufika mahakamani kwa ajili ya kutafuta haki zao.


Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa leo na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Elizabeth Mkwizu, Mahakama hiyo itasikiliza kesi madai na jinai,
zilizoko katika Masjala ya Tabora, Mwanza, Bukoba na Mbeya, ambazo
zitasikilizwa na Majaji tofauti 17 wa Mahakama ya Rufaa.


Hivyo Mahakama hiyo, imeanza
kusikiliza kesi hizo mapema Oktoba 9, mwaka huu na imesi
kiliza jumla ya
kesi 12, zilizoko katika masjala ya Mwanza na Tabora kwa kutumia mfumo
huo.


Kwa upande wa Mwanza, Mahakama
hiyo imesikiliza kesi sita, kati ya hizo mbili zimesikilizwa na Mhe.
Jaji Stella Mugasha, katika Kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo
Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.


Jaji Mugasha alisikiliza
kesi  ya maombi namba 447/08/2019  ya Benjamin Manota na wenzake ambao
ni Mwana Selemani na Mussa  Benjamin dhidi ya Geita Gold Mine Limited,
‘The Principal  Secretary Minisrty of Minerals’ na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, kesi hiyo imeahirishwa kwa sababu wadawa wote wamefariki mpaka
watakapochaguliwa wasimamizi wa mirathi.


Kesi ya pili kusikilizwa na
Jaji huyo ni kesi ya maombi ya madai namba 31/08/2019 ya Tella Bupamba
dhidi ya Elisha Shija, inayohusu kuomba kuongezewa muda wa kibali cha
kuja Mahakama ya Rufaa na imesikilizwa pande zote mbili na yanasubiriwa
maamuzi yakiwa tayari wahusika watajulishwa.


Mahakama hiyo pia imeskiliza
kesi ya tatu ambayo imesikilizwa na Mhe, Jaji Richard Mziray. Kesi hiyo
namba 46/08/2019 ya Samwel Munsiro dhidi ya Chacha Mwikwabe.


Katika kesi hiyo Samwel ameomba
nyongeza ya muda kuwasilisha kibali Mahakama Kuu ili aweze kuwasilisha
maombi ya mara ya pili baada maombi ya awali kukataliwa, ambapo Mwikwabe
alidai kuwa maombi yake hayana mantiki.


Mhe. Jaji Mziray alisema amewasikiliza na kuangalia nyaraka, hivyo atatoa uamuzi na utakapokuwa tayari watapewa.


Jaji Mziray pia alisikiliza
kesi ya madai ya maombi namba 602/08/2017 ya Victor Binamungu dhidi ya
Geofrey Kabala na Farida Hamza.


Kesi hiyo ilihairishwa ili
kutoa nafasi kwa Farida kuwasilisha nyaraka ya maelezo ya kesi na Majibu
ya kiapo cha mleta maombi na kuhakikisha Victor na Geofrey wamezipata
ndani ya siku 14 kuanzia Oktoba 9 mwaka huu. 


Kesi ya tano kusikilizwa ni
madai ya maombi namba 63/17/2018 inayomhusu ‘The board of trustees of
the National Social Security Fund,’ iliyowakilishwa na Wakili Dkt.
Masumbuko Lamwai dhidi ya Nakara Hotel Limited, aliyewakilishwa na Dkt.
Tugemeleza Nshalla, imesikilizwa na Mhe. Jaji Shabani Lila.


Jaji Lila aliahairisha kesi hii kwa sababu Dkt. Nshalla anaumwa, hivyo itasikilizwa siku nyingine.


Kesi nyingine ya sita ya madai namba 32/08/2019 ya Edward Chuwa dhidi ya Aaron Kabunga, ambapo Chuwa aliomba kuongezewa muda.


Akisikiliza kesi hiyo Jaji
Lila alisema hayana msingi katika Mahakama hiyo na alimwamuru mleta
maombi kumlipa gharama aliziotumia mjibu maombi. 


Kwa upande wa masjala ya
Tabora kesi sita zimesikilizwa, ambazo ni ya madai moja na jinai
tano.Kesi hizi zimesikilizwa na majaji mbalimbali katika ukumbi wa
Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.


Kesi zilizosikilizwa ni ya
jinai namba 03/20/2015 ya Juma Kahukule dhidi ya Jamhuri,jinai namba 2/
‘B’/2015 ya Hamis Mashishanga dhidi ya Jamhuri, jinai namba 3/20/2016 ya
Chiganga Mapesa dhidi ya Jamhuri namadai namba 524/11/2018 ya Athumani
Mauruti dhidi ya Yusta Maganga.


Nyingine ni jinai namba 02/2016 ya Hussein Masoud dhidi ya Yusuph Said na jinai namba 4/2016 ya Yusuph Said dhidi ya Jamhuri.


Kesi nyingine zitasikilizwa
kwa kutumia mfumo huo, Oktoba 10, 15 na 16 mwaka huu. Mfumo huo ulianza
kutumika rasmi Desemba 5, mwaka 2018, ambapo Mahakama ya Tanzania
ilianza kutumia vitendea kazi vyake yenyewe.