Mahakama yakamilisha kusikiliza ushahidi wa kesi ya mwanafunzi kuvunjwa uti wa mgongo

Na Amiri Kilagalila-Njombe

Kesi
namba 141-2019 inayomkabili mwalimu Focus Mbilinyi anayetuhumiwa
kumvunja uti wa mgongo aliyekuwa  mwanafunzi wa shule ya msingi Madeke
wilayani Njombe Hosea Manga baada ya kumpa adhabu ya viboko 10 kwa madai
ya kukosa hesabu 10 imeendelea kusikilizwa katika mahakama ya hakimu
mkazi mkoa wa Njombe kwa kukamilisha mahojiano na mashahidi wawili wa
mwisho kutoka upande wa utetezi ambao ni wanafunzi wenza wa majeruhi
huyo.


Akitoa
utetezi mbele ya mahakama,Catheline Hongoli aliyekuwa kiongozi wa
darasa la  Hosea Manga anasema machi 21 ,2017 mwalimu wa hesabu aliingia
darasani na kuagiza wanafunzi ambao hawajafanya hesabu alizotoa kupita
mbele ,ambapo miongoni mwa wanafunzi waliopita alikuwepo Hosea Manga
ambaye aliadhibiwa viboko vitatu makarioni kwa kosa hilo.

Baada
ya adhabu hiyo mwalimu alitoka darasani na Hosea Manga akaelekea chooni
na kurejea akiwa darasani akiwa mzima na kisha baada ya muda mfupi
akadondoka na kushindwa kusimama hali ambayo iliwasukuma wanafunzi
kumwita mwalimu mkuu ambaye alimtoa na kumlaza nje ya darasa kijana
Hosea Manga.

Shahidi
wa pili na wa mwisho kwa upande wa uetetezi  Sephania Kyelula ambaye
pia ni mwanafunzi mwenza wa kijana Hosea anasema kabla ya kupatiwa
adhabu ya viboko vitatu Hosea Manga alikuwa na uwezo wa kutembea huku
akidai kuwa na maumivu ya mguu lakini mapema baada ya kuadhibiwa alitoka
na kwenda chooni na kisha kurejea darasani na muda mfupi akadondoka na
kushindwa kuinuka.

Kesi
hiyo inayoendeshwa na hakimu mkazi Ivran Msaki na kusimamiwa na
mawakili watatu wa upande wa utetezi ambao ni Liliani Gama,Octavian
Mbugwani na Innocent Kibadu imeahirishwa mpaka februali 4
itakaposikilizwa kesi ya majumuisho na kutajwa tarehe ya hukumu.