Majibu ya rais magufuli baada ya mwananchi kumtaka aachie fedha, maisha magumu

Rais Magufuli amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii na waache kulalamika kwamba hawana fedha wakati hawajitumi.


Magufuli
ametoa kauli hiyo leo Novemba 27, katika eneo la Shelui wilayani Igunga
mkoani Tabora akiwa njiani kuelekea Shinyanga baada ya mwananchi mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Abel Mbinga kumlalamikia maisha magumu.

“Rais
unafanya kazi nzuri sana, lakini fedha hakuna mheshimiwa, watu wana
hali mbaya, akina mama wananyang’anywa TV, friji kwa ajili ya mikopo
midogomidogo, tunaomba uachie fedha, mtaani, hali ngumu, mengine yote
hatuna shida na wewe, yakikamilika haya hata ukitawala milele,” amesema
Abel.

Majibu
ya Rais Magufli: “Usipofanya kazi hela zitaisha tu, ukitaka hela fanya
kazi, wapo watu wanalima sasa hivi, baadaye watapata pesa, wewe umekaa
kijiweni unataka pesa ikukute hapo? Labda ukaoe mwanamke mwenye pesa.
Cha bure hakipo, hata mimi sina, kinachotakiwa ni kuchapa kazi, maandiko
yanasema asiyetaka kazi na asile.

“Kalime
viazi au matikiti, ukiyaweka hapa barabarani yataliwa tu, ukitaka vya
bure hupati, nenda hata machimboni utapata kazi, unataka mkono wako uwe
soft (laini)… pesa hakuna, mimi sikuja hapa kuleta hela, nimekuja
kuwaambia Watanzania ukweli.

“Serikali
inatafuta pesa kwa ajili ya kujenga hospitali, barabara, maji na miradi
mingine ya maendeleo. Siwezi kutafuta pesa kwa ajili ya kukulisha wewe
na mke wako, na ukikosa (pesa) na mke anakukimbia….. Hata Ulaya
wanafanya kazi wasiwadanganye wapo wanaolala kwenye mashimo. Mimi
nimekwenda Ulaya wapo wenye shida kuliko huku, bahati mbaya kwao kuna
baridi. Ukitaka kutengeneza maisha yako chapa kazi,”