Makamu mwenyekiti wa uwt taifa ahimiza jamii kushirikiana na smaujata (wadau) mkoa wa shinyanga kutokomeza ukatili

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania wa
chama cha mapinduzi UWT Taifa, Bi. Zainabu Shomar ameiasa jamii kushirikiana na
serikali pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo kampeni ya shujaa wa maendeleo na
ustawi wa jamii Tanzania SMAUJATA  katika
juhudi za kupinga ukatili.

 

Ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 28,2023 wakati
akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Isaka
Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama ikiwa ni sehemu ya ziara ya UWT Taifa,
Mkoani Shinyanga.

 

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo
viongozi wa kampeni ya kupinga ukatili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga ambapo pamoja
na mambo mengine Bi. Zainabu Shomar ameitaka jamii kutofumbia macho vitendo vya
ukatili vinavyoendelea kutokea katika jamii hasa kwa wanawake na watoto.

 

Bi. Zainabu Shomar ametumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi
wa kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwa utekelezaji wa majukumu yao katika
kuibua masuala la ukatili huku akiwaomba wananchi kushirikiana na kampeni hiyo
ili kutokomeza ukatili unaoendelea katika jamii.

 

Amewasisitiza
wananchi  kuendelea kushirikiana na
serikali pamoja na wadau mbalimbali katika juhudi za kulinda maadili,ambapo
amehimiza wazazi na walezi kuwekeza zaidi kwenye malezi na makuzi bora kwa
watoto huku  akikemea tabia inayofanywa
na baadhi ya wanaume wanaofanya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa
Maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Bwana Solomon
Nalinga Najulwa amesema kampeni hiyo itaendelea kushirikiana na UWT pamoja na
viongozi wengine wa serikali katika hatua za kuibua na kupinga ukatili.

Kampeni ya SMAUJATA inafanyakazi
zake chini ya Wizara ya  maendeleo ya
jamii jinsia, wanawake na makundi maalum inayoongozwa na Waziri Dkt. Dorothy
Gwajima ambayo ilianzishwa na Waziri huyo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa
SMAUJATA Taifa Bwana Sospeter Bulugu ikiwa lengo ni kuisaidia serikali
kutokomeza ukatili Nchini.

Nao baadhi ya wanawake wa kata ya Isaka wilayani Kahama wamesema
licha ya juhudi mbalimbali zinazoendelea katika kupinga ukatili lakini
wameviomba vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa
wanaobainika kuhusika na matukio ya ukatili.

 

Wananchi hao wa kata ya
Isaka wakiwemo wanawake wameiomba serikali kutowafumbia macho wale wote
wanaobanika kufanya ukatili hasa kwa wanawake na watoto ambapo wamesema mmoja
ya changamoto zinazosababisha mmomonyoko wa maadili ni baadhi ya wanaume
kutelekeza familia zao na kukimbia kusikojulikana.

Viongozi wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania  wa chama cha mapinduzi UWT Taifa wameendelea
na ziara kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na
kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya CCM.

 

Katika kata ya Isaka
umoja wa wanawake Tanzania
 UWT umetembelea
na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo Bweni la Wasichana na Bweni la Wavulana
katika shule ya sekondari Isaka ambapo Mwenyekiti wa UWT kata ya Isaka Bi.
Nabila Kisendi amewapongeza na kuwashukuru viongozi wa UWT kwa kutekeleza lengohilo
la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania wa
chama cha mapinduzi UWT Taifa, Bi. Zainabu Shomar akizungumza kwenye mkutano
huo kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Mhe. Gasper Kileo akizungumza
kwenye mkutano huo, kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo
Jumatatu Agosti 28,2023. 

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga Santiel Kirumba akizungumza
kwenye mkutano huo, kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo
Jumatatu Agosti 28,2023. 


Mwenyekiti wa UWT kata ya Isaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila Kisendi akizungumza kwenye mkutano huo, kata
ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Mwenyekiti wa kamati ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga
Bwana Solomon Najulwa Nalinga jina maarufu Cheupe akizungumza kwa niaba ya
Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga leo kwenye mkutano huo, kata ya Isaka
Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Awali akiwasili Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa
Tanzania wa chama cha mapinduzi UWT Taifa, Bi. Zainabu Shomar katika mkutano
huo leo Jumatatu Agosti 28,2023.