
Na, Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Makandarasi wametakiwa kuhakikisha kuwa na wataalamu stahiki na kuzingatia ubora wa rasilimali katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya usimamizi wa rasilimali yaliyofanyika kwa siku tatu Jijini Arusha, Msajili wa Bodi ya Usajli Makandarasi Nchini Mhandisi Rhoben Nkori, amewataka Makandarasi kuhakikisha kuwa na wataalamu stahiki wanaofanya kazi kwa mujibu wa mkataba alioingia na kuwa waaminifu katika kazi zao ili kuzidi kupata mafanikio na kuaminiwa kwa wingi.
“Makandarasi wanatakiwa kutambua wajibu wao, kwa maana ya kuwa na wataalam stahiki bila kujali wanasimamiwa au hawasimamiwi, ili kukitokea changamoto waweze kukabiliana nazo, sambamba na kusaidiana kutoa taarifa za Makandarasi wasiokuwa waaminifu ili wapewe adhabu stahiki pindi wanapokiuka taratibu” amesema Mhandisi Nkori.
Aidha amewataka kuwa wasimamizi wazuri wa kazi zao, na kufanya kazi kwa ufanisi pindi wanapokabidhiwa miradi ili kuongeza imani kwa Makandarasi Wazawa.
“Kuliko upate kazi nyingi na uzifanye chini ya kiwango cha chini, ni bora ukapata kazi kidogo ukazifanya vizuri na ukajenga jina zuri, hatua hiyo itakupa nafasi ya kupata kazi nyingi na mafanikio makubwa” amesema Mhandisi Nkori.
Kwa upande wake Zephania Kwayu, mshiriki wa mafunzo hayo akitokea Kampuni ya Zekwa Trading Company LTD alisema kuwa, ushiriki wake kwenye mafunzo umemsaidia kuimarika katika eneo la usimamizi mzuri wa rasilimali mahali pa kazi za ujenzi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa na kukamilika kwa ubora unaotakiwa.
“Nimefarijika na kufurahia kuhudhuria katika mafunzo haya, tumepata mafunzo mazuri, tumekuwa na mijadala mizuri na tumeweza kushirikishana uzoefu baina ya makandarasi tuliohudhuria, wakati mwingine tulidhani tunajua lakini kupitia mafunzo haya tumejua mengi zaidi” amesema Kwayu.
Aidha, ameishukuru Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa uratibu wa mafunzo hayo na kuwataka makandarasi wengine kuhudhuria mafunzo yanayotangazwa na Bodi kwa ustawi wa tasnia ya Makandarasi.
Naye, Grace Mungunasi amesema kupitia mafunzo hayo yamemsaidia kuyapata majibu ya changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika upande wa usimamizi wa rasilimali mahala pa kazi za Ujenzi ambazo amekuwa akikumbana nazo.
Aidha ametoa rai kwa makandarasi kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ndani ya sekta ya ukandarasi kwa kuhakikisha wanazingatia ubora na usimamizi mzuri wa miradi wanayoitekeleza hali itakayowafanya kuaminika Zaidi na kutumiwa sana kwenye utekelezaji wa miradi mingi.
“Sisi Makandarasi tunayo nafasi ambayo hata ikitengenezwa miongozo ya namna gani, kama hakuna utekelezaji, wasimamizi watapata changamoto kwenye kusimamia hivyo, suala la ubora wa kazi zetu ni suala la msingi sana sambamba na ubora wa rasilimali” amesema Mungunasi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa mbali mbali hapa nchini.