Makongolosi wafurahia ujio wa shule ya mchepuo wa kingereza

Mkurugenzi wa Shule ya Holyland Pre &
Primary school iliyopo Makongorosi wilayani Chunya mkoani Mbeya,Lawena Nsonda
maarufu kwa jina la Baba mzazi  wakiwa na
mmoja wa walimu wa shule hiyo Tracila Joachim wakiwaangalia baadhi ya wanafunzi
wa shule hiyo wakicheza mchezo wa kubembea wakati wa mapumziko.(Picha na
Joachim Nyambo)
Na Joachim Nyambo,Chunya.
WAKAZI katika mji mdogo wa Makongolosi wilayani
Chunya wamesema kufunguliwa kwa shule ya mchepuo wa kingereza kwenye eneo lao
kumeanza kuleta mwamko na hamasa kwa wazazi kuacha tabia ya kuwatumikisha
watoto wao kwenye shughuli za machimbo na sasa wanaona elimu inaweza kuwakomboa
zaidi.
Wakazi hao wamesema wazazi wameanza kushawishika
baada ya kuona watoto wachache wanaosoma katika shule ya mchepuo wa
kingereza  ya Holyland Pre & Primary
school iliyopo katika mji wao wanaonesha uwezo wa kuongea kingereza na kuona
kama iwapo wataendelea kutochangamkia fursa za elimu nchini watoto wao wanaweza
kuendelea kubaki vibarua kwa wasomi.
Wakizungumza na waandishi wa habari wanaofuatilia
Masuala ya elimu na changamoto zake kwa watoto kwenye maeneo yaliyo na machimbo
ya madini wakazi hao wamesema jitihada za wadau mbalimbali katika kuchangia
sekta ya Elimu zinahitajika ili kuwakomboa watoto waishio kwenye maeneo ya
migoni.
Mmoja wa wakazi hao Listaa Rashid Masumaye alisema
ufunguaji wa shule bora na za kisasa jirani na maeneo ya wakazi waishio karibu
na zinakofanyika shughuli za machimbo ni moja kati vishawishi vikibwa
vinavyoweza kuwahamasisha wazazi kuona elimu kwa watoto wao inapaswa ipewe
kipaumbele kwanza kabla ya shughuli zao.
 “Mazingira yenye kumtamanisha mzazi yanaweza
kumsaidia kuwa na tama ya kuiga ili watoto wake waonekane wa kitofauti na wa
wenzake.Unajua hapa Makongolosi awali tulikuwa kama tunaishi kwa mazoea kwa
kuona mbona hata waliosoma wanafanana na watoto wetu tu wanashinda wote kwenye
kuchimba.Lakini kumbe ilikuwa ni kwakuwa hatukuona utofauti wa elimu inayoweza
kutolewa.”
“Ilikuwa ajabu kuona mtu akiongea kingereza..Kuna
mahafali moja ilifanyika hapa..ilileta mwamko mkubwa sana katika
Makongolosi..kwamba hivi kuna uwezekano mtoto mdogo namna hii kuongea
kingereza…Hapa imekuwa kama kituo cha utalii…vitoto vidogo viliwaacha watu
mdomo wazi..Kilichofuata sasa kila mzazi hata familia ambazo zimekuwa nyuma
kupeleka watoto shule wakaanza kusema lazima tujitahidi watoto
wasome.Vinginevyo watoto wetu watakuja kubaki vibarua wa hawa wanaochangamkia
elimu.”alisema Rashid.
Mkazi huyo aliwasihi wazazi kutumia fursa ya uwepo
wa sifa kubwa ya kielimu kwa mkoa wa Mbeya kwa kubadilika na kuendana na maisha
ya kisasa kwa kuwapeleka watoto wapate elimu jambo alilosema litakuja
kuwasaidia pia katika shughuli zao za uchimbaji kwakuwa watakuwa na utaalamu
zaidi ya wazazi wao.
Mkazi mwingine Edith Jairos alikiri kuwa tofauti na
miaka ya nyuma ambapo wakazi wa wilaya ya Chunya walikimbilia kazi za uchimbaji
na kusahau kupeleka watoto shuleni,utandawazi unaonekana kuwaunganisha wakazi
hao watu wa maeneo mengine hatua inayowasukuma kuanza nao kutafuta shule
zitakazowawezesha watoto wao kustahimili ushindani wa soko la ajira.
Edith alisema wapo wachimbaji ambao hivi sasa
wamefikia hatua ya kufanya mashindano kwa kila mmoja kutamba kwa kumpeleka
mtoto wake kwenye shule inayofanya vizuri zidi ya wenzie hatua aliyosema kwa
miaka ya nyuma ilikuwa ni ndoto.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Shule ya Holyland Pre
& Primary school,Lawena Nsonda alisema wakazi wa mji wa Makongolosi na
maeneo ya jirani ndiyo waliosababisha akabadili mawazo badala ya kufungua
Hospitali akaamua iwe shule ya mchepuo wa kingereza kulingana na mahitaji
yaliyokuwepo.
Nsonda alisema awali yeye na rafiki zake madaktari
ambao wengi wanafanya shughuli zao katika Hospitali zilzopo jijini Mbeya
walikuwa na mpango wa kufungua hospitali ili iweze kutoa huduma za matibabu kwa
wakazi wa maeneo hao ambao wengi wao shughuli zao ni za machimbo ya madini na
hasa dhahabu lakini baadaye wakazi walimfuata na kutana iwe shule.