Makundi na kutegeana kumechelewesha miradi kukamilika momba

Uwepo
wa makundi yasiyo na tija, kutegeana katika kazi na kutoshirikiana
baina ya watumishi kumesababisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa
katika halmashauri ya Wilaya ya Momba kuchelewa kukamilika.


Hayo
yamebainishwa jana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo
walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus
Mwangela alipokutana nao kutaka kufahamu sababu za kutokamilika kwa
wakati ujenzi wa miradi mbalimbali katika halmashauri hiyo.

Mmoja
wa watumishi amesema, “unapokuwa na mradi wa sekta fulani mfano afya,
kilimo au elimu watumishi wenzako wanakaa pembeni hawakusaidii, ni kama
wanakutegea waone utakavyoshindwa kitu ambacho sio sahihi, miradi yote
ni ya halmashauri na inalenga kuwanufaisha wananchi wote.”

Watumishi
hao wamesema baada ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wameona kuwa makundi
na kutoshirikiana havitaijenga halmashauri na hivyo wameapa kubadilika
na kufanya kazi kwa pamoja kama timu moja.

Aidha
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amesema anaamini
tatizo la kutoshirikiana baina ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Momba limeisha na watafanya kazi kwa pamoja.

Brig.
Jen. Mwangela ameongeza kuwa mara baada ya kikao hicho ameona
ushirikiano wa watumishi katika ujenzi wa Soko la Mazao la Kakozi ambapo
wote kwa pamoja wameonyesha nia kufanikisha ujenzi huo kwakuwa umesha
chelewa kwa zaidi ya miezi sita.

Naye
Msimamizi wa Ujenzi wa soko la mazao la Kakozi Aloyce Sakaya amesema
kwa sasa mradi huo utatekelezwa kwa kasi zaidi kwakuwa changamoto zilizo
sababisha ukachelewa ikiwa ni pamoja na kutoshirikiana baina yao
zimeondolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *