Malipo ya wakulima wa pamba simiyu kufanyika kielektroniki

Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akifungua Mkutano Mkuu wa Wadau wa pamba juu
ya malipo ya wakulima wa pamba kupitia T-PESA mkoani  Simiyu,
uliofanyika Oktoba 02, 2019 Mjini Bariadi.
 Baadhi ya viongozi  wa Serikali,
Vyama vya ushirika wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka akifungua Mkutano Mkuu wa Wadau wa pamba juu ya malipo ya wakulima
kupitia T-PESA Mkoani Simiyu, uliofanyika Oktoba 02, 2019 Mjini
Bariadi.
Katibu wa Itikadi na uenezi  wa
CCM Mkoa wa Simiyu, Bw. George  Mayunga akizungumza na Wadau wa pamba
katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa pamba juu ya malipo ya wakulima kupitia
T-PESA Mkoani Simiyu, uliofanyika Oktoba 02, 2019 Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Malipo ya
Wakulima wa zao la Pamba Mkoani Simiyu, katika msimu ujao yanatarajiwa
kufanyika kwa mfumo wa kielektroniki kupitia huduma ya T-PESA ya Shirika
la Mawasiliano Tanzania(TTCL).
Hayo
yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika
Mkutano wa Wadau wa Pamba uliowahusisha viongozi mbalimbali wa Chama na
Serikali, wataalam wa kilimo, viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika
(AMCOS), kwa lengo la kujadili  juu ya malipo ya wakulima wa zao hilo
kupitia huduma ya T-PESA uliofanyika Oktoba 02, 2019  mjini Bariadi.
Mtaka amesema
kuwa sambamba na mfumo wa ulipaji wa fedha za wakulima wa pamba kwa
njia ya Kielekroniki taarifa zote za kilimo zitapatikana kwa njia hiyo
huku akiongeza kuwa mfumo huo utasaidia kuondokana na hasara katika
vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS) iliyokuwa inasababishwa na baadhi
ya viongozi wasio waaminifu.
“Tumewaleta
hapa TTCL tunataka tufanye digital farming(kilimo kidigitali) malipo ya
pamba, mambo yote ya pamba na kilimo kwa ujumla yawe kwenye kiganja
chako kwa sababu leo hakuna nyumba ambayo haina simu; ni vizuri elimu
hii viongozi wa AMCOS muifikishe kwa wakulima ili wawe  na uelewa wa
pamoja,” alisema Mtaka.
Akizungumza
katika Mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano  Tanzania 
(TTCL) Waziri Kinamba amesema mfumo  huo mpya utaanza kutumika katika
msimu ujao na utawasaidia wakulima kupata fedha zao kwa usalama,
urahisi, kwa wakati na kupunguza matumizi yasiyofaa.
“Lengo letu
ni kutoa suluhu ya matatizo mbalimbali yanayojitokeza katika vyama vya
msingi vya ushirika kama upotevu wa fedha, uporaji na tunaamini wakulima
wakipata pesa zao kidigitali itaondoa changamoto hizo na kuwafanya
wakulima kuwa na maisha bora kutokana na uchumi utakaoboreka baada ya
mauzo watakayofanya kupitia TTCL PESA,” alisema Kindamba.
Kwa upande
wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Ushirika Mkoa (SIMCU), Emmanuel
Mwelele amesema  kuwa mfumo huu ni mzuri na unalenga kwasaidia wakulima
kupata fedha zao kwa usalama na akaahidi kuwa viongozi wa chama hicho
watatoa elimu kwa vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS) ili wakulima wote
wawe na uelewa wa pamoja.
Hadi sasa
mkoa wa Simiyu una wakulima wa pamba wapatao 314,000 na matarajio ya
uzalishaji katika msimu wa mwaka huu yalikuwa ni  kilo milioni 180,
ambapo hadi sasa jumla ya kilo milioni 148 zimekusanywa kutoka kwa
wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *