Mama aua mtoto wake kwa kumnywesha sumu ya kuulia wadudu mbeya


Na Esther Macha – Malunde 1 blog Mbeya 


JESHI la Polisi Jijini Mbeya linamshikilia mwanamke aitwaye Silvia Sande
(28) Mkazi wa Nsongwi kwa tuhuma za kumuua mwanae mwenye umri wa mwaka
mmoja na miezi miwili kwa kunywesha sumu ya kuulia wadudu kisha mwanamke
huyo nae kunywa sumu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Mkoani mbeya, Ulrich Matei amesema tukio
hilo limetokea Septemba 16,2019 saa 4 asubuhi katika kijiji cha
Nsongwi kilichopo Kata ya Ijombe, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya
Vijijini.
Alisema  mtuhumiwa alikunywa sumu ya kuulia wadudu chumbani kwake kwa
lengo la kujiua kisha kumnywesha sumu hiyo mtoto wake mdogo aitwaye
Asifiwe Baini mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili, mkazi wa
Nsongwi juu.
Hata hivyo alisema mtuhumiwa na mtoto wake baada ya tukio hilo
walikimbizwa kituo cha afya Igawilo ambapo mtoto huyo alifariki. 
Kamanda Matei alisema jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea
kumshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi na mara baada ya upelelezi
kukamilika atafikishwa Mahakamani. 
Aidha alisema chanzo cha tukio kinachunguzwa.