Mama aua mtoto wake wa miaka miwili ili apate utajiri kishirikina alivyoelekezwa na sangoma wa sumbawanga

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei
Na Esther Macha,Mbeya
WATU wanne wanashikiliwa na Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mtoto, Tamali Simon (2), ambapo miongoni mwa watuhumiwa ni mama mzazi wa mtoto huyo akidaiwa kushirikiana na watu hao kufanya unyama huo.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei amesema jana kwamba watuhumiwa hao walikamatwa wakati wa msako maalum uliofanywa na Polisi Mei 6, mwaka huu saa 4.00 usiku katika Kijiji cha Iwindi Kata ya Utengule Usongwe Mji Mdogo Mbalizi.
Kamanda Matei amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Rehema Kasela (36) ambaye ni mama mzazi wa mtoto, Riziki Muhema (20) mkazi wa Mtakuja Mbalizi 3, Estar Msongole (52) mganga wa kienyeji mkazi wa Sumbawanga, Mtumwa Haonga (65) mganga wa kienyeji mkazi wa Mtakuja Mbalizi ambao wote wanatuhumiwa kumuua mtoto Tamali mwenye umri wa miaka miwili na miezi mitatu.
Aidha Kamanda Matei amesema chanzo cha tukio hilo ni tamaa za kupata utajiri kwa njia za ushirikina na baada ya mtuhumiwa ambaye ni mganga wa kienyeji kuwapa masharti yaliyopelekea kifo cha mtoto huyo.
Akielezea zaidi Kamanda Matei amesema Mei 4, mwaka huu saa 2.00 usiku katika Kijiji na Kata ya Iwindi Tarafa ya Usongwe mtoto Tamali alikutwa ameuawa kwa kunyongwa shingo na mtu asiyejulikana na mwili wake kutelekezwa.
Amesema baada ya tukio hilo Polisi walifanya msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa katika maeneo tofauti na kwamba wakati wa mahojiano watuhumiwa walikiri kuhusika kwenye tukio hilo baada ya kupewa masharti na mganga wa kienyeji.
“Polisi walipofanya upekuzi nyumbani kwa mganga wa kienyeji walikuta vifaa mbali mbali vya uganga na dawa za kienyeji za aina mbali mbali, upelelezi wa tukio hilo unaendelea na mara baada kukamilika watafikishwa mahakamani,”amesema.