Mamia wajitokeza kufanyiwa uchunguzi saratani ya matiti

Dkt. Ndigwake Mallango (kulia) akimuelekeza Bi. Mekitilda
Wamala jinsi ya kujifanyia uchuguzi wa awali wa saratani ya
matiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila.

Mtaalam wa mionzi, mawimbi sauti na usumaku wa Hospitali ya
Mloganzila Mariam Ndosa (kulia) akichukua vipimo vya urefu na
uzito kabla ya Bi. Masha Jum kufanyiwa uchunguzi wa awali wa
saratani ya matiti.
Muwakilishi kutoka MEWATA mkoa wa Pwani Dkt. Deograsia
Mkapa akitoa elimu kwa kina mama kuhusu ugonjwa wa saratani
ya matiti, ambapo zaidi ya kina mama 200 wamejitokeza kwa ajili
ya kufanyiwa uchunguzi wa awali katika Hospitali ya Mloganzila
kati ya hao 45 wamekutwa na viashiria.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili- Mloganzila,
Dkt Julieth Magandi akiwa katika picha ya pamoja na watoa
huduma mara baada ya kumalizika kwa zoezi la uchunguzi wa
awali wa saratani ya matiti lililofanyika kwa siku mbili.
**************************************
Dar es salaam 27-10-2019
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Chama cha
Madaktari Wanawake Tanzania-MEWATA- imefanya zoezi la uchunguzi wa awali
wa saratani ya matiti bila malipo kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya ugonjwa
huo na kuhamasisha jamii umuhimu wa kujichunguza mapema.
Zoezi la uchunguzi limefanyika kwa siku mbili ambapo kina mama zaidi ya 200
wamehudumiwa huku 45 wakigundulika kuwa na viashiria vya saratani ya matiti
hivyo wanahitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka MNH-Mloganzila Dkt. Lulu Sakafu ametaja
huduma zilizotolewa kuwa ni elimu ya ugonjwa wa saratani ya matiti, dalili zake
na jinsi ya kujichunguza mwenyewe.
“Kujichunguza ni muhimu hasa kwa kina mama ambao ndio waathirika wakubwa
wa saratani ya matiti kutokana na uwepo wa vichocheo (Hormone) katika miili yao
ambavyo vinaweza kuchangia kupata ugonjwa huu’’ amesema Dkt. Sakafu.
Kwa upande wake muwakilishi kutoka MEWATA ambaye pia ni Daktari Bingwa
wa magonjwa ya saratani Dkt. Sikudhani Muya, amesema tatizo la saratani ya
matiti ni kubwa na huathiri wanawake kati ya umri wa miaka 28 hadi 50 kwa
asilimia kubwa, na ni asilimia moja tu ya wanaume hukutwa na ugonjwa huu.
“Uchunguzi kama huu husaidia kugundua iwapo mtu anaviashiria vya saratani ya
matiti na kisha hufanyiwa uchunguzi wa kina na kupelekwa kwa madaktari bingwa
wa magonjwa ya saratani kwa hatua zaidi” amefafanua Dkt. Muya.
Saratani ya matiti ni ya pili katika saratani zinazowapata wakina mama hapa nchini
ya kwanza ikiwa ni saratani ya shingo ya kizazi.