Mamia ya waombolezaji wajitokeza kumzika mtoto wa mkuu wa majeshi aliyefariki kwa ajali ya ndege

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mamia
ya wananchi kutoka mikoa ya Simiyu, Mara, Shinyanga, Mwanza na Dar es
Salaam wameshiriki katika mazishi ya mtoto wa Mkuu wa Majeshi  marehemu
Nelson Mabeyo aliyekuwa rubani wa ndege ya Shirika la Auric Air, ambaye
alifariki Septemba 23, 2019 kwa ajali ya ndege iliyotokea katika Uwanja
mdogo wa Seronera  uliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani
Mara.Mazishi
hayo yamefanyika Septemba 26, 2019 katika Kijiji cha Masanzakona wilaya
ya Busega Mkoani Simiyu, ambapo yalitanguliwa na ibada ya mazishi
iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yuda Tadei lililipo
kijijini hapo ambapo ni nyumbani kwao na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,
Jenerali Venance Mabeyo.

Akihubiri
wakati wa ibada ya mazishi, Askofu Michael Msonganzila, Jimbo Katoliki
Musoma amewasihi waombolezaji wote kuendelea kuifariji na kuiombea
familia ya Mkuu wa Majeshi ili wapokee msiba huo kwa jicho la imani,
masikio ya imani na kama mpango wa Mungu.

Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akitoa
salamu za serikali  amesema “marehemu Nelson Mabeyo alikuwa  kijana
mcheshi na mchapakazi leo hatuko naye tena nitoe pole kwa familia ya
Jenerali Mabeyo, sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea niwaombe
tuendelee kuwaombea katika kipindi hiki kigumu Mwenyezi Mungu awape
ustahimilivu.”

Naye
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akizungumza  kwa niaba ya
wananchi wa mkoa wa Simiyu na wakuu wa mikoa ametoa pole kwa familia ya
Mkuu wa Majeshi na kumshukuru kwa namna Mkuu  alivyowaunganisha watu wa
Masanza, Busega na Simiyu katika masuala mbalimbali ya  ikiwemo Ujenzi
wa Kanisa ambalo ibada ya mazishi ya marehemu Nelson imefanyika.

Kwa
upande wake  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenrali Venance Mabeyo
amewashukuru watu wote walioshirikiana na familia yake tangu msiba wa
mwanaye Nelson ulipotokea , ambapo amesema kama familia hawauchukulii
msiba huo kama adhabu bali makusudi ya Mungu mwenyewe kwa mtoto wao .

Mazishi
ya marehemu  Nelson Mabeyo yalihudhuriwa na  watu mbalimbali wakiwemo
viongozi wa dini, viongozi na Maafisa wa JWTZ walioko kazini na
wastaafu, mawaziri na manaibu waziri, makatibu wakuu, wakuu wa Taasisi,
viongozi wa Vyombo vya Usalama, wabunge, Wakuu wa mikoa ya Simiyu, Mara,
Shinyanga, Kagera, Kigoma, Mwanza na Dar es salaam , kamati ya ulinzi
na usalama ya Mkoa wa Simiyu na wakuu wa wilaya.