Marekani yasema wanajeshi wake 34 walijeruhiwa na wanapatiwa matibabu baada ya shambulizi la makombora la iran

Wizara
ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesema makumi ya Wanajeshi wa nchi
hiyo walijeruhiwa na kupatwa na matatizo ya kisaikolojia kufuatia
shambulizi la makombora la Iran dhidi ya kambi mbili za kijeshi za nchi
hiyo huko Iraq mapema mwezi huu, licha ya utawala wa Washington hapo
awali kudai kuwa hakuna askari wake hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa
katika shambulizi hilo


Katika
kikao na waandishi wa habari mjini Washington jana Ijumaa, Jonathan
Hoffman, msemaji wa Pentagon alisema, “askari 34 hivi sasa wanapatiwa
matibabu kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia, msongo wa
mawazo na madhara mengine ya ubongo kufuatia shambulizi la Iran la
Januari 8. Wanane waliopelekwa Ujerumani wameletwa katika Hopitali ya
Kijeshi ya Walter Reed (karibu na Washington) na wengine tisa wamebaki
huko Ujerumani.”

Maafisa
wa Marekani wanaendelea kukiri hatua kwa hatua juu ya kujeruhiwa
wanajeshi wa nchi hiyo na makombora ya Iran, licha ya hapo awali
kukataa 

Awali
Kamandi ya Jeshi la Marekani Asia Magharibi (CENTCOM) ilidai kuwa 
askari 11 wa nchi hiyo waliojeruhiwa Iraq katika makombora ya Iran
wanatibiwa mjini Landstuhl nchini Ujerumani na katika kambi ya Arifjan
nchini Kuwait.


Masaa
machache baada ya Iran kuvurumisha makombora na kupiga kambi mbili za
Marekani nchini Iraq, Rais Donald Trump alijitokeza mbele ya vyombo vya
habari na kudai kuwa, “ni furaha kuwatangazia Wamarekani kuwa hakuna
askari wetu hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulizi la
makombora la Iran nchini Iraq.”