Na Mwandishi Wetu,
APC Blog, Arusha.
Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyopo Jiji la Arusha imetumia kiasi cha shilingi milioni 82.6 kwa matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Katika taarifa yake ya utendaji kazi ya miezi mitatu kwa waandishi wa habari ofisini kwake leo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Alex Ernest amesema kiasi hicho cha fedha kimetumika kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Dkt. Alex amesema hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wote bila kuangalia uwezo wa kiuchumi hali inayosababisha baadhi yao kutibiwa bure na wakati mwingine kusafirishwa bure pindi wanapopewa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Hospitali hii ni ya umma, Kwa hiyo hatuwezi kumrudisha mgonjwa kwa sababu hana fedha, kupitia kitengo chetu cha ustawi wa jamii tumetoa msamaha kwa wagonjwa 1034 kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo gharama zao ni shilingi milioni 82.6”
Akizungumzia upande wa maboresho yanayoendelea hospitalini hapo amesema zaidi ya shilingi bilioni tano imetolewa na serikali ambazo zitasaidia kuboresha huduma za afya kwa kuongeza majengo ya kutolea huduma pamoja na vifaa tiba.
“Fedha hizi zitasaidia kununua mashine ya CT scan, Digital X-ray, vifaa vya ICT za watoto na watu wazima, ujenzi wa jengo jipya Kwa ajili ya hewa tiba” amesema Dkt Alex.
Amesema kwa sasa wanatumia kuanzia shilingi milioni 60 hadi 80 kwa mwezi kwa ajili ununuzi wa hewa tiba, hivyo ujenzi wa jengo hilo itasaidia kuokoa gharama kubwa.

Amesema wagonjwa wa kansa ambao hadi Sasa wanalazimika kwenda katika hospitali za KCMC ya mjini Moshi na Ocean Road ya Jijini Dar es Salaam wataanza kupata huduma hiyo kuanzia mwezi wa nne mwaka huu baada ya ujenzi wa jengo la kutoa huduma hiyo kukamilika ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 20 Kwa wakati mmoja.
“Pia jengo la damu salama litakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa, kwa sasa sampuli za damu zinapelekwa hospitali ya Kanda ya KCMC Kwa ajili ya uchakataji lakini pia huduma ya upasuaji kwa njia ya matundu itaanza rasmi mwezi wa kumi”.
Amesema upasuaji wa matundu ni njia sahihi na salama kwa wagonjwa kwani haimuachii mgonjwa majeraha mwilini lakini pia humpunguzia muda wa kukaa hospitali pamoja na kupunguza gharama.
Kwa mujibu wa Dkt. Alex magonjwa yanayoongoza kwa wagonjwa wa nje hospitalini hapo ni magonjwa yasiyoambukiza ya kisukari na shinikizo la damu huku wagonjwa wa kulazwa wanaongoza kutokana na ajali za barabarani.
Amesema magonjwa hayo yanaweza kuzuilika kwa kufuata mtindo sahihi wa maisha kwa kula mlo kamili na kwa wakati sahihi, kufanya mazoezi na kuwa na tabia ya kuchunguza afya mara kwa mara.
