Kansela wa Ujerumani Bi. Angel Markel |
Na
Mwandishi Wetu
Matumaini ya
kupatikana chanjo ya virusi vya corona yanazidi kuongezeka baada ya kampuni ya
dawa ya Moderna Inc ya nchini Marekani kusema chanjo yake imeonyesha mafanikio kwa asilimia 94.5
katika kuzuia maambukizi ya COVID-19.
Hayo yanatokea wakati kansela wa
Ujerumani Angela Merkel akitarajia kukutana na mawaziri wakuu wa majimbo 16 ili
kutathmini athari za kufungwa kwa baadhi ya shughuli nchini humo kufuatia
kuongezeka kwa maambukizi. Lilian Mtono anaarifu.
Moderna imesema chanjo yake
imeonyesha mafanikio kwa asilimia 94.5, kufuatia taarifa za awali kutoka kwenye
kampuni hiyo baada ya utafiti unaoendelea. Wiki moja iliyopita, mshindani wake
Pfizer Inc zote za nchini Marekani ilitangaza chanjo yake ya COVID-19 kwamba
nayo imeonyesha mafanikio makubwa.
Taarifa hizo zimeyakutanisha
makampuni hayo kwa pamoja katika mchakato wa kusaka kibali cha matumizi ya
dharura ya chanjo hizo nchini Marekani.
Dokta Stephen Hoge ambaye ni Rais
wa kampuni ya Moderna ameidhibitisha taarifa hiyo na kusema ni hatua muhimu,
akisema kuwepo na matokeo ya kufanana kutoka kwenye makampuni mawili tofauti
ndicho kitu kinachowahakikishia kwamba chanjo hiyo inaleta matumaini makubwa.
Ameliambia shirika la habari la AP kwamba kuna
uwezekano mkubwa kwamba chanjo hiyo italizuia janga hilo na kuna matarajio kwamba
hatimaye Marekani itarudia maisha ya kawaida.
Mtaalamu wa ngazi za juu kabisa wa magonjwa ya
kuambukiza nchini humo Dr. Anthony Fauci amewaambia waandishi wa habari kwa
njia ya simu kwamba chanjo hiyo imeleta mwangaza mkubwa. Fauci hata hivyo
amewaomba Wamarekani kutobweteka na taarifa hizo akiwataka kuendelea kujikinga.
Huku hayo yakiendelea, nchini Ujerumani Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
pamoja na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 ya Ujerumani wanataraji
kufanya tathmini ya athari za hatua ya kusimamisha baadhi ya shughuli iliyodumu
kwa takriban wiki mbili, katika harakati za kukabiliana na kusambaa kwa virusi
vya corona, huku kukitarajiwa kutangazwa vizuizi vipya.
Ujerumani ilichukua hatua ya kufunga baadhi ya
shughuli, mwanzoni mwa mwezi Novemba iliyohusisha kufunga mikahawa na majumba
ya makumbusho lakini tofauti na awali haikuzifunga shule na maduka ya vyakula,
kufuatia kuongezeka kwa kasi kwa virusi vya corona mwezi Oktoba.
Ongezeko la maambukizi mapya imepungua tangu
kuchukuliwa kwa hatua hiyo, lakini siku ya Ijumaa Ujerumani ilirekodi visa
23,542, idadi ya juu kabisa ya maambukizi mapya. Siku ya Jumatatu, taasisi ya
kupambana na magonjwa imerekodi visa vipya 10,824, lakini idadi hiyo mara zote
huwa ni ya chini mwanzoni mwa wiki kwa kuwa hufanyika vipimo vichache mwishoni
mwa wiki na pengine taarifa kuchelewa kufika kituoni hapo.
Kansela Merkel pamoja na magavana
hao 16 pia wanataraji kuanzisha vizuizi vipya, ambavyo ni pamoja na kuvaa
barakoa shuleni pamoja na vizuizi vikali kuhusu mikusanyiko ya nyumbani ili
kukabiliana na wimbi la pili kabla ya sikukuu za Christmas.
Muswada kuhusiana na vizuizi
hivyo ulioonwa na shirika la habari la Reuters umesema watu wataombwa kujizuia
kabisa na mikusanyiko ya sherehe katika kipindi cha wiki zijazo.
Kansela Merkel amenukuliwa na shirika la
habari la Ujerumani la DPA akiwaambia wafuasi wa chama chake cha Christian
Democratic Union, CDU kwamba idadi ya maambukizi inapungua, lakini taratibu
mno.
Kulingana na muswada huo,
wataalamu wa Ujerumani wanatarajia kulikabili janga hilo baada ya majira ya
baridi hasa kwa kuwa kasi yake ya maambukizi imeshuka kutokana na hali ya joto
na pengine kuanza kutolewa chanjo.
Kulingana na muswada huo ambao
hata hivyo unaweza kubadilika kwa kuzingatia mazungumzo kati ya serikali ya
shirikisho na serikali za majimbo 16, mikusanyiko binafsi kwenye maeneo ya umma
huenda ikafanyika tu kwa watu wanaotoka nyumba moja na wengine wawili kutoka
kwenye nyumba nyingine, tofauti na awali ambapo idadi ya juu kabisa ilikuwa
watu 10 kutoka familia mbili.