Mawaziri wa kazi na ajira sadc waipongeza tanzania kutekeleza programu ya ukuzaji wa ujuzi kwa vijana

Na: Mwandishi Wetu

Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Nchi Wananchama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) sekta ya kazi na ajira waipongeza Serikali ya Tanzania kwa mikakati iliyojiwekea katika kuwajengea uwezo vijana kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.

 Pongezi hizo zimetolewa na Mawaziri na Wadau wa utatu wa Jumuiya hiyo ikiwemo Jukwaa la Vyama vya Waajiri Kusini mwa Afrika (SPSF), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Kusini mwa Afrika (SATUCC), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji kanda ya Kusini mwa Afrika (IOM).

Akizungumza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) na waandishi wa habari wakati wa ziara yake aliyoambatana na Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipotembelea Chuo cha Don Bosco Network kilichopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam na Maeneo ya Vivutio vya Utalii Bagamoyo alieleza kuwa Serikali iliamua kuanzisha programu hiyo lengo ikiwa ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuajiriwa au kujiajiri.

“Mawaziri na Wadu wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira wamefurahia kuona namna Serikali inavyotekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuza kwa Vijana ambayo kwa kiasi kikubwa itawawezesha vijana kupata uwezo na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira kwa nchi hizo wanachama,” alisema Waziri Mhagama.

 “Zipo nchi wananachama wameomba kukutana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inatekeleza programu hiyo kwa lengo la kuweza kupata uelewa wa taratibu na namna ya kutekeleza programu hiyo, nchi ya Eswatini tayari imeonyesha nia ya kukutana na ofisi yangu ili nao waweze kuanzisha programu hiyo nchini kwao,” alieleza Mhagama

Alieleza kuwa wakati wa uzinduzi rasmi wa Mkutano huo wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira uliozinduliwa Machi 5, 2020 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Serikali iliona umuhimu wa kuzindua Programu mmoja wapo ambayo ni Programu ya Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi (Internship) ili kuelezea nchi wanachama mikakati ambayo Serikali imejiwekea katika kutatua changamoto ya ajira inayowakabili vijana kwa kuwawezesha vijana kuwa na uzoefu katika utendaji kazi.

Aidha aliongeza kuwa katika mkutano huo uliowakutanisha waliweza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Kazi na Ajira ambazo ni masuala ya Hifadhi ya Jamii, Uhamishaji wa nguvu kazi, mapitio ya sera na miongozo iliyotungwa na nchi wanachama kuhusu masuala ya kazi na ajira, haki na wajibu wa wafanyakazi, mapitio ya mikataba ya kimataifa na mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) inayoongoza masuala ya ajira pamoja na kuwajengea uwezo vijana.

 Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde wakati akielezea kuhusu programu ya ukuzaji ujuzi kwa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira alieleza kuwa Programu hiyo ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inafadhiliwa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha vijana ambao kwa asilimia kubwa ndio nguvukazi ya taifa wanapata ujuzi na uzoefu ambao utawafanya waweze kujitegemea.

“Hii ni habari njema kwa sisi Watanzania kutembelewa na Mawaziri na Wadau wa Utatu ambao wamekuja kujionea namna serikali yetu inavyowajali vijana na jinsi inavyowatumikia katika kuwawezesha kupata ujuzi ambao utawasaidia pindi vijana hao wanapomaliza mafunzo waweze kujiajiri ama kuajiriwa,” alisema Mavunde

 Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu Programu ya Ukuzaji Ujuzi ikiwemo Mafunzo kwa Njia ya Uanagenzi, Mafunzo ya Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi, Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi kwa Wahitimu na Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa walio Makazini na Mpango huo wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior Learning).

Katika ziara hiyo Mawaziri na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na Ajira walipata fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria yaliyopo Bagamoyo ikwemo Ngome Kongwe, Soko la zamani la Watumwa, Bandari iliyokuwa inatumika kuwasafirisha watumwa, eneo la Msalabani ambapo Ukristo ulianzia kuenezwa hapo na wakoloni, Magofu ya Kaole lengo la ziara hiyo ilikuwa kutangaza maeneo ya vivutio vya kihistoria vilivyopo hapa nchini.

Waziri wa Kazi na Ajira Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Ilunga Nkulu Nene alieleza kuwa wamevutiwa sana na maeneo ya kihistoria yaliyopo Tanzania kama vile mji wa kihistoria wa Bagamoyo Pwani, ambayo unaifanya Tanzania iwe nchi ya kuigwa kwa historia ya Nchi za Kusini mwa Afrika.

 “Nchi ya Kongo ina maeneo mengi ya kitalii lakini hatuyatangazi kama Tanzania inavyofanya, kama kiongozi nimejifunza jambo katika ziara ya leo na hivyo nitakaporudi Kongo nitahamasisha utangazaji wa maeneo ya kihistoria yaliyopo kwa lengo la kuvutia watalii,” alisema Nene

Mawaziri wa Kazi na Ajira kutoka SADC waliosimama
mbele wakiwa pamoja na wanafunzi wa mafunzo ya Ufundi katika fani mbalimbali
walioko katika Chuo cha Don Bosco Jijini Dar es Salaam walipotembelea kujifunza
baada ya Mkutano wa Mwaziri wa Kazi na Ajira na Wadau wa utatu wa Nchi za SADC
ulifanyika Machi 5, 2020 JNICC Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenyeulemavu,
Mhe.Jenista Mhagama akiwa na wageni wake(Mawaziri wa Kazi na Ajira Nchi za
SADC) baada ya kutembelea  Ngome kongwe
katika makumbusho ya kihistoria  yaliyoko
Mji wa Bagamoyo walipotembelea baada ya kumaliza Mkutano wa Mwaziri wa Kazi na
Ajira na Wadau wa utatu wa Nchi za SADC ulifanyika Machi 5, 2020 JNICC Jijini
Dar es Salaam, Tanzania.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenyeulemavu,
Mhe.Jenista Mhagama akitoa maelezo kwa wageni wake(Mawaziri wa Kazi na Ajira
Nchi za SADC) mara baada ya kuwasili Ngome kongwe katika makumbusho ya
kihistoria Mji wa Bagamoyo walipotembelea baada ya kumaliza Mkutano wa Mwaziri
wa Kazi na Ajira na Wadau wa utatu wa Nchi za SADC ulifanyika Machi 5, 2020
JNICC Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Waziri
wa Ajira, Kazi, Uzalishaji na Maendeleo ya Ujuzi wa Botswana, Mhe.Mpho Balopi
akipiga ngoma za kikundi cha Utamaduni kutoka chuo cha Sanaa Bagamoyo TASUBA,
kabla ya kutembelea makumbusho ya kihistoria KAOLE Bagamoyo, wanashuhudia
kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Wenyeulemavu, Mhe.Jenista Mhagama na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi.
Zainabu Kawawa.