MAWAZIRI WAONGEZA NGUVU UTEKELEZAJI KAMPENI YA MAMA SAMIA MKOANI ARUSHA.

Na Seif Mangwangi, Arusha

Waziri wa ardhi na maendeleo ya makazi, Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete wameongeza nguvu katika kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia leo 6machi 2025 jijini Arusha.

Wakiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, mawaziri hao wametembelea mabanda mbalimbali kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kukagua utekelezaji wa kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia.

Ndejembi amesema mamia ya wakazi wa Arusha wameshapatiwa msaada wa kisheria tangu kampeni hiyo ilipoanza Machi mosi mwaka huu na bado wanaendelea kupatiwa.

Msaada huo ni sehemu ya maandalizi ya awali kuelekea Machi 08, 2025 wakati Arusha itakapokuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya wanawake duniani.

Wakizungumzia ujio wa mawaziri hao Mama lishe wa Mkoa wa Arusha kwa kauli moja wamesem kutokana na mambo mengi mazuri wanayotaja kufanyiwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na uwezeshaji mkubwa wanaoupata kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda, kwa kauli moja wameeleza kuwa kura zao watampatia Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, amewaomba wananachi wa Arusha Kumuunga mkono Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kumuombea kwa mwenyenzi Mungu kwani amekuwa mstari wa mbele katika kushughulika na maisha ya watu na ustawi wao.

Amesema Rais Samia ameboresha sekta ya mikopo na kuweka utaratibu mzuri wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kunufaika na mikopo.

“Arusha tumependelewa na Mwenyenzi Mungu, tukapembelewa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.Ombi langu kwenu ni kumuombea huyu mama, kumpenda na kumuunga mkono. Yawezekana tungebaki na ule utaratibu wa zamani kuna watu hata msingepata mikopo.” Amesema Makonda wakati akizungumza na Vikundi vya wajasiariamali, wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.

Amesema Rais Samia kupitia Wizara ya TAMISEMI katika maboresho waliyoyafanya kwenye mikopo hiyo ni pamoja na uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za ofisi za wakuu wa mikoa, halmashauri na kata pamoja na kusanifu na kujenga mfumo mpya unaoitwa Wezesha Portal.

Amesema mfumo huo utatumika kwa ajili ya taratibu za ukopeshwaji wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na kujenga uwezo kwa wasimamizi wa mikopo hiyo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.