Mbunge wa rorya lameck airo ashangaa milioni 60 kujenga madarasa mawili

Jengo la madarasa mawili,ofisi moja
shule shikizi ya Mtakuja Kijiji cha Bubombi kata ya Bukura wilayani
Rorya mkoani Mara ambalo ujenzi wake umegharimu milioni 60 fedha
zilizotolewa kwa ufadhili wa Shirika EQUIP.

Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo akizungumza jambo na Abas Amir
ambaye ni Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Bubombi Kata ya Bukura wakati
wa ziara yake 
***
Na Mwandishi wetu,Rorya
Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara Lameck Airo amezitaka Serikali za
Vijiji kusimamia vyema fedha za wafadhili zinazotolewa kujenga miradi ya
maendeleo.
Mbunge Airo alisema kuwa kuna baadhi ya miradi iliyojengwa haiendani na
matumizi halisi ya fedha zitolewazo ukiwemo ujenzi wa shule shikizi ya
Mtakuja Kijiji Cha Bubombi kata ya Bukura.
Shule hiyo imejengwa kwa sh.Milioni 60 kwa ufadhili wa EQUIP ambapo
fedha zake ziliwekwa kwenye akaunti ya shule ya msingi Bubombi Kata ya
Bukura ambayo ujenzi wake ulianza january 2019.
Airo aliyasema hayo mbele ya Viongozi wa Serikali ya kijiji cha Bubombi
baada ya kusomewa taarifa ya matumzi ya milioni 60 ya ujenzi wa shule
shikizi ya Mtakuja ambapo alishangaa kusikia kuwa kiasi hicho kimejenga
madarasa mawili pekee,ofisi moja na choo chenye matundu 6 huku bado
wakihitaji pesa nyingine milioni 6,620,000 kukamilisha ujenzi.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule shikizi katibu wa kamati ya ujenzi
wa shule hiyo ambaye pia ni mkuu wa shule ya msingi ya Bubombi Nelson
Ryaga alisema kuwa mradi wa ujenzi ulianza 2019 kwa kujenga madarasa
mawili ,ofisi moja,vyoo vya wanafunzi matundu manne na vyoo vya walimu
matundu mawili ujenzi uliofadhiliwa na shirika la EQUIP kwa kutoa
milioni 60.
“Ujenzi wa madarasa, ofisi na vyoo umekamilika ila kuna mapungufu
yaliyojitokeza ya kutonunuliwa vifaa kama matenki mawili ya maji yenye
thamani ya shilingi 600,000/=,Water gutters 600,000/=/=,Madawati 20 ya
thamani 500,000/=,saruji mifuko 10 sawa na 200,000/=”,alisema
Rangi lita 60 sawa na 120,000 jumla ikiwa shilingi 2,020,000 pamoja na
shilingi 4,600,000 ambazo shule inadaiwa baada ya kukopa vifaa kwa
mzabuni jumla ya fedha zote pungufu ni shilingi  6,620,000”,aliongeza
Ryaga.
Ryaga alisema kuwa sababu kubwa ya upungufu unatokana na hali ya
Kijiografia ya eneo iliyosababisha gharama kubwa ya ujenzi wa msingi
ikilinganishwa na maelekezo ya B.O.Q,paa ya nyumba kufanyiwa marekebisho
katika upauaji tofauti na B.O.Q pamoja na kutopatikana kwa mchango wa
jamii kushiriki kuchangia nguvu kazi.
Mbunge Airo alisema hajaridhishwa na taarifa hiyo
“milioni 60 kujenga madarasa mawili !nawakati shule zingine tumejenga
darasa moja kwa sh.milioni 15 na linakamilika kila kitu hizo pesa ni
nyingi zilipaswa kubaki kiasi kingine au mngeongeza darasa
lingine”,alisema Airo.
“Tena bado mnasema mmepungukiwa zaidi ya milioni 4 kukamilisha ujenzi,
jamani viongozi wa Serikali ya vijiji simamieni fedha zimeletwa kwenye
akaunti ya shule mnashindwaje kumsimamia mzabuni?kuweni makini na watu
wa halmashauri na wahandisi unaambiwa kanunua vifaa kwa mtu fulani bati
unauziwa 35,000 na wakati hilo hilo kwingine linauzwa 25,000-28,000
 Diwani wewe ndiyo Mwenyekiti WDC unashindwaje kusimamia fedha mpaka mnaingizwa mkenge?”alihoji Airo.
Diwani wa kata ya Bukura Meshack Mamba alisema ujenzi huo umefanywa bila Halmashauri kumshirikisha. 
“Ni kweli milioni 60 haziendani na huu ujenzi halmashauri ilileta
mainjinia na mzabuni sisi hatukuwa na nguvu hatukuhusishwa kwenye
shughuli ilikuwa inasimamiwa na wilaya na mkoa’’,alisema Mamba.
Diwani huyo anaongeza kuwa ujenzi huo ukikamilika na shule kuanzishwa
itasaidia kupunguza umbali wa km.8 kwenda kusoma Bubombi na shule ya
msingi Masonga itapunguza mrundikano shule ya Bubombi yenye wanafunzi
1090 kati ya hao wavulana wakiwa 550 na wasichana 540 na walimu 12,
wanaume 8 na wanawake 4,idadi iliyosababisha kujengwa shule shikizi.