Egidia Vedasto, APC Media Arusha.
Jumla ya Wenyeviti na Wajumbe 920 waliochaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika nchini kote Novemba 27 wametakiwa kuanza kazi mara moja kuwatumikia wananchi ili kuharakisha maendeleo yao.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kwa viongozi hao, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo amewataka kushirikiana na wananchi katika suala la ulinzi na usalama wa Jiji, sambamba na kukomesha vitendo vya rushwa.
Aidha amewakumbusha viongozi hao kusimamia miradi ya elimu, afya na TASAF katika mitaa yao kutokana na uwepo wa pesa zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mchini kote.
“Kumbukeni ahadi mlizoahidi kwenye majukwaa, kwamba mtawatumikia wananchi kwa uaminifu, msinyanyue mabega wala kuwaomba rushwa, bali shirikianeni katika kujadili mambo ya msingi yatakayoleta mageuzi ya uchumi na kijamii kwa muda wote mtakaowatumikia” ameongeza
“Mkawe nguzo na tabasamu la wananchi, mkaisaidie serikali na kutenda kazi kama mnavyotakiwa, mkawe njia ya kumaliza migogoro, na kusimamia ujenzi wa holela ili kujenga Jiji linaloendana na sifa zake” amefafanua Kayombo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Simanjiro Kata ya Sombetini Richard Kivuyo, ambaye amechaguliwa kuongoza kwa kipindi kingine ameahidi kuendeleza ushirikiano na wananchi wake ili kutatua changamoto zilizoshindikana kipindi kilichopita.
“Ninachowaomba wananchi wa mtaa wangu ni kuzingatia kuhudhuria mikutano mbalimbali pindi inapoitishwa, itakayosaidia kuunda sheria ndogondogo za kuchochea maendeleo na kuimarisha ulinzi shirikishi” amesema Kivuyo.
Aidha Viongozi hao wakila kiapo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Jijini Arusha, Salma Mwamende, wameapa kulinda sheria na kanuni za chama na kutotoa siri zinazohusu majukumu yao isipokuwa kwa mujibu wa sheria.