Mkutano wa taasisi za fedha nchini kufanyika arusha novemba 21 & 22, 2019

Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Umoja wa Mabenki Tanzania
(TBA) imeandaa mkutano wa taasisi za fedha nchini utakaofanyika jijini
Arusha kujadili namna ya kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha nchini.



Mkutano
huo wa 19 wa taasisi za fedha unatarajiwa kufunguliwa na kiongozi wa
ngazi ya kitaifa. Utahudhuriwa na washiriki wapatao 300 wakiwemo Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, mawaziri, wakuu wa taasisi za
fedha, wachumi wabobezi, wanataaluma na washirika mbalimbali wa
maendeleo.

Mada
zingine zitakazotolewa na kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na,
‘Matumizi ya teknolojia katika kukuza sekta ya fedha ili kuleta
mapinduzi ya viwanda’; ‘Maeneo yenye fursa za uwekezaji katika sekta ya
fedha’ na ‘Vigezo vinavyochangia kujenga tabia za ukopaji’.

Pia,
washiriki wa mkutano huo watajadili kuhusu ‘Jinsi ya kukinga
vihatarishi katika sekta ya fedha’; ‘Namna ya kuoanisha sekta ya fedha
na maendeleo ya viwanda’; na ‘Tathmini ya mchango wa sekta ya benki
katika huduma jumuishi za kifedha nchini’.

Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikiandaa mikutano ya taasisi za fedha kila baada ya miaka miwili tangu miaka ya 1980. 

Katika
mikutano hii, viongozi wakuu wa taasisi za fedha, yakiwemo mabenki,
mashirika ya bima, mifuko ya hifadhi za jamii na taasisi zingine za
fedha wamekuwa wakikutana na kujadili masuala mbalimbali kwa ajili ya
maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla. Mkutano wa 18
wa taasisi za fedha ulifanyika mwaka 2016 jijini Arusha na mada kuu
katika mkutano huo ilikuwa ni ‘Jinsi sekta ya fedha inavyoweza kuifanya
Tanzania inufaike kiuchumi kutokana na uwepo wake kijiografia’
(Harnessing Tanzania’s Geographical Advantage: The role of financial
sector).