Moto waunguza nyumba na kuua watu wanne

WAKAZI
wa Makueni, Bi Regina Mueni 49, binti yake Faith Mangeli na wajukuu
zake Angel Masava na Amelina Masava wamefariki dunia kutokana na ajali
ya moto iliyoikumba nyumba yao iliyopo maeneo ya soko la Nyunzu maeneo
ya Makueni nchini Kenya.
Katika tukio hilo mama yake Mueni
aliyetambulika kwa jina la Monica Matolo, 75, alipata majeraha kadhaa ya
moto na kukimbizwa hospitali ya rufaa ya Makueni kwa ajili ya matibabu.

Aidha, katika uokozi huo mali za thamani
zilishindwa kuokolewa na zikateketea. Taarifa zinaeleza kuwa nyumba
hiyo ilikuwa na harufu kali ya petroli jambo linaloonyesha kuwa kuna mtu
alihusika kuunguza nyumba hiyo.



Polisi wanamhisi kaka yake Mueni
kuhusika katika tukio hilo kutokana na kuwapo kwa mgogoro wa ardhi wa
kifamilia. Aidha, miili minne iliyokutwa katika tukio hilo ilibebwa na
kwenda kuhifadhiwa mochwari ya hospitali ya rufaa ya Makueni.