-Awataka wajadili adhabu kali itakayokomesha wala rushwa
Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Licha ya jitihada mbalimbali za kuzuia na kupambana na rushwa lakini bado vitendo hivyo vimeendelea kuota mbawa, hatua inayorudisha nyuma jitihada za serikali na kuzorotesha maendeleo ya wananchi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU Jijini Arusha, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wa TAKUKURU kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya kupambana na vitendo hivyo hususan katika maeneo ya ardhi, polisi, ukusanyaji mapato serikali kuu na halmashauri, masuala ya tenda, upatikanaji wa leseni na masuala ya uchaguzi.
Aidha amesisitiza viongozi wote kuonyesha mfano bora katika kuzingatia maadili sheria na kanuni za maadili, kutoa taarifa za kweli za takwimu za mali na madeni, ameongeza kuwa kuna taarifa ya takwimu ya mwaka 2022/2023 inayoonyesha kuwa bado ofisi 50 ambazo hazijaunganishwa na mfumo wa TEHAMA, hovyo kupitia mkutano huo ameshauri wahakikishe mifumo ya TEHAMA inasomana.
“Nasisitiza kwamba, watendaji wote wanaofanya kazi za uchunguzi wa vitendo vya rushwa wapatiwe mbinu za kisasa na mafunzo maalum, watambuliwe na kulindwa wawapo kazini na nje ya kazi, lakini pia msisahau kuwa, kiongozi anatakiwa kuwa mtu asiyetiliwa mashaka katika utendaji na uwajibikaji wake usiobagua juu ya umma, anatakiwa kuwa na utimamu wa akili na uadilifu wa kiwango cha juu” amefafanua Dkt. Mpango.
Amesema kuwa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TAKUKURU ya mwaka 2022/2023 pamoja na mambo mengine wamefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi takriban bilioni 172.3, kukamilisha uchunguzi wa majalada 900, ikiwa uchunguzi wa majalada 21 ya rushwa kubwa yenye thamani ya bilioni 92,245,716,335.50 na dola za Marekani 439, kati ya kesi 496 zilizoamriwa mahakamani ikiwa ni asilimia 67.72% ya kiwango cha kushinda kesi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila amebainisha kuwa lengo la mkutano ni kuangalia utendaji kazi ili kubainisha changamoto na mafanikio, kuweka mikakati ya kupambana na rushwa sambamba na kujadili uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita , ili kuweka mikakati ya kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Vilevile amesema kuwa wamepata mafanikio yaliyotokana na jitihada kubwa za serikali na wadau wengine wa TAKUKURU kupitia mafunzo ya weledi, uwepo wa vitendea kazi na uongozi thabiti uliopo, hatua iliyosaidia kufikia lengo, amesema kutokana na uwezeshaji huo bilioni 18 zimeokolewa na kurudishwa serikalini kupitia operesheni za kazi za uchunguzi kwa kipindi cha miezi 12 kupitia miradi ya maendeleo.
“Tunaendelea kupambana na vitendo vya kupambana na kuzuia rushwa, kupitia warsha, machapisho, elimu kwa vikundi, maonyesho, vipindi vya redio, elimu kwa wanafunzi shuleni na elimu kwa jamii, kuendelea kutoa elimu ni dhahiri kwamba changamoto zisipotatuliwa kwa wakati na zinaweza kusababisha rushwa”,
“Tunaendelea kuchunguza tuhuma za vitendo vya rushwa na kupeleka kesi mahakamani, tuna safari ya kufikia wastani wa juu zaidi ili kupata majawabu kupitia mkutano huu, mada mabalimbali
zitakazowasilishwa, sambamba na hayo tutafanya shughuli za kijamii, kama kutoa damu, kutembelea watoto waliozaliwa kabla ya wakati (njiti) wagonjwa waliokaa muda mrefu hospitali na kupanda miti” amesema Chalamila.
Hata hivyo amebainisha kuwa, wamekuwa wakifanya shughuli zao kwa ushirikiano na kila mmoja kutimiza majukum yake, vyombo vya dola, wanahabari, mahakama na wengine wengi.
Mkuu wa mkoa wa arusha Paul Makonnda amesema wananchi wa mkoa wa Arusha wanataka pesa, hivyo suala la rushwa likidhibitiwa hata mapato ya wananchi yatapanda.
“Unajua suala la rushwa ni mtambuka, hivyo baada ya mkutano huu kuisha natamani mngeenda kila kata ili mhakikishe mnaimaliza rushwa, maana ndio hasa kikwazo cha maendeleo na kurudisha nyuma jitihada za serikali”,
“Ikikupendeza Makamu wa Rais ushirikiane nasi katika siku tatu za maombi ya nguvu kabla ya kumaliza mwaka huu ili tunapoingia mwaka mpya wa 2025 uwe wa baraka na mafanikio, tumeamua kuomba ili Mungu ashughulike na sisi hususan suala la ardhi ambalo watu wengi wanateseka na kuumizwa mfano kudhurumiwa, kutapeliwa na mengine mengi” amefafanua Makonda.
Katika namna hiyohiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalum na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge walio katika Mapambano dhidi Rushwa wa Barani Afrika Tawi la Tanzania George Mkuchika, amewataka viongozi wa TAKUKURU kuwatembelea viongozi wote kuhakiki na kuorodhesha mali zao ikiwa ni njia muhimu ya kubaini vitendo vya rushwa ili kuwachukulia hatua.
Ameongeza kuwa juhudi kubwa zimeendelea kufanyika hadi hatua ya kila wiki kutolewa gazeti lenye taarifa ya waliokamatwa na rushwa, amehimiza elimu kutolewa kwa viongozi ngazi ya wilaya ili kuwafikia wananchi wote, ambapo kwa kiasi kikubwa huko ndiko wananchi wanatafuta haki zao.
“Rushwa inapofusha macho ili watu waendelee kukiuka vitendo vya haki, vitendo vya rushwa vinaongezeka na watu hawaoni aibu kula rushwa, zamani ulikuwa ukijenga nyumba kubwa, unaanza kuwaza kwamba utahojiwa, lakini leo imeonekana ni kawaida wizi wa waziwazi, msisahau nimekuwa Waziri wenu kwa miaka 6, hivyo mimi na Wabunge wenzangu tuataendelea kushirikiana kuzuia rushwa, si hivyo tu bali elimu itolewe kwa taasisi zote na elimu ienezwe kwa wingi katika jamii” amesema Mkuchika.
Mkutano huo utakaofanyika kwa siku nne, umejumuisha Viongozi wakuu wa TAKUKURU 206 na washiriki wengine na kufanya idadi ya kufikia 400 mkutano huo umebeba kaulimbiu “Kukabiliana na Rushwa ni Jukumu Langu na Lako Tutimize Wajibu Wetu”
***************