Na, Egidia Vedasto, APC Media, Arusha.
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo amekabidhi mabati 100 katika Kata ya Ungalimited kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Kata, ahadi aliyoitoa Septemba 2022.Sambamba na tukio hilo la kukabidhi mabati, amefanya ziara katika kata hiyo na kujionea ubovu wa miundombinu na adha kubwa wanayoipotia wananchi.
“Nawaahidi ujenzi wa barabara hizi utaanza hivi karibuni, kwa kuwa taratibu zote zimekamilika, nia ya Serikali yetu ni kuona wananchi wetu wanatumia miundombinu safi inayopitika hata vipindi vya mvua” amefafanua Gambo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Esso Amani Abdallah ameomba suala la barabara hiyo kushughulikiwa haraka ili kuwaepushia wananchi adha wanayopitia kwa sasa.

“Hii barabara imekuwa changamoto kwa muda mrefu, lakini inaonekana chanzo cha ubovu huu ni kwa sababu maji hayajaelekezwa kwenda Mto Ngarenaro, ndio maana inazidi kuchimbika kwa sababu mvua ikinyesha karibu maji yote yanapitia barabara hii” amesema Amani.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Wilfred Soileli ameamuru ujenzi wa barabara hiyo kuanza maramoja ili wananchi waondokane na adha hiyo, ambayo imekuwa gumzo kwa muda mrefu.
“Serikali inafanya kazi kubwa, hivyo na sisi kwa pamoja tushirikiane na kuhakikisha wananchi hawa wanasahau mateso haya wanayoyapitia leo, tunataka watoto waende shule bila kikwazo chochote, vivyo hivyo watumia vyombo vya moto na watembea kwa miguu wote kwa pamoja wafurahie kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita” ameeleza Saileli.
Pia Katibu CCM Kata ya Unga limited Jazira Shaban amefurahishwa na kitendo cha Mbunge kutimiza ahadi yake aliyoitoa miaka mitatu iliyopita.
“Hakika Mbunge wetu ni mfano bora wa kuigwa, hajawahi kuacha kutimiza ahadi zake, kila mwananchi wa kata hii amejionea mabadiliko aliyoyafanya, kubwa kuliko ni shule ya sekondari ya Ungalimited ambayo imejengwa vizuri sana na leo wananfunzi wanapata elimu katika mazingira rafiki” amesema Jazira.

