Mtangazaji maarufu maulid kitenge ‘chumvi’ aipiga chini efm…atua wasafi fm

MTANGAZAJI maarufu wa Habari za Michezo
Tanzania, Maulid Kitenge ‘chumvi’ ameweka wazi kuwa ameachana na Kituo
cha Redio cha EFM na kujiunga Wasafi FM inayomilikiwa na mwanamuziki,
Diamond Platinumz.


Maulid Kitenge alikuwa mtangazaji wa EFM tangu mwaka 2015 akiwa kama
Mkuu wa Idara ya Vipindi vya Michezo, huku akitangaza vipindi vya
michezo vya Sports Headquarters na E-Sport, pamoja na kusoma magazeti
kwenye Kipindi cha Joto la Asubuhi ndani ya EFM iliyoko Kawe Beach
Jijini Dar es Salaam. Katika kile kilichoelezwa kuwa ni sapraizi kwa
mashabiki,jana EFM walimtambulisha msanii, Elizabeth Michael ‘Lulu’
asubuhi kama mbadala wa Kitenge na kuibua gumzo.
Spoti Xtra lilikuwa la kwanza kufichua ishu ya Diamond kumalizana na
Kitenge wiki kadhaa zilizopita walipokutana nchini Marekani kwenye dili
zao. Kitenge ameliambia Spoti Xtra jana kwamba ni kweli ameachana na EFM
juzi Jumanne na amejiunga rasmi na Wasafi FM ambapo atakuwa akikiongoza
Kipindi cha Michezo cha Sports Arena.
Kitenge ambaye amewahi kung’ara na Radio One, aliongeza kuwa, kipindi
hicho kitaanza Jumatatu ijayo na kitakuwa kikiruka hewani kuanzia saa
mbili hadi saa tano asubuhi.
“Ni kweli nimeachana na EFM na nimehamia Wasafi FM ambapo kuanzia
Jumatatu ya wiki ijayo nitakuwa nafanya Kipindi cha Sports Arena ambacho
kitakuwa hewani kuanzia saa mbili hadi saa tano asubuhi, lakini pia
nitakuwa nasoma magazeti kwenye kipindi cha asubuhi saa moja na nusu.
“Katika kipindi hicho nitakuwa na Yusuph Mkule na Mwanaidi Suleiman
ambao nilikuwa nikifanya nao kazi EFM, pia nitakuwa na watangazaji
wengine kama Edo Kumwembe na Ahmed Abdallah.
“Baada ya wiki moja nitakuwa natangaza kipindi kingine cha michezo
kitakachoanza saa moja usiku,” alisema Kitenge ambaye pia ni mchambuzi
wa Gazeti la Championi Ijumaa.
CHANZO ; GLOBAL PUBLISHERS