Mwanamke akamatwa na kadi 23 za benki akiwa amezificha kwenye sehemu zake za siri dar

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam linamshikilia Halima Juma (23), mkazi wa Chalinze mkoani Pwani,
baada ya kudaiwa kukutwa na kadi za ATM 23 alizozificha sehemu za siri.

Imedaiwa na jeshi hilo kuwa alikuwa
anazitumia kuiba fedha katika benki mbalimbali nchini kwa kujitolea
kuwapa msaada watu wasiojua kutumia kadi za ATM, baadaye kuwabadilishia
kadi zao kinyemela.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa,
alidai mbele ya waandishi wa habari jijini jana kuwa, mtuhumiwa huyo
alikamatwa Jumanne kwenye tawi la Benki ya CRDB Mbagala wilayani Temeke.

“Askari wetu walimtilia shaka binti huyu
ambaye wakati huo alikuwa katika chumba cha ATM cha CRDB akijifanya
anawasaidia wazee na wastaafu wasiojua kutumia mashine hizo.

“Lengo lake lilikuwa ni kuchukua namba
za siri zao kisha kuwabadilishia kadi za ATM na baadaye kuwaibia fedha
kwenye akaunti zao kwa kutumia kadi halisi za wahusika baada ya
kuzibadilisha ‘password’ (nywila),” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo
alikamatwa na askari wanaolinda benki hiyo na alipopekuliwa katika
pochi yake aliyoificha sehemu za siri, alikutwa na kadi za ATM 23 za
watu mbalimbali.

“Alikutwa na kadi saba za CRDB, sita za
NMB na benki za NBC, Amana na Posta, ambazo alikutwa na kadi mbili mbili
kwa hizo benki zingine. Pia alikutwa na kadi moja moja za benki za ACB,
Stanbic, DTB na Equity,” alidai.

Kamanda Mambosasa alidai mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na jeshi hilo na atafikishwa mahakamani wakati wowote.

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM KUIMARISHA ULINZI KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.

Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limejipanga vizuri kuhakikisha
uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu.

Ndugu
wana habari, tarehe 24/11/2019 ni siku ya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, Vijiji na Vitongoji hivyo basi sisi kama Jeshi la Polisi
tutaimarisha ulinzi maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam, katika vituo
vya kupigia kura, ofisi zote za vyama vya siasa na ofisi zote za
watendaji wa kata.
Aidha
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa onyo kali kwa mtu
yeyote au kikundi chochote cha watu watakao jaribu kuvuruga amani jeshi
la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA WIZI WA FEDHA KWENYE MASHINE ZA KUTOLEA FEDHA (ATM) NA ATM KADI 23
Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Bi Halima Juma
(23)Mkazi wa Chalinze kwa tuhuma za wizi wa fedha kwenye mashine za
kutolea fedha (ATM)
Mnamo
tarehe 19/11/2019 katika benki ya CRDB tawi la Mbagala akiwa katika ATM
hizo, aidha alimtilia mashaka binti huyo aliyekuwa kwenye chumba cha
ATM ya benki hiyo akijifanya kuwasaidia wazee na wastaafu wasiojua
kutumia ATM mashine vizuri, lakini lengo lake ni kuchukua namba za siri
za wastaafu na wazee hao na kisha kuwabadilishia ATM kadi zao na baadaye
kuwaibia fedha kwenye akaunti zao kwa kutumia kadi halisi za wahusika
baada ya kuwabadilishia kadi na kuchukua namba za siri.
Mtuhumiwa
huyo alikamatwa na askari wanaolinda Benki hiyo na alipopekuliwa
alikutwa na ATM kadi 23 za watu mbalimbali za benki tofauti tofauti
zikiwa katika pochi yake huku akiwa amezificha katika sehemu zake za
siri ukeni.
Kadi hizo ni kama ifuatavyo;
1.CRDB kadi 07
2.NMB kadi 06
3.NBC kadi 02
4.AMANA kadi 02
5.POSTA BENKI kadi 02
6.ACB kadi 01
7.STANIBIC kadi 01
8.DTB kadi 01
9.EQUITY kadi 01
Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani hivi karibuni.

TAHADHARI YA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM.​

Jeshi
la Polisi kanda maalum Dar es salaam linapenda kutoa tahadhari kwa
wakazi wa jiji la Dsm wote kuwa makini kipindi hiki cha mvua
zinazoendelea kunyesha ili kuepukana na majanga yanayoweza kuepukika. 

Hivyo
wananchi wote wanatakiwa kuwa makini na watoto wadogo wanaohitaji
uangalizi wa karibu, pia kujiepusha kupita kwenye maji ya mito
midogomidogo au madimbwi ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
Aidha hadi sasa zimepokelewa taarifa za watu wawili kufariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

LAZARO .B. MAMBOSASA – SACP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM.